• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 5:55 AM
KIKOLEZO: Maceleb ombaomba

KIKOLEZO: Maceleb ombaomba

NA SINDA MATIKO

ILE dhana kuwa maceleb ni watu wenye uwezo, ushawishi mkubwa, matajiri, wanaishi maisha ya staha na anasa, imekataliwa na matukio fulani.

Unaweza ukalaumu umma kwa kuwa na dhana hiyo lakini pia nao maceleb wana kila sababu ya kulaumiwa.

Imeshuhudiwa wengi wao wanapokuwa katika nafasi hizi hujibeba kama miungu, lakini maisha yanapotokea na kuwapunguza spidi, wanaishia kunyenyekea.

Mitandao ya kijamii pia wameitumia sana kutaka kuionyesha jamii jinsi wanavyoishi maisha hayo.

Lakini kama wasemavyo Waswahili, ving’aavyo vyote si dhahabu. Katika miaka ya hivi karibuni hasa toka janga la corona lizuke, maceleb kadhaa ghafla wamegeuka na kuwa omba omba.

Wale waliodhaniwa hawana ukoo na shida za fedha, ndio wamejitokeza kuomba mashabiki na umma msaada wa kifedha. Kinaya ni kuwa, wakati baadhi yao wakijitokeza kuomba misaaada, wenzao walioko kwenye kiwanda kimoja wanaonekana kushamiri.

Kinachobakia ni swali tu, je walishindwa kujipanga, au kweli makubwa yaliwakuta? Pengine kupata picha, itakuwa sawa kushuka na kesi hizi za maceleb omba omba.

CONSUMATOR

Mvunja mbavu Peter Wamwea ndiye celeb wa hivi karibuni kujitokeza kuomba umma msaada.

Consumator alijipatia umaarufu wake alipochipukia pale Churchill Show. Lakini juzi kaibuka akiwa katika hali mbaya na kuwapigia magoti wananchi akiomba msaada.

Kulingana naye maisha yamekuwa magumu sana kiasi kwamba amejikuta akiwa mwana vibarua. Ule utanashati tuliomfahamu nao haupo tena. Anafanya vibarua ili kuishi. Consumator amedai sababu ya yeye kusota ilitokana na babake alipougua saratani ya kibofu 2019 na kumpelekea kutumia fedha nyingi ikiwemo akiba zake kwenye matibabu yake.

Baada ya mwaka huo uliofuatia ikazuka janga la corona lililositisha shoo alizokuwa anategemea kuingiza kipato.

“Ilifika sehemu nikashindwa kulipa kodi na nikaenda kuishi na rafiki yangu Zimmerman. Makubaliano yakawa ni kwamba tutachangiana kulipa kodi. Mwanzoni mambo yalikuwa mazuri lakini baadaye nikaanza kulemewa kulipa kodi. Ilifika sehemu nikashindwa kabisa na rafiki yangu akanichuja. Iliniuma sababu ni kitu kilichonifedhehesha kwa kuwa kwenye ploti ile nilikuwa najulikana kama “Consumator”, kaungama.

Kwa sasa anawaomba mashabiki na umma wamsaidie ili aweze kurejea kwenye hali yake ya zamani.

AKUKU DANGER

Ni mchekeshaji mwingine aliyejikuta kwenye hali mbaya. Mannerson Oduor Ochieng, jina lake halisi, aliibukia kwenye Churchill Show. Jina lake la stejini ni la marehemu babu yake maarufu Akuku Danger aliyekuwa na wake zaidi ya mia na watoto wanaotosha kujaza shule tatu za sekondari.

Aprili mwaka jana kuliibuka taarifa kuwa jamaa kafukuzwa kwake baada ya kushindwa kulipa kodi. Hii ilitokana na video moja iliyosambaa ikimwonyesha akitupiwa virago vyake nje. Lakini alijitokeza na kusema haikuwa kweli, maisha yake yapo sawa na kwamba alikuwa na kipato kinachomtosheleza. Alikwenda zaidi na kufafanua kwamba ile ilikuwa video aliyounda kuelezea masaibu wanayopitia Wakenya wengine. Aidha alisema video hiyo imempelekea kupata fedha kutoka wahisani alizopania kuwasaidia wasiojiweza nazo.

Lakini kuelekea mwisho wa mwaka jana, Akuku alijipata kwenye hali mbaya akilazwa hospitalini baada ya mapafu yake kufeli. Akuku alilazwa mara mbili kwenye chumba cha wagonjwa wenye hali mahututi. Bili za hospitali zikawa kubwa mno. Aliishia kuwaomba msaada mashabiki kumsaidia kugharamia bili yake ya hospitalini ya zaidi ya Sh1.5 milioni.

JUSTINA SYOKAU

Ndiye mwanamuziki kutoka Ukambani aliyewashika watu na hiti yake ya ‘Twendy Twendy’. Hata kabla ustaa umshike vizuri, Syokau alianza kulalamikia ugumu wa kimaisha na kuwaomba mashabiki wamsaidie.

2020 kupitia Facebook, alidai maisha yamekuwa magumu sana na kwamba hana pesa za kuwarai mashabiki wamchangie ili asikwame. Michango kadhaa ilifanyika kumsaidia.

Msanii Justina Syokau. PICHA | CHRIS ADUNGO

Lakini Januari 2021, Justina alijitokeza tena na kuomba msaada upya akisema hali yake ni mbaya. Hii ni licha ya kuwa alipochipuka aliweza kupata dili kadhaa za kibalozi

RUTH MATETE

Aliwahi kushinda Sh5 milioni kupitia shindano la Tusker Project Fame, lililompa umaarufu 2012.

Ingawaje miaka hiyo maisha hayakuwa magumu sana kama sasa, Matete alishindwa kujipanga vizuri na fedha hizo na badala yake akaamua kuwa na matumizi mabaya.

Mwisho wa siku ziliisha na akabaki hana kitu. Aliwahi kukiri kutaka kujitoa uhai wake taarifa zilipotoka kuwa kasota.

Ruth Matete. PICHA | MAKTABA

Maisha yaliendelea na 2019 akafunga ndoa kabla ya mume wake kufariki katika njia ya kutatanisha ndani ya miezi mitano kwenye ndoa yao. Baada ya miezi kadhaa, Matete alijitokeza na kuomba umma msaada wa kifedha ili aweze kumlea mtoto wake aliyekuwa tumboni babake alipofariki. Matete alikiri kupitia kipindi kigumu cha kifedha huku akisisitiza kuwa alikuwa akimtegemea sana mume wake.

ALVAN LOVE GATITU

Mwanamuziki huyu ni miongoni mwa wacheshi wakubwa kwenye TikTok. Naye alichipukia Tusker Project Fame, shindano lililomfungulia milango mingi ya nuru.

Lakini Juni 2020 mwanamuziki huyo aliposti video akielezea masaibu yake ya kushindwa kulipa kodi. Gatitu alisimulia jinsi alivyofungiwa nyumba na landilodi baada ya kulemewa kulipa kodi. Aliomba michango na kwa siku chache akachangiwa zaidi ya Sh2 milioni.

OMOSH KIZANGILA

Kamau Kinuthia alipata umaarufu mkubwa kupitia kipindi cha Tahidi High alikoigiza. Enzi za maigizo, Omosh aliwahi kukiri kwamba ilikuwa kawaida yake kuangukia dili za fedha nyingi kiasi kisichopungua Sh150,000. Hata hivyo, alikiri tabia zake za ulevi zilimfanya ashindwe kuwekeza au kuweka akiba. Lakini kubwa hata zaidi ilikuwa ni matunzo ya familia yake kubwa ya wake wawili. Tahidi High ilipofikia kikomo, maisha yakawa shubiri kwa msela. Aliwahi kukiri kuwa ilifika hatua aligeuka na kuwa omba omba ‘kazi ilikuwa kupiga luku na kutoka kwenda kuzurura’. Utakuwa unaikumbuka meme hiyo iliyoundwa kutokana na kipande cha video aliyorekodiwa akieleza masaibu yake.

Kisa cha Omosh kiliwagusa watu wengi waliojitokeza na kumchangia fedha ikiwemo kumnunulia uwanja na kumjengea nyumba. Lakini taarifa zinadai kuwa Omosh amekuwa kwenye harakati za kutaka kuiuza nyumba ile ili kuendeleza uraibu wake wa pombe.

SWALEH MDOE

Licha ya jamaa kuwa mtangazaji mkubwa na anayelipwa fedha nyingi, miaka kadhaa iliyopita alijitokeza na kukiri kalemewa kifedha. Alikwenda hatua zaidi na kuomba usaidizi kutoka kwa umma.

Mdoe alikiri kuwa na madeni mengi yaliyokuwa yakimkaba koo.

Mwanahabari Swaleh Mdoe. PICHA | MAKTABA

Baada ya kuona hapati ujanja, alijitokeza na kusema yupo tayari kuuza moja ya figo zake kwa nusu milioni ili kumwezesha kulipa madeni yake.

LOUIS OTIENO

Ni mtangazaji mwingine maarufu wa zamani aliyegeuka na kuwa omba omba. Enzi ya nyota ya utangazaji wake, aliishi maisha ya kistaa kwenye majumba ya kifahari katika mitaa ya nguvu jijini Nairobi. Katika miaka ya nyota yake, Louis alikuwa ndiye mtangazaji wa runinga aliyekuwa akilipwa mkwanja mrefu zaidi.

Maisha yake yalikwama alipokumbwa na skendo ya mauaji na kuishia kuchujwa kazi katika runinga ya KTN. Kabla ya kuwa mtangazaji aliwahi kufanya kazi katika Shirika la Posta kabla ya kujisuka na kupata fursa KBC kisha KTN wakamchukua.

Baada ya kuchujwa, Louis hakuwa amejipanga, maisha yakawa magumu sana kwake. Februari 2018 aliugua na baada ya kulazwa, aliwaomba Wakenya msaada wa kifedha kugharamia matibabu yake.

JEMUTAI

Mchekeshaji mwingine wa Churchill Show aliyewashtua wengi ni Jemutai aliyejitokeza mara ya kwanza mwaka 2021 na kutangaza anauza akaunti yake ya Facebook kwa Sh1.7 milioni.

Alisema anaiuza akaunti yake ili kuweza kupata pesa za kuwalea watoto wake baada ya hali kuwa ngumu kufuatia janga la Covid.

Kilikuwa kipindi kigumu ambacho pia alifichua kwamba mzazi mwenza mchekeshaji Profesa Hamo aliyemzalisha watoto hao wawili, alikuwa hatoi matunzo.

Mnunuzi alipokosekana, Jemutai aliwaomba Wakenya msaada wa kifedha kugharimia mahitaji ya wanawe.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamme ashindwa kulipa chakula cha hoteli Sh15,350

Man-City kuzindua mnara wa Sergio Aguero ugani Etihad mnamo...

T L