• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Man-City kuzindua mnara wa Sergio Aguero ugani Etihad mnamo Mei 13, 2022

Man-City kuzindua mnara wa Sergio Aguero ugani Etihad mnamo Mei 13, 2022

NA MASHIRIKA

MANCHESTER City watazindua mnara wa aliyekuwa mwanasoka wao Sergio Aguero mnamo Mei 13, 2022, miaka 10 tangu nyota huyo raia wa Argentina awafungie bao lililowawezesha kunyanyua taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2011-12.

Hiyo ilikuwa mara ya kwanza tangu 1968 kwa Man-City kutia kapuni ubingwa wa EPL.

Kwa mujibu wa taarifa ya Man-City, usimamizi wa klabu hiyo umepania kumtunuku Aguero mnara huo kwa kuwa ni miongoni mwa wanasoka nguli katika historia ya kikosi chao.

Mnamo Mei 2012, Aguero alifunga bao mwishoni mwa muda wa ziada dhidi ya Queens Park Rangers (QPR) na kutwalia Man-City taji la EPL katika siku ya mwisho ya kampeni za kipute hicho.

Mnara wa Aguero umetengezwa na mchoraji maarufu raia wa Scotland, Andy Scott, na utawekwa karibu na minara ya wachezaji Vincent Kompany na David Silva waliowahi kucheza pamoja na Aguero ugani Etihad.

Jumla ya mashabiki 2,000 wa Man-City watapata fursa ya kuhudhuria hafla ya kuzinduliwa kwa mnara huo wa Aguero. Hafla hiyo itahudhuriwa pia na baadhi ya masogora waliokuwa sehemu ya kikosi kilichoshindia Man-City taji la EPL mnamo 2011-12.

Aguero, 33, aliagana rasmi na Man-City mnamo Juni 2021 na kuyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Barcelona kabla ya kustaafu baada ya mfupi kutokana na matatizo ya moyo.

Hadi alipoondoka ugani Etihad, alikuwa amefungia Man-City jumla ya mabao 260 na kunyanyulia kikosi hicho mataji matano ya EPL, Kombe la FA na ubingwa wa League Cup mara sita chini ya kipindi cha miaka 10.

Aguero ni miongoni mwa wachezaji wa kigeni (wasio wazawa wa Uingereza) wanaojivunia kufunga idadi kubwa ya mabao katika soka ya EPL. Alipachika wavuni jumla ya magoli 184, tisa zaidi kuliko yale ambayo Mfaransa Thierry Henry aliwahi kufungia Arsenal. Waingereza Alan Shearer (260), Wayne Rooney (208) na Andrew Cole (187) ndio wanaongoza orodha ya wafungaji bora wa muda wote katika historia ya kivumbi cha EPL.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

KIKOLEZO: Maceleb ombaomba

Gonzalo Higuain kustaafu soka mwishoni mwa msimu huu wa...

T L