• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 6:50 AM
KIKOLEZO: Maisha na mikasa ya nguli Tedd Josiah

KIKOLEZO: Maisha na mikasa ya nguli Tedd Josiah

NA SINDA MATIKO

NILIMKUTILIZA Edmond Josiah almaarufu Tedd Josiah, akiwa anajipangapanga kwenye makao yake mapya yaliyopo mtaa wa kifahari wa Runda.

Ni siku chache toka alipohamia kwenye mjengo huu wa ghorofa wenye vyumba vya kutosha. Pembeni kuna mjengo mkubwa ambao kaugeuza kuwa kiwanda cha kutengeneza mabegi yake ya ngozi JokaJok Leather.

KWA NINI ALIACHA MUZIKI

JokaJok ndio biashara yake mpya inayomwingizia mtaji tangu aamue kuacha muziki, sanaa aliyodumu nayo kwa zaidi ya miongo mitatu.

“Hamna haja ya kuendelea kuandaa muziki wakati hamna malipo yoyote niliyopata kwa hiti zote hizo nilizotengeneza,” Tedd Josiah ananiambia.

Kabla ya Insta, Facebook na mitandao mingine ya kijamii ikiwemo YouTube iliyozinduliwa Kenya 2009, Josiah alihusika kwenye utengenezaji wa hiti kibao zilizovuma toka 1995 hadi 2005.

Ngoma kama vile Unbwogable, Bless ma room, Kenyan Boy Kenyan Girl, Tafsri Hii, Tension, Uhiki, Kisumu 100, Megarider, Atoti, 4 in 1, Msichana Mwafrika na nyingi nyinginezo.

Tedd ndiye produsa aliyechipua manguli wa zamani wa kizazi kipya kina Nameless, Nazizi, Wyre, Gidi Gidi Maji Maji, Hardstone, Dirge miongoni mwa wengine waliohiti enzi hizo.

“Nazizi nilipata kumjua kupitia marehemu mjombake Emile Juma akiwa na umri wa miaka 15 tu. Gidi Gidi na Maji Maji nilipokutana nao kwenye shoo moja, walikuwa ni maadui wakubwa ila niliwaambia kama wanataka kufanya kazi na mimi, basi ni lazima washirikiane kwa sababu staili yao ya uimbaji ilifanana.”

Emile alikuwa ni msomi wa muziki baada ya kupata mafunzo hayo kule Marekani. Aliporejea nchini na kugundua msela ana ujuzi mdogo wa kuprodyuzi muziki, alimchukua na kumpa mafunzo zaidi na hapo akampevusha hata zaidi Josiah.

Hata hivyo, miaka hiyo muziki haukuwa unalipa na Tedd anasema walitegemea zaidi wahisani.

“Kulikuwa na kampuni nyingi kama Salama Condoms, Close Up ambazo zilikuwa zinatudhamini. Hiti tulizokuwa tukitengeneza zilivutia halaiki na ili kuwateka, kampuni zikalazimika kushikana nasi.”

Utandawazi baadaye ulikuja ukabadilisha mambo na pia muziki ukachukua mkondo tofauti.

“Naamini kabisa kama wasanii tungelikuwa tunalipwa haki zetu kupitia mirabaha basi mpaka leo ningekuwa natengeneza muziki tena hiti kali ukizingatia tekinolojia ya kisasa. Niliamua kuachana na muziki 2007 baada ya kuona haulipi.”

KIBAKI AMTIMUA NCHINI

2002 Ted aliandaa hiti ya Unbwogable iliyotumiwa na Mwai Kibaki kwenye kampeni zake akiwa na sapoti ya Raila Odinga kwenye harakati za kumaliza utawala wa Rais Daniel Moi. Moi alikuwa ameteua Uhuru Kenyatta kuwa mrithi wake.

Wimbo huo ukamfanya Ted na kina Gidi Gidi na Maji Maji kuwa maarufu. Josiah akaanza kupata dili kibao za kutengeneza video za biashara matangazo.

Kwenye uchaguzi wa 2007, alitenegeneza video ya biashara matangazo Domo Domo ya kumpigia debe Raila Odinga ambaye safari hii alikuwa ndiye mpinzani wa Kibaki.

“Tangazo hili lilizua tumbojoto sana baada ya kuvuma sana kiasi cha marehemu Lucy Kibaki kutishia. Nilianza kuona nafuatwa na watu nisiowajua na siku moja nikiwa nimeshuka kwenye gari naelekea kwenye afisi yangu nilitekwa na watu nisiowajua. Kwa bahati nzuri ilikuwa sehemu ya wazi na mabaunsa wangu wakawa wepesi kuzua tukio lililowafanya wale majamaa watoweke.”

Kilichofuatia ni Ted kuipiga vumbi pasipoti yake na kutimkia zake London, Uingereza.

“Nilijua nikiendelea kuwa Kenya, na hali ilivyokuwa, kulikuwa na uwezekano mkubwa ningeuawa.”

NDOA YAVUNJIKA, KIFO CHA MKE

Wakati anaondoka, nyuma aliiacha ndoa yake na Cynthia Akoth ikiwa juu ya mawe. Tayari ndoa ilikuwa ishaingia mdudu na kuondoka kwake, kukachangia kuvunjika kwa ndoa hiyo kabisa.

Kwa miaka mitano, Tedd aliishi majuu hadi 2015 aliporudi Kenya akiwa na uhakika sasa kuwa mambo yametulia.

“Baada ya kurudi nilijaribu kuanzia lebo ya SwaRnB nikamsaini msanii Masauti na baada ya kumtengenezea hiti moja akatoweka.”

Hapo akaamua kuifunga lebo baada ya kuona ni biashara ambayo haingelipa. Ni kipindi hicho ambapo alikuja kukutana na marehemu mkewe Regina Katar.

Ni mwanafesheni Regina ndiye alimtambulisha kwenye masuala ya fasheni na hata kumpa wazo la kuanzisha kampuni ya kutengeneza bidhaa za ngozi.

Mahaba yao yalikuwa mazito mno ila hayakudumu. Septemba 30, 2017 Regina aliaga dunia ikiwa ni miezi mitatu tu baada ya kujifungua mwana wao Jameela Wendo.

AACHWA HOI NA KINDA

Ted anakiri huku akijitahidi kubana machozi yanayomlenga kwamba, kumlea Jameela toka akiwa na miezi mitatu hadi sasa ana miaka saba kuwa jukumu nzito sana na lililomwacha hoi.

“Sikujua nini cha kufanya, umeachiwa mtoto mchanga ambaye muda wote analia na hujui nini cha kufanya. Niliamua sitaoa sababu nilitaka kuhakikisha nampa muda wote mwanangu na pia ndiye hunipa kumbukumbu za marehemu kipenzi mke wangu.

Ili kumuenzi Katar, hapo aliamua kuanzisha JokaJok ambayo kimsingi kiunganishi cha majina yao matatu.

“Nashukuru kwamba biashara kwa sasa imenoga ila kubwa zaidi JokaJok ni urithi mahususi ninaokusudia kumwachia Jay Jay (Jameela). Muda wangu utakapofika, huu ndio urithi nitakaomwachia, ambayo ni kumbukumbu ya safari yetu sote watatu.”

  • Tags

You can share this post!

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Umuhimu wa vazi la hijabu kwa...

KASHESHE: Miaka 10 akiwa singo na hajuti

T L