• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
KIPWANI: Baada ya mishemishe Nairobi, amerejea nyumbani Mombasa

KIPWANI: Baada ya mishemishe Nairobi, amerejea nyumbani Mombasa

NA SINDA MATIKO

MASHARIKI au Magharabi, Kusini au Kaskazini nyumbani ni nyumbani tu.

Mwaka 2021 mwigizaji msupa Brenda Wairimu alipofanya uamuzi wa kurudi nyumbani, alifanya kwa kusudi.

Mwanzo alitaka kurudi nyumbani ili kuyatoka maisha ya kasi ya Nairobi lakini pia, alitaka unafuu wa maisha na hata zaidi kuwa karibu na familia yake.

Inaeleweka kuwaona wengi wakishangaa wanapogundua kuwa Brenda anatokea Mombasa. Huko ndiko nyumbani, huko ndiko kitovu chake kilikozikiwa, huko ndiko alikulia na kulelewa. Nairobi alikoishia kupata umaarufu wake, alikuja tu kusaka maisha. Umaarufu huo alianza kuupata 2011 alipotokea katika kipindi cha Mali kilichopeperushwa na runinga ya NTV.

Kisha umaarufu huo ukaongezeka alipoingia kwenye mahusiano na rapa Juliani ambaye walijaliwa mtoto wa kike Amor. Kwa sasa Juliani ni mume wake Lilian Ng’ang’a.

Wengi hushangaa wanapogundua unatokea Pwani?

Nimezaliwa na kulelewa Mombasa, sema wakati jina langu laja kujulikana, nilikuwa nikipiga mishemishe zangu Nairobi.

Kuwa mwigizaji, ilikuwa ndoto au tukio tu?

Wala haikuwa ndoto yangu. Kama usemevyo, ilikuwa tukio tu. Ajali vile. Haikuwa kitu cha kupanga. Ndio, niliigiza nilipokuwa kidato lakini nikaja kuachana na mchakato huo nilipoingia kidato cha tatu sababu nilihitaji muda zaidi wa masomo.

Kwa hiyo hata kuigiza huko chuoni, ilikuwa kusukuma muda?

Inawezekana ikawa hivyo. Si wajua tena maisha ya shuleni yalivyo? Sikuwahi kuwa na mawazo hayo kabisa ni hali tu ndio iliyonipelekea nikajikuta huko.

Hali ipi hiyo shangazi?

Nilipojiunga na Chuo Kikuu cha USIU kusomea Biashara, ndiko safari yangu ya uigizaji ilipoanzia.

Nilikuwa namtegemea mamangu tu na mara nyingi maisha yalikuwa magumu sana kwetu. Mama alikuwa na ugumu wa kunipa hela za matumizi sababu hakuwa na uwezo mkubwa.

Ilifikia wakati nilichoka kumwomba mwomba mama hela kila mara na hapo nikaamua kuanza kujihangaikia. Hii ikawa hatua yangu ya kwanza kujikuta kwenye uigizaji.

En-hee! Ikawaje?

Nakumbuka siku moja kwenye pita pita zangu niliona bango lililotoa mwaliko kwa waigizaji kwenda kwenye usajili wa kipindi cha Changing Times.

Nikawashtua mashoga zangu, hao sisi tukatinga eneo kujaribu bahati zetu. Nakumbuka kulikuwepo na zaidi ya watu 800 waliofika kwenye usajili. Nilipaniki kidogo ila sikufa moyo. Wiki moja baadaye nikamwona Size 8 kwenye episodi moja ya kipindi hicho cha Changing Times. Hapo nikajijazia kuwa sikufuzu sababu naye nilikuwa nimemwona kwenye auditions halafu kipindi hicho alikuwa tayari ameanza kupata jina. Wiki mbili baadaye nikiwa tayari nimeshayaondoa mawazo yangu pale, nikapokea simu kuwa nahitajika kwenye uhusika mpya wa kipindi hicho. Safari hiyo ikaanza.

Wakati jina lako limeanza kutambulika, zilikuwepo tetesi zilizodai urembo wako ulikubeba, ulizisikia?

Haha! Ndivyo tulivyo binadamu. Tunapenda kujaza susu kwa yasiyo tuhusu. Mwanzo wakati naanza kuigiza, mwenyewe sikuwa najua chochote kabisa. Sio kwamba nilikuwa najua kuigiza. Jinsi ya kuzungumza, jinsi ya kwenda na matukio na mambo mengi tu ya sanaa hii sikuwa nafahamu. Wengi walinikashifu sana na ndiko tetesi hizo zilikochipukia. Ila sikufa moyo, kila nilipo kashifiwa, nilijitahidi kurekebisha mapungufu hayo hadi mwishowe nikawa mkali wao. Jitihada zangu zilijipa nilipoteuliwa kuwania tuzo za Kalasha na hapo ndipo produsa wa Mali aliponiona na kunialika nikapata uhusika wa Lulu. Mali ndicho kipindi kilichonifungulia milango ya nuru na kheri, baada ya hapo kazi zikawa zinanifuata tu. Nikaishia kupata kazi nyingi za uigizaji kiasi cha kunifanya nikose muda wa masomo. Mwaka wa 2014 nikaamua kusitisha masomo yangu chuoni.

Aisee ulikuwa uamuzi mzito huo, kuacha masomo?

Sikuacha, nilisitisha. Wajua baada ya Mali kazi zilianza kuja kwa fujo. Shoo hizi tulikuwa tunashuti kutwa nzima, muda wa vitabu ningeutoa wapi?

Isitoshe, mshahara ulikuwa mzuri sana, singeachia pesa zinipite hivyo eti kwa sababu ya masomo ukizingatia ule ugumu niliokuwa nimeupitia na mama. Nilijiambia bora masomo yasuburi nipige mpunga kwanza.

Kwa ufanisi uliopata ni kwa nini uliamua kujiengua kwenye gemu?

Zipo sababu kadha wa kadha zilizonipelekea kusita kuigiza. Nahisi kuwa mshahara ninaolipwa hauendani kabisa na uwezo au mchango ninaoutoa. Uigizaji ni kujituma na unapokosa kulipwa inavyotakiwa unaweza ukashindwa. Hii ni moja tu. Kazi zipo nyingi ila sio nyingi zinazofikia dau langu. Lakini pia nilihitaji muda wangu wa kupumzika na kuwa karibu na familia yangu.

Kwa hiyo mishe mishe kwa sasa ni zipi?

Nina mambo mengi tu ninayoyafanya ya kuniingizia kipato toshelezi lakini pia niliamua kurudi nyumbani Mombasa ambapo maisha sio magumu sana kama yalivyo kule Nairobi. Stresi nyingi nimepunguza na presha. Maisha huku sio kama ya Nairobi. Ni nafuu na hayakwendi kwa kasi sana. Kutokana na hilo ninaweza kuchagua nini cha kufanya bila ya kuwa na presha.

Mwonekano wako pia umebadilika, umenenepa kidogo?

Haha! Acha tusema stresi za Nairobi hizo zimeniondokea. Ila nafikiri kwa sasa nipo sehemu nzuri zaidi karibu na familia yangu na pia kisaikolojia.

Nimeishi kuwa na mwili mdogo tangu zamani ila kazi za uigizaji na kuwa kwenye mahusiano yalichangia zaidi kunikondesha. Hizi presha ndio sasa sina kabisa ndio pengine kidogo naonekana tofauti.

Unamaanisha rapa Juliani au kuna mwingine?

Hehe! Tuyaache maisha yalishasonga.

Wengi tuliamini kabisa yenu yangeishia kwenye ndoa, miaka saba pamoja sio mchezo?

Mbona mng’ang’anizi wewe. Lakini ndivyo maisha yalivyo, tulijitahidi lakini ikatokea ilivyotokea. Nilijitahidi kufanikisha uhusiano ila kilichokuwa kikinikera ni kuwa kila nilipokuwa nachambwa, hakuwa akinitetea. Ukimya wake ulinivunja sana sababu naamini alistahili kunitetea. Lakini pia zile tetesi za kuchepuka alizinyamazia.

Lakini msela huwa anakusifia sana?

Si jambo la kheri hilo, tuna mtoto pamoja.

Vipi mahusiano mapya?

Mahusiano yalinichosha. Sipo mpweke kabisa. Niligundua ninapokuwa kwenye mahusiano, huwa najitoa sana muhanga kwenye mapenzi ila sipati mapenzi hayo kwa kiwango ninachotoa mimi.

Maisha ya kuwa singo nafuu. Hayana presha.

You can share this post!

Wolves wasema anayetaka kiungo wao Ruben Neves sharti aweke...

Kibarua cha Azimio Mombasa

T L