• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 2:19 PM
Wolves wasema anayetaka kiungo wao Ruben Neves sharti aweke mezani Sh15.6 bilioni

Wolves wasema anayetaka kiungo wao Ruben Neves sharti aweke mezani Sh15.6 bilioni

Na MASHIRIKA

KOCHA wa Wolverhampton Wanderers, Bruno Lage, ametaka klabu za Barcelona, Liverpool na Manchester United zinazowania huduma za mwanasoka Ruben Neves kuweka mezani Sh15.6 bilioni ndipo kiungo huo abanduke ugani Molineux.

Mkataba wa sasa kati ya Wolves na Neves ambaye ni raia wa Ureno unatarajiwa kutamatika rasmi mnamo 2024. Sogora huyo mwenye umri wa miaka 25 amefungia Wolves mabao manne kutokana na mechi 31 katika mashindano yote msimu huu.

“Ni mchezaji spesheli ambaye hatutaki kabisa aagane nasi. Lakini iwapo atahiari kuondoka kwa matarajio kwamba hatua hiyo itamkuza zaidi kitaaluma na kumwezesha kufikia ndoto zake katika ulingo wa soka, basi kikosi kitakachomtwaa lazima kitoe Sh15.6 bilioni,” akasema Lage.

Lage alipokezwa mikoba ya Wolves mwishoni mwa msimu wa 2020-21 baada ya mkufunzi Nuno Espirito Santo kubanduka ugani Molineux na kuyoyomea kambini mwa Tottenham Hotspur alikohudumu hadi Novemba 2021 kabla ya nafasi yake kutwaliwa na Antonio Conte.

Neves aliingia katika sajili rasmi ya Wolves mnamo 2017 baada ya kuagana na FC Porto ya Ureno kwa Sh2.5 bilioni.

Lage aliwahi kupoteza sogora tegemeo kambini mwake kwa kiasi kikubwa cha fedha baada ya kuruhusu Joao Felix kuagana na kilichokuwa kikosi chake cha Benfica nchini Ureno na kuyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Atletico Madrid.

“Nilitamani sana kusalia na Felix kambini mwa Benfica. Lakini ofa ya Sh13.4 bilioni iliwekwa mezani na Atletico na tukashawishika kumwachilia,” akasema mkufunzi huyo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Bukayo Saka ndiye mwanasoka bora barani Ulaya miongoni mwa...

KIPWANI: Baada ya mishemishe Nairobi, amerejea nyumbani...

T L