• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 10:44 AM
Kibarua cha Azimio Mombasa

Kibarua cha Azimio Mombasa

WINNIE ATIENO NA VALENTINE OBARA

MUUNGANO wa Azimio la Umoja- One Kenya, unaoongozwa na kinara wa ODM Raila Odinga, unatarajiwa kukumbwa na kibarua kigumu katika mpango wa kushirikiana kusimamisha mgombeaji mmoja wa ugavana katika Kaunti ya Mombasa.

Hii ni baada ya Mbunge wa Kisauni, Bw Ali Mbogo, kukabidhiwa tikiti ya Chama cha Wiper kuwania wadhifa huo.

Kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka ambaye ni kinara mwenza wa muungano huo, alidokeza kuwa Kaunti ya Mombasa ni miongoni mwa zile ambazo zinazingatiwa kuwa na mgombea mmoja wa Azimio kwa ugavana.

Kulingana naye, Mkurugenzi Mkuu wa Azimio, Bw Raphael Tuju, ndiye atasimamia kikundi cha wawakilishi wa vyama tanzu ambao watashauriana kuhusu mipango hiyo.

Bw Musyoka alisema Bw Tuju, ambaye alitangazwa rasmi kushikilia wadhifa huo Jumatano, atasaidiana na makatibu wakuu wa vyama vingine ambao ni Shakila Abdalla (Wiper), Edwin Sifuna (ODM), Jeremiah Kioni (Jubilee) miongoni mwa wengine.

“Tunataka kuangalia hali zote ili tuamue kwa mfano Nairobi, Nakuru na Mombasa muungano ukubaliane kuhusu mgombeaji mmoja na mgombea mwenza katika wadhifa wa ugavana. Haya ni masuala ya mikakati inayolenga kutuongeza idadi ya ushindi,” akasema.

Katika Kaunti ya Mombasa, ODM inasubiriwa kutangaza rasmi atakayepewa tikiti baada ya kubainika kuwa, Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, aliibuka mwenye umaarufu zaidi katika kura za maoni zilizodhaminiwa na chama hicho.

Bw Nassir anashindania tikiti hiyo dhidi ya mfanyabiashara Suleiman Shahbal, ambaye amepinga mpango wa chama kupeana tikiti ya moja kwa moja.

Chama kingine tanzu cha Azimio la Umoja ambacho kimemsimamisha mgombeaji ugavana Mombasa ni Pamoja African Alliance (PAA), ambacho mgombeaji wake ni Naibu Gavana, Dkt William Kingi.

Bw Mbogo alikabidhiwa tikiti ya Wiper kuwania ugavana Jumatano.

Katika hafla hiyo iliyofanywa Nairobi, Bw Musyoka alieleza kuwa, Bw Mbogo ndiye anastahili kurithi kiti cha Gavana Hassan Joho.

“Ameletea chama chetu cha Wiper fahari kubwa. Hatuna shaka kuwa yeye ndiye mgombeaji anayefaa zaidi kwa kiti cha ugavana Mombasa na tunamuunga mkono,” akasema Bw Musyoka.

Bw Mbogo alisema kupewa tikiti kumempa motisha na msukumo wa kuendeleza mbele kampeni zake za kutaka kukomboa wakazi wa Mombasa kutokana na uongozi mbaya.

“Nilitunukiwa tikiti ya moja kwa moja kwa sababu sikuwa na mpinzani kwenye chama chetu. Nimeshahitimu, sasa ni kwenda uwanjani kusaka kura,” akasema Bw Mbogo.

Hivi majuzi, viongozi wa Jubilee walitangaza kuwa chama hicho hakitakuwa na mgombeaji ugavana Mombasa bali wataunga mkono mgombeaji atakayedhaminiwa na Azimio la Umoja-One Kenya.

Wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Jubilee katika kaunti hiyo, Bi Hazel Katana, walisema watakuwa na wagombeaji viti vingine isipokuwa urais na ugavana.

Endapo mtindo huo utatumiwa katika kaunti nyingine za Pwani, kibarua kitakuwa katika Kaunti ya Taita Taveta ambapo Jubilee imemsimamisha Gavana Granton Samboja kutetea kiti chake, huku ODM kikiwa na Bw Thomas Mwakwida, na Wiper kikimsimamisha aliyekuwa seneta, Bw Dan Mwazo.

Katika Kaunti ya Kilifi, ODM inasubiriwa kutangaza rasmi atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwa uchaguzi wa ugavana, huku PAA ikiwa na wakili George Kithi.

ODM inatakiwa kutangaza mgombeaji wake kati ya aliyekuwa waziri msaidizi wa ugatuzi, Bw Gideon Mung’aro, Spika wa Bunge la Kaunti ya Kilifi, Bw Jimmy Kahindi, na Naibu Gavana Gideon Saburi.

  • Tags

You can share this post!

KIPWANI: Baada ya mishemishe Nairobi, amerejea nyumbani...

Wasiwasi wakongwe wakitakiwa kuhama

T L