• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 6:50 AM
Kitendawili cha barakoa

Kitendawili cha barakoa

NA PAULINE ONGAJI

WIKI moja baada ya shule kufunguliwa – baada ya wanafunzi kukaa nyumbani kwa muda wa miezi kumi kufuatia janga la virusi vya corona – wazazi wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kusimulia visa kuhusu watoto wao na barakoa shuleni.

Baadhi ya wazazi wamekuwa wakielezea jinsi watoto wao, haswa wanaosoma chekechea na Gredi 1, wamekuwa wakirejea nyumbani jioni na barakoa za rangi tofauti na walizoenda nazo asubuhi.

“Mtoto wangu alitoka na barakoa ya rangi ya bluu asubuhi lakini alirudi jioni na nyeupe. Sijui kilichofanyika shuleni. Ni maombi tu,” akaandika Mercy Aoko katika mtandao wa Twitter.Naye John Wanyoike alisema kuwa bintiye anayesoma chekechea alirejea nyumbani bila barakoa licha ya kwenda nayo shuleni asubuhi.

“Mwanangu anayesoma ‘Play Group’ (darasa la kuwaandaa watoto kujiunga na chekechea) alirejea na barakoa mbili jioni na nilipojaribu kumhoji aliniambia kuwa alipewa moja na rafiki yake. Lakini barakoa aliyodai kupewa ilikuwa tayari imevaliwa!” akaelezea Evans Makori kupitia Facebook.

Visa hivyo ni ithibati kuwa kuna changamoto kubwa ya kuhakikisha kuwa watoto wanavalia barakoa shuleni ili kupunguza maambukizi ya virusi vya corona shuleni.

Evelyne Musyoka anayefundisha watoto wa ‘Play Group’ katika shule ya Wonderland, mtaani Kahawa West jijini Nairobi, anakiri kuwa amekuwa na kibarua kigumu kuhakikisha kuwa watoto wanavalia barakoa wakati wote wanapokuwa shuleni.

Anasema kwamba huwa anatumia wakati mwingi kuwakumbusha kuvalia barakoa, kutokaribiana na kunawa mikono mara kwa mara.“Ni kibarua kigumu kuhakikisha kuwa wanavalia barakoa kila wakati. Vilevile, kuna changamoto kubwa kuwazuia kukaribiana wanapokuwa shuleni ili kuwakinga na maambukizi ya corona,” anasema.

Kabla ya kufunguliwa kwa shule wiki iliyopita, waziri wa Elimu Prof George Magoha alisema kuwa hakuna mtoto anayefaa kwenda shuleni bila barakoa.

“Hakuna mwanafunzi ambaye atafukuzwa kutokana na ukosefu wa karo, lakini hakuna mwanafunzi ataruhusiwa kusoma bila kuwa na barakoa. Wazazi wanunulie watoto wao barakoa. Kuanzia sasa barakoa itakuwa sehemu ya sare ya shule,” akasema Prof MagohaNi agizo hilo la Prof Magoha ambalo limesababisha baadhi ya shule kuwarejesha nyumbani wanafunzi wanaofika bila barakoa.

Wizara ya Elimu haijatoa mwongozo kuhusu umri wa watoto ambao hawafai kuvalia barakoa.

Suala la Umri

Umri ambao watoto hawafai kuvalia barakoa limesalia suala la mjadala kote duniani.Mnamo Juni, mwaka jana, Prof Magoha alitoa mwongozo ambapo alisema kuwa watoto wa chini ya umri wa miaka sita hawakufaa kuvalia barakoa endapo shule zingefunguliwa Agosti 1, 2020.

Lakini siku chache kabla ya shule kufunguliwa Januari 4, mwaka huu, waziri huyo wa Elimu aligeuka na kuagiza kuwa ni sharti kila mtoto; kuanzia chekechea hadi Kidato cha Nne, avalie barakoa.

Kaimu mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Kuzuia Maradhi Dkt Pacifica Onyancha, mnamo Juni mwaka uliopita, alifafanua kuwa watoto wa chini ya umri wa miaka miwili ndio pekee hawafai kuvalishwa barakoa.

Dkt Onyancha alisema kuwa watoto wa umri wa kati ya miaka 2-5 hawafai kuvalia barakoa wanapokuwa katika ndani ya gari la kibinafsi au peke yao nyumbani.

Mwongozo uliotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mnamo Agosti mwaka jana, unasema kuwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano hawafai kuvalia barakoa.

“Hili linatokana na ukweli kwamba ni vigumu kuwalazimisha watoto wa chini ya umri wa miaka mitano kuvalia barakoa kila wakati. Vilevile, kuna uwezekano wa barakoa kutatiza ukuaji wa watoto,” linasema shirika la WHO.Shirika hilo la Umoja wa Mataifa (UN), hata hivyo, lilikiri kuwa uamuzi wa kuwataka watoto wa chini ya umri wa miaka mitano wasivalie barakoa ulitolewa bila kuwa na ushahidi wowote unaotokana na utafiti wa kisayansi.

“Wataalamu wetu waliafikia uamuzi huo baada ya kukubaliana kuwa miili ya watoto hukua kwa kasi wanapokuwa chini ya umri wa miaka mitano. Wakivalia barakoa kwa muda mrefu huenda ukuaji huo ukatatizika,” linasema shirika la WHO.

Badala yake shirika la WHO linapendekeza kuwa njia mbadala kama vile kunawa mikono na kuwatenganisha zinafaa kutumika kuhakikisha kuwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano hawaambukizani corona, haswa wanapokuwa darasani.

“Endapo baadhi ya nchi zitaamua kuwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano wavalie barakoa, basi kunafaa kuwa na uangalizi wa karibu kuhakikisha kuwa hawadhuriki. Lakini mbinu mbadala zinaweza kutumika kudhibiti maambukizi miongoni mwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano badala ya kuwavalisha barakoa,” unaelezea mwongozo wa WHO.

Aidha WHO linapendekeza kuwa watoto wa zaidi ya miaka 12 wanastahili kuvalia barakoa kila wakati sawa na watu wazima.Kituo cha Kudhibiti Maradhi (CDC) kinapendekeza kuwa ni watoto wa umri wa chini ya miaka miwili tu ndio hawafai kuvalishwa barakoa.

CDC pia inapendekeza kuwa watoto walio na ugonjwa wa pumu (asthma) na matatizo mengineyo ya kiafya yanayosababisha ugumu wa kupumua pia hawafai kuvalishwa barakoa.“Watoto walio na ulemavu au wasio na uwezo wa kujitoa barakoa puani bila kusaidiwa pia hawafai kuvalishwa,” unasema mwongozo wa CDC.

Nchini Uingereza, si lazima watoto wa chini ya umri wa miaka 11 kuvalia barakoa shuleni. Nchini humo wanafunzi wa shule za sekondari ndio wanatakiwa kuvalia barakoa mara kwa mara.

Barakoa pia si lazima kwa wanafunzi wa umri wa miaka 11 nchini Ufaransa. Wanafunzi wanaruhusiwa kutangamana wanapokuwa shuleni ila sharti wawe wachache. Madawati na vifaa vingine ambavyo huguswa mara kwa mara na wanafunzi vinanyunyiziwa dawa ya kuua virusi angalau mara moja kwa siku.

Oksijeni

Wataalamu wa afya wamepuuzilia mbali madai ya kupotosha ambayo yamekuwa yakisambazwa katika mitandao ya kijamii kuwa watoto au vijana wanapovalia barakoa, ubongo hushindwa kukua vyema kutokana na uhaba wa oksijeni.

Utafiti uliofanywa na wanasayansi wa nchini Amerika mnamo Julai mwaka jana ulibaini kuwa hakuna ushahidi wa kuthibitisha kuwa barakoa inasababisha ubongo kukosa oksijeni ya kutosha.

Kulingana na CDC, barakoa ni salama kwa watoto na watu wazima.“Kuvalia barakoa ndio njia salama ya kupunguza maambukizi ya virusi vya corona,” kinasema kituo cha CDC.

WHO linashauri kuwa watoto wa chini ya umri wa miaka 12 wasio na matatizo ya kiafya wavalie barakoa zilizotengenezwa kwa kipande cha nguo (fabric).Barakoa zilizojulikana kama ‘surgical’ zinafaa kuvaliwa tu na watoto walio na matatizo ya kiafya kama vile kisukari.

Mwongozo wa WHO pia unahitaji watoto wasivalie barakoa wanapocheza uwanjani ili zisiwazuie kupumua vyema.“Wakati wa michezo, wanafunzi hawafai kukaribiana na walimu wahakikishe kuwa watoto wananawa mikono mara kwa mara,” unasema mwongozo wa WHO.

Tafiti ambazo zimefanywa nchini Amerika, Sweden na Norway zimebaini kuwa kuna kiwango cha chini cha maambukizi miongoni mwa wanafunzi wa chekechea.Ili kuepuka visa vya kubadilishana barakoa shuleni, mtaalamu wa masuala ya saikolojia ya watoto Dkt Dorcas Magai, anasema kuwa wazazi au walimu wanafaa kuhakikisha kuwa wanawapa watoto barakoa za rangi wanazopenda

.“Mnapoenda kununua barakoa, basi mwachie mtoto achague rangi ya barakoa anayohitaji. Hii ni kwa sababu ukimnunulia rangi asiyoipenda akifika shuleni anabadilishana na mwenzake,“Mtoto anaposhirikishwa katika kuchagua barakoa ataipenda na ataivalia bila kumezea mate za wenzake,” anasema Dkt Magai.

Anasema kuwa mzazi au mwalimu anastahili kuchukua hatua mtoto anapolalamika kwamba hahisi vyema anapovalia aina fulani ya barakoa.

“Mtoto akilalamika kwamba anafinywa na barakoa au hahisi vyema mzazi au mwalimu anastahili kuchukua hatua aibadilishe sio kumlazimisha kuivaa. Ukimlazimisha kuivaa ataitoa akifika darasani na haitakuwa imesaidia,” anaelezea.

Mtaalamu huyo anasema kuwa wazazi wanafaa kumvalisha mtoto barakoa ambayo inamtoshea vyema. Barakoa inayompwaya inaweza kumletea usumbufu wa kuirejesha mara kwa mara.

“Aidha, wazazi au walimu wanafaa kujadili suala la kuvalia barakoa na watoto ili wafahamu umuhimu wake. Watoto wakielewa kwa nini wanavalia haitakuwa rahisi kwao kuitoa,” anasema.

Walimu

Tofauti na mwongozo wa wizara ya Afya kuwa walimu sharti wavalie barakoa wakati wote wanapokuwa darasani, shirika la WHO linasema kuwa walimu wanafaa kuvalia tu wanapokuwa karibu na wanafunzi.

Mwongozo wa WHO unasema kuwa mwalimu anapokuwa umbali wa zaidi ya mita 2 kutoka kwa watoto anaweza kufundisha watoto bila kuvalia barakoa.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Illinois ulibaini kuwa walimu wanapovalia barakoa zilizotengenezwa kwa vitambaa kama vile vitenge, wanafunzi wanakuwa na ugumu wa kusikia anachozungumza.

Watafiti waligundua kuwa barakoa za vitambaa zinapunguza sauti hivyo kusababisha wanafunzi kushindwa kusikia anachosema.Watafiti walipendekeza kuwa walimu wawe wakitumia barakoa zinazojulikana kama N95 au ‘surgical’ ambazo zimebainika kuwa hazizuii sauti.

You can share this post!

Sijali kupigwa kalamu, afoka Kang’ata

Jinsi ya kujitengenezea chokoleti nyumbani