• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:47 PM
GWIJI WA WIKI: Justina Syokau

GWIJI WA WIKI: Justina Syokau

Na CHRIS ADUNGO

MWANGWI wa kueneza Ukristo, kusisitiza uadilifu na kupigia chapuo makuzi ya Kiswahili ni jambo linaloakisika katika nyimbo za Injili ambazo Justina Syokau huzifyatua kwa mtindo wa Benga.

Kitambulisho chake katika ulingo wa muziki ni ufundi wa kutumia lafudhi ya lugha yake ya kwanza (Kikamba) bila kuathiri ujumbe anaowasilisha kwa Kiswahili.

“Hiki ni kipaji nilichokitambua udogoni. Nilitia azma ya kukitononoa na walimu wakanipa majukwaa ya kukipalilia. Nilikuwa mcheshi darasani na upekee huo ukanifanya maarufu miongoni mwa wenzangu shuleni,” anasema.

Syokau alizaliwa katika eneo la Mua Hills, Kaunti ya Machakos. Ndiye wa tatu katika familia ya watoto watano wa Bw David Nzomo na marehemu Bi Mary Nzomo.

Alisomea katika Shule ya Msingi ya Mua Farm kisha Shule ya Upili ya Aman Bright Future Academy, Machakos. Baada ya uchechefu wa karo kumzimia mshumaa wa elimu, alisalia nyumbani kuchoma makaa, kuuza kuni na kukuza sukumawiki kabla ya kuelekea Nairobi halafu mjini Eldoret kufanya kazi ya uyaya.

“Kwenda jijini kulinipa fursa ya kutangamana na vyombo vya habari mara kwa mara. Nilihimizika kujitosa katika tasnia ya muziki baada ya kusoma kadhia za wasanii niliowastahi magazetini na kutazama wengi wao runingani.”

Baada ya machafuko ya kisiasa ya 2007-2008 kumtoa Eldoret, Syokau alielekea Kijabe alikopata kibarua katika hospitali ya AIC Kijabe. Alitoa albamu yake ya kwanza yenye vibao vinane ‘Mwachie Yesu’ mnamo 2009.

“CD za muziki huo zilinunuliwa kwa wingi Kimende, Naivasha na Nakuru na nikamfungulia mamangu biashara ya nafaka, mboga na matunda.”

Syokau alipitia misukosuko tele baada ya kuolewa na kuhamia Nairobi kuishi na mumewe.

Ndoa ilivunjika baada ya mwaka mmoja na akatemwa siku saba baada ya kujifungua.

“Japo wahisani walinichangia nauli ya kurejea Mua Hills, presha ya kulaumiwa na wazazi pamoja na kejeli za wanakijiji hazikuniweka nyumbani kwa muda. Nilirudi Nairobi kuendeleza muziki na kuhudumu kanisani.”

Kufikia sasa, Syokau anajivunia vibao 92 ambavyo amevihifadhi katika albamu saba zikiwemo ‘Future Nzuri’, ‘Nataka Kuishi’, ‘Ng’ang’ana’, ‘Mama’ na ‘2021 Mwaka wa Lestolation (Restoration)’.

Wimbo ulimkweza zaidi kwenye chati za muziki na kumzolea sifa kedekede ni ‘Twendi Twendi’ aliofyatua muda mfupi baada ya kutoa ‘Kilisimass’ mnamo Disemba 2019. Miongoni mwa vibao vingine maarufu ambavyo amevicharaza ni ‘Neno la Yesu’, ‘Liliz (Release)’, ‘Nimerudi’, ‘Tujikinge na Corona’ na ‘Najileta Kwako’.

Syokau amepata mialiko mingi ya kuandaa shoo nchini Amerika, Uingereza, Ujerumani, Canada, Namibia, Tanzania na Afrika Kusini.

Zaidi ya kuwa mwimbaji, yeye pia ni mhubiri, mvumishaji wa bidhaa za kampuni mbalimbali na mshauri nasaha. Aliandika kitabu ‘Arise and Manifest your Potential’ mnamo 2015. Aidha, anaendesha kampeni maalumu ya kusambaza sodo na vyakula kwa mayatima pamoja na kuwalipia karo kupitia mpango wa Justina Hope Initiative. Azma yake ni kupigana na ukeketaji, ndoa za mapema na dhuluma dhidi ya wanawake.

You can share this post!

Aguero astaafu soka kwa sababu ya matatizo ya afya

Tanzania: Vidokezo vinne vya kuzuia kutapeliwa malipo yako...

T L