• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:24 PM
Man-United wasitisha mazungumzo ya kurefusha mkataba wa Lingard ugani Old Trafford, kulikoni?

Man-United wasitisha mazungumzo ya kurefusha mkataba wa Lingard ugani Old Trafford, kulikoni?

Na MASHIRIKA

MUSTAKABALI wa kiungo Jesse Lingard kambini mwa Manchester United sasa umezingirwa na suitafahamu baada ya kikosi hicho kusitisha mazungumzo kuhusu uwezekano wa kurefusha mkataba wake.

Kandarasi ya sasa kati ya Man-United na kiungo huyo raia wa Uingereza inatamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu wa 2021-22 na yalikuwa matarajio ya kocha Ole Gunnar Solskjaer kushuhudia sogora huyo akiendelea kuwa sehemu ya mipango yake ugani Old Trafford.

Ushawishi na mchango wa Lingard umehisika pakubwa kambini mwa Man-United muhula huu tangu aagane rasmi na West Ham United waliojivunia huduma zake kwa mkopo mnamo 2020-21.

Licha ya kuwania na vikosi sita tofauti vya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) muhula huu, Lingard alihiari kusalia kambini mwa Man-United kwa matumaini kwamba angepata uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza.

Badala yake, amewajibishwa katika kikosi cha kwanza cha Man-United mara moja pekee kufikia sasa muhula huu – dhidi ya West Ham United kwenye EFL Carabao Cup mnamo Septemba 2021. Aidha, amewajibishwa mara saba akitokea benchi kwa jumla ya dakika 76.

Ina maana kwamba Lingard amechezea timu ya taifa ya Uingereza mara nyingi zaidi mwaka huu kuliko Man-United licha ya kukosa kuwa sehemu ya kikosi kilichotegemewa na kocha Gareth Southgate dhidi ya Albania na San Marino katika michuano ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mnamo 2022 nchini Qatar.

Man-United wamepangiwa kuchuana na Watford katika mchuano ujao wa EPL kabla ya kupimana ubabe na Villarreal kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kisha kumenyana na Chelsea katika gozi kali ligini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Quincy Rapando

KASHESHE: ‘Siri ya ndoa kunyenyekea’

T L