• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
NBC: Chama cha Uanahabari katika shule ya Upili ya Ndalani, eneo la Matuu

NBC: Chama cha Uanahabari katika shule ya Upili ya Ndalani, eneo la Matuu

Na CHRIS ADUNGO

CHAMA cha Uanahabari cha Ndalani Broadcasting Corporation (NBC) sasa ni jukwaa mwafaka zaidi kwa wanafunzi wa Shule ya Upili ya Ndalani katika eneo la Matuu, Kaunti ya Machakos kuchapukia somo la Kiswahili.

Chama hiki kilichoanzishwa na mwalimu Titus Okello mnamo 2014, kilipata mwamko mpya mnamo 2016 baada ya wanachama kuanza kutangaza habari gwarideni kila Jumatatu na Ijumaa.

Miongoni mwa malengo makuu ya NBC ni kuwa mstari wa mbele kukuza na kulea vipaji vya wanafunzi katika sanaa mbalimbali pamoja na kuwaamshia hamu ya kujitosa katika taaluma za uanahabari, ualimu, tafsiri, ukalimani na uhariri wa vitabu.

Mwalimu Okello anahisi kwamba NBC ni chombo imara kinachotoa fursa kwa wanafunzi kujifahamisha masuala yanayofungamana na mazingira yao kitaifa na kimataifa kila wanapokusanya habari kuhusu masuala ibuka na matukio muhimu ndani na nje ya shule na kuziwasilisha gwarideni.

Mbali na kuzidisha maarifa ya utafiti katika masomo ya lugha, chama pia kimechangia kuvusha wanafunzi katika masuala ya kiakademia. Wanapokutana kila Jumatano kuanzia saa kumi hadi saa kumi na moja jioni ili kujadili mikakati ya kuendeleza NBC, wanachama pia hutumia vikao hivyo kuzamia baadhi ya mada zinazowatatiza katika somo la Kiswahili chini ya uelekezi wa viongozi wao – Newton Bonge (Mwenyekiti), Peter Ngundi (Katibu) na Faith Neema (Mhazini).

Mbali na kuanzisha kitengo cha uigizaji kitakachorahisisha ufundishaji na ujifunzaji wa Fasihi Andishi, chama pia kinalenga kuchapisha jarida rasmi la NBC. Kufaulu kwa mpango huo chini ya udhamini wa Mwalimu Mkuu Bi Jane Gateri Wainaina, kutawapa wanafunzi nafasi ya kutononoa vipaji vyao vya uhariri na uandishi wa kazi bunilizi.

Kufikia sasa, matunda ya chama yameonekana. Wanafunzi ambao ni wanachama wa NBC wamekuwa wakifaulu vyema katika Kiswahili na kuwapiku wenzao wanaochangamkia zaidi masomo mengine.

“Chama pia kinapania kuchochea maadili miongoni mwa wanafunzi na kuboresha matokeo ya mitihani ya kitaifa ya kidato cha nne (KCSE) kupitia usomaji wa gazeti la Taifa Leo kila Alhamisi,” akaongeza Bw Okello.

You can share this post!

Inshallah nchi yetu iwe na amani zaidi mwaka 2022

Ploti ya Onyesho la Kwanza tendo la tatu katika tamthilia...

T L