• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 7:52 PM
MWALIMU WA WIKI: Okwalo ni mtunzi na mwalimu stadi

MWALIMU WA WIKI: Okwalo ni mtunzi na mwalimu stadi

Na CHRIS ADUNGO

JOHN Okwalo Wambani alianza kuvutiwa na ualimu akiwa mtoto mdogo.

“Walimu walikuwa watu wa kustahiwa katika jamii na walikuwa wamepiga hatua kubwa kimaendeleo. Ualimu ilikuwa, na bado ni kazi yenye hadhi na tija,” anasema.

Bi Kendeli na Bw Andrew Shikanda waliomfundisha Okwalo katika Shule ya Msingi ya Mumias Complex ndio walimvuvia mwanafunzi wao huyu hamu ya kuzamia taaluma ya ualimu.

Mwingine ni Bw Peter Murabula Lumonya aliyemtanguliza vyema katika sanaa ya utunzi wa mashairi katika Shule ya Upili ya Nambale Boys, Busia.

Mashairi ya Okwalo yalivutia kutokana na ubunifu na ufundi uliodhihirika katika matumizi yake ya lugha. Alikuwa maarufu miongoni mwa wanafunzi wenzake waliompagaza lakabu ‘Malenga Ibuka’.

Mnamo 2009, Okwalo alitunga shairi lililoibuka la kwanza katika Mkoa wa Magharibi na la tatu kitaifa katika tamasha za muziki na drama zilizoandaliwa Pwani ya Kenya.

Anakiri kuwa mtaala mpya wa umilisi (CBC) una nafasi kubwa katika kukuza umilisi wa wanafunzi kwa kuegemea zaidi katika upekee na ukubwa wa uwezo wao ndani na nje ya darasa.

Mbali na kujenga utaifa, uzalendo na umoja wa kitaifa, CBC inalenga kumkuza mwanafunzi ili hatimaye afikie maendeleo ya jamii kitamaduni, kiuchumi, kiteknolojia na kiviwanda. Ni mpango unaosisitiza maendeleo ya mtu binafsi ili ajitegemee katika maisha ya baadaye.

“Inakuza wanafunzi kimaadili na kuwachochea kutambua umuhimu wa usawa na uwajibikaji katika jamii. Pia inawajengea msingi wa kuelewa mawanda mapana ya jamii ya kimataifa na umuhimu wa kuzikumbatia tamaduni za wanajamii wengine,” anasema.

Okwalo alizaliwa katika kijiji cha Bubere, Mumias Mashariki, Kakamega. Ndiye wa tatu katika familia ya watoto wanne wa Bw Moses Wambani na Bi Gladys Namenya Mwanga.

Alianza masomo katika chekechea ya Mawang’i, Malaha (1994-1995) kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Sikinga, Busia (1996-1997). Alisomea baadaye katika Shule ya Msingi ya Mumias Complex (1998-2002) kabla ya kujiunga na St Mary’s Nambale alikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) mnamo 2003.

Baada ya kusomea katika Shule ya Upili ya Nambale Boys (2004-2007), alijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Nyanchwa Adventist, Kisii (2009-2011).

Alijitosa katika ulingo wa ualimu mnamo 2011. Alifundisha Olympic Junior Academy, Kisii hadi Septemba 2014 kabla ya kuhamia Malaba Railways Academy. Akiwa huko, aliamsha ari ya kuthaminiwa kwa sanaa miongoni mwa wanafunzi. Moto wa masomo ulirindima na mikwiro ikapiga ngoma ya Kiswahili kwa kani na idili.

Mnamo Februari 2015, aliajiriwa na Shule ya Msingi ya Ridgesview Academy, Naivasha. Msukumo wa kufanya kazi karibu na nyumbani ulimchochea kuguria Booker Academy Mumias mnamo Julai 2016.

Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimwajiri mnamo Agosti 2017 na kumtuma kufundisha katika Shule ya Msingi ya Suwo, eneo la Matungu, Kakamega. Alihamia katika Shule ya Msingi ya St Peter’s Mumias mnamo 2019.

Ndiye mkuu wa hati na mratibu wa somo la maktaba katika Idara ya Kiswahili.

You can share this post!

PAUKWA: Biashara Haramu ya Titi (sehemu 5)

Gor yarejea kileleni, Vihiga Bullets ikisimamisha AFC

T L