• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 5:50 AM
PAUKWA: Biashara Haramu ya Titi (sehemu 5)

PAUKWA: Biashara Haramu ya Titi (sehemu 5)

Na ENOCK NYARIKI

“KWENU ni wapi?’’ afisa kwenye zamu katika kituo cha polisi alimuuliza Machugachuga.

“Masosa. Kwetu ni Masosa katika kaunti ya Nyamira,’’ Machugachuga alieleza.

“Umetoka mbali hivyo kuja kufanya biashara ya kuuza pombe haramu?’’ ni kama yule askari alimuuliza, ni kama alimsuta.

Machugachuga alijitetea kwamba yeye alikuwa msaidizi wa Titi aliyeimiliki biashara hiyo haramu. Maneno yake hayakumsadikisha afisa yule ambaye alimwambia kinaganaga, “Anayepatikana na ngozi ya ng’ombe ndiye mwizi.’’

Alipofikishwa katika mahakama ya Sotik Mjini, kijana yule alishtakiwa kwa makosa mawili. Alipatikana na hatia ya kutengeneza na kusafirisha pombe haramu ya chang’aa. Hukumu ya makosa hayo ilikuwa faini ya shilingi elfu tano au kifungo cha miezi sita jela. Alikuwa mgeni katika mji wa Sotik hivyo basi hakumfahamu jamaa wala rafiki ambaye angemlipia faini aliyotozwa. Alihiari kutumikia kifungo.

Miezi sita gerezani ilionekana mingi. Ilikuwa sawa na miaka sita. Hata hivyo, jela haikuwa mahali pa adhabu tu bali pia kwa kuirekebisha na kuibadili tabia yake iliyokuwa imefanya ufa.

Ni humu gerezani ambamo alijifunzia kozi fupifupi ikiwamo ile ya useremala. Alidhamiria kuutumia ujuzi ambao angeupata kuanzisha mradi wa kujikimu kimaisha siku ambayo neema ingemfungulia milango.

Falsafa moja aliyojifunza wakati wote alipokuwa gerezani ni kuwa ni heri mtu kula makapi kuliko kuvunja sheria. Milango ya jela ilipomtanulia viganja; ishara kwamba sasa alikuwa mtu huru alifurahi ukomo wa furaha.

ITAENDELEA

You can share this post!

ELIMU MSINGI: Binti mfumaji mazulia

MWALIMU WA WIKI: Okwalo ni mtunzi na mwalimu stadi

T L