• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 10:36 AM
Maajabu mwanamuziki akila mlo kwenye sahani moja na mbwa  

Maajabu mwanamuziki akila mlo kwenye sahani moja na mbwa  

Na SAMMY WAWERU  

CAROL Mwaura, mwimbaji wa nyimbo za injili amewasha mjadala moto mitandaoni kufuatia video anayoonekana akila chakula kwenye sahani moja na mbwa.

Tukio la msanii huyo wa nyimbo za Kikuyu, limegeuka kuwa gumzo la mitandao wachangiaji wakishangazwa na tabia hiyo.

Katika video ya Tiktok, Carol anashabikia chakula mbwa akiendelea kukikwea huku aking’ang’ania kilicho chake.

Hana wasiwasi wowote, na kwa kijiko anashtaki njaa raha mustarehe.

“Inaonekana umepoteza fahamu. Unakula chakula kwa sahani moja na mbwa?” aliyenasa video hiyo anaskika akiuluiza.

Wanazungumza kwa lugha ya Kikuyu.

Carol Mwaura akila chakula kwenye sahani moja na mbwa. PICHA / HISANI

“Ni kiumbe safi, mtoto anayeoshwa. Huwa hapiti lango kuu, na isitoshe humpaka jeli kulainisha manyoya yake,” anaelelezea.

“Caro, una uhakika uko sawa? Mimi siwezi nikala mlo kwenye sahani moja na mbwa, hata akiwa safi kiasi gani,” mwenzake anaelezea, akiskika kushangazwa na tendo hilo.

Kulingana na msanii huyo, ni heri kula kwenye sahani moja na mbwa kuliko wasaliti au watu wanaojifanya marafiki ilhali ni maadui.

Wakati akiendelea na ‘starehe’ zake, mmoja wa wimbo aliotunga unachezwa.

“Hebu kula babaa.”

Kwa mujibu wa mazungumzo, inaskika kana kwamba alikuwa ametembelea rafikiye.

Video hiyo yenye urefu wa dakika 1 na sekunde 54, mwanadada mwingine anaonekana akisimama mlangoni na sawa na mwenyeji, anaashiria kushangazwa na tukio hilo.

“Carol inaonekana haupo makini maishani.”

Mwimbaji wa nyimbo za injili Carol Mwaura akila chakula kwenye sahani moja na mbwa. PICHA / HISANI

Baada ya kushiba, mnyama huyo anaenda zake.

Ni tendo ambalo limezua mdahalo mkali mitandaoni, wachangiaji wakihoji huenda ameingiwa na wazimu.

Hata ingawa kuna uwezekano anasaka ufuasi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, wengi wanasema ni kitendo ambacho hawawezi kufanya licha ya mbwa kuwa mnyama kipenzi.

Visanga vinavyohusisha binadamu na wanyama, tumekuwa tukivitazama kupitia filamu za ng’ambo.

Kisa cha Carol Mwaura, ni ishara kuwa vipindi vya aina vimetua hapa Kenya.

Kinastaajabisha.

Mbwa, licha ya kuwa mnyama mwenye thamani kwa sababu ya huduma zake za ulinzi, anachukuliwa kama kiumbe asiyebagua anachokumbana nacho almuradi kiwe ni mlo.

  • Tags

You can share this post!

Shakahola: 10 waokolewa wakiwa wamedhoofika kiafya

 Seneta ashtakiwa kwa kukwepa kulipa ushuru

T L