• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 5:30 PM
Maandalizi ya Maonyesho ya ASK Nairobi 2023 yakamilika

Maandalizi ya Maonyesho ya ASK Nairobi 2023 yakamilika

NA SAMMY WAWERU

MATAYARISHO ya Maonyesho ya Kimataifa ya Kibiashara na Kilimo jijini Nairobi mwaka huu, yanayoandaliwa na Chama cha Kilimo cha Kenya (ASK), yamekamilika huku maelfu ya watu wakitarajiwa kuhudhuria.

Maonyesho hayo yamevutia zaidi ya waonyesha 350, kutoka ndani na nje ya nchi, ambao wamethibitish kuhudhuria kulingana na waandalizi.

Aidha, yameratibiwa kung’oa nanga mnamo Jumatatu, Septemba 25 hadi Oktoba 1, na kauli mbiu ya 2023 ni “Kukuza kilimo na miradi ya kibiashara yenye mapato kwa ukuaji wa uchumi endelevu”.

Yatafanyika katika Uwanja wa Maonyesho wa Jamhuri, Nairobi.

“Kila kitu kiko tayari, na majukwaa yameandaliwa,” anasema Bw Joseph Mugo, Mwenyekiti wa Tawi la ASK la Nairobi.

Hafla hiyo inalenga kuleta pamoja wadau wote katika sekta ya kilimo na biashara, ikiwa ni pamoja na viwanda, biashara ndogondogo na za wastani – kadri (MSMEs), huku bunifu, teknolojia za kisasa kuboresha kilimo, huduma za kifedha na matangazo, pamoja na maonyesho ya moja kwa moja, yakiwa ni baadhi ya mambo ambayo watakaohudhuria watashuhudia.

Josephat Gitonga, Mwenyekiti Kamati ya Mauzo ASK tawi la Nairobi akielezea kuhusu maandalizi ya shoo ya ASK Nairobi 2023, Jamhuri Grounds. PICHA|SAMMY WAWERU

Maonyesho hayo pia yatawapa wakulima fursa kuuliza maswali kwa wataalamu wa kilimo, kuunda mtandao wa masoko, na kuleta ushirikiano na wachezaji katika sekta ya kilimo na biashara.

Maonyesho hayo ya siku saba, yatatoa mafunzo ya bure kwa wakulima kupitia semina, na maonyesho ya mifugo.

“Bunifu, teknolojia na mifumo ya kisasa kuendeleza kilimo imedhihirisha kuongeza mazao ikilinganishwa na mbinu za jadi, ni muhimu kuwapa wakulima jukwaa ambalo watapata mafunzo. Maonyesho haya yatashirikisha yote hayo,” anasema Bw Batram Muthoka, Afisa Mkuu Mtendaji wa ASK.

Antonina Kandie kutoka Kenya Seed, mojawapo ya kampuni na mashirika yatakayohudhuria Nairobi ASK 2023. PICHA|SAMMY WAWERU

Kauli mbiu ya 2023 ikiegemea kuangazia changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, Betty Rotich, Meneja wa Tawi la ASK Nairobi, anasema watanufaika kufunguliwa macho na mawazo jinsi ya kukabiliana na kero ya hali ya hewa.

Bunifu na teknolojia zitakazoonyeshwa ni pamoja na njia za kuvuna na kuhifadhi maji, unyunyiziaji mimea na mashamba kwa kutumia mifereji, teknolojia ya nishati ya kijani, uzalishaji wa gesi, na nishati ya jua.

“Tumefanya juhudi kuleta wadauhusika watakaoonyesha mbinu na teknolojia hizo,” Bi Betty akaambia Taifa Leo Dijitali, kupitia mahojiano ya kipekee.

Betty Rotich, Meneja ASK tawi la Nairobi. PICHA|SAMMY WAWERU

Kulingana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Kenya ni miongoni mwa nchi zilizoathirika vibaya na mabadiliko ya tabianchi katika Pembe ya Afrika.

Hivyo, kuna haja ya kampeni kutumia teknolojia na uvumbuzi wa kisasa kupambana na janga hili.

Kupevusha wakulima kuhusu mbinu hizo, mazao yanayostahimili athari za ukame, yatakuwa kwenye majukwaa.

Kuna nafasi 2, 000 ambazo zitatumika kutoa maonyesho, hafla hiyo ikianza kushika kasi miaka miwili baada ya kuvurugwa na kusambaratishwa na janga la Covid-19 mwaka 2020.

Josephat Gitonga, Mwenyekiti Kamati ya Mauzo ASK tawi la Nairobi akiwa kwenye kipande cha shamba la mahindi. PICHA|SAMMY WAWERU

Wakulima wachanga, watashiriki kupitia Mpango wa 4K Club – Mradi unaokuza wanafunzi shuleni kunoa makali kuendeleza kilimo na ufugaji.

4K Club ilifufuliwa 2021 na Rais Uhuru Kenyatta, ambaye kwa sasa ni mstaafu.

Rais wa sasa, Dkt William Ruto anatarajiwa kufungua rasmi maonyesho hayo.

Ada za kuingia ni Sh300 kwa watu wazima kila mmoja, Sh250 kwa watoto, na kwa makundi, mtu mzima atalipa Sh250 na mtoto Sh200.

Wanachama wa ASK wenye kadi halali ya uanachama wanaweza kuitumia kuingia maonyeshoni.

Joseph Mugo, Mwenyekiti ASK tawi la Nairobi na Betty Rotich, Meneja. PICHA|SAMMY WAWERU
  • Tags

You can share this post!

Mpenzi wangu ataka nitafute mwanamume mwingine maana...

Dorcas Gachagua: Ufukara katika familia nusra usababishe...

T L