• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 3:31 PM
Maandamano ya Azimio kufanyika siku tatu kila wiki

Maandamano ya Azimio kufanyika siku tatu kila wiki

NA SAMMY WAWERU

CHAMA cha ODM kimetangaza Ijumaa kuwa maandamano ya upinzani yatakuwa yakifanyika siku tatu kwa wiki. 

Akizungumza wakati wa ziara katika Shule ya Msingi ya Kihumbuini, Kangemi, Nairobi seneta wa Nairobi Edwin Sifuna alisema Azimio imetathmini ratiba ya awali iliyopendekeza maandamano kufanyika kati ya Jumatatu na Jumatano kuanzia wiki ijayo.

Kulingana na Katibu Mkuu huyo wa ODM, maandamano ya upinzani sasa yatakuwa yakifanyika Jumatano, Alhamisi na Ijumaa kila juma.

“Tumefanya mabadiliko hayo kufuatia maombi ya umma, hivyo basi yatakuwa yakifanyika Jumatano, Alhamisi na Ijumaa,” Bw Sifuna akasema.

Mwanasiasa huyo ambaye ni mwandani wa kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga aliye pia kinara wa muungano wa Azimio la Umoja – One Kenya, alisema kila wiki siku tano zitatengwa kuomboleza na kukumbuka waandamanaji walioangamia Jumatano, Julai 12, 2023 kwa kupigwa risasi na maafisa wa polisi.

Wakili Sifuna alizuru Shule ya Kihumbuini, ambapo wanafunzi wa taasisi hiyo walirushiwa gesi ya vitoa machozi wakati wa maandamano. 

Alikuwa ameandamana na mbunge wa Westland, Bw Tim Wanyonyi na Babu Owino (Embakasi). 

Viongozi hao walilalamikia askari kurusha gesi ya vitoa machozi katika shule yenye watoto wadogo kiumri. 

“Wakitaka kurusha gesi ya vitoa machozi, wanirushie au waje kwangu kwa sababu nimezoea,” Bw Sifuna alisema. 

Kinara wa Azimio, Raila Odinga ameapa kuendeleza maandamano licha ya serikali ya Rais William Ruto kuyataja kuwa haramu na yanayolenga kulemaza uchumi. 

Bw Odinga alisema shabaha yake ni kushikiniza serikali kushusha gharama ya juu ya maisha, inayozidi kulemea Wakenya. 

Isitoshe, upinzani unapinga kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2023, unaopendekeza nyongeza ya ushuru (VAT) wa bidhaa muhimu za kimsingi, ikiwemo mafuta ya petroli kutoka asilimia 8 hadi 16. 

  • Tags

You can share this post!

Viongozi wa Azimio wawatembelea wanafunzi waliorushiwa...

Mandago adai Gavana Bii alirithi Sh104 milioni za mpango wa...

T L