• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Mandago alivyomualika Gachagua kwa Kongamano la Ugatuzi Uasin Gishu asijue masaibu yaliyomsubiri  

Mandago alivyomualika Gachagua kwa Kongamano la Ugatuzi Uasin Gishu asijue masaibu yaliyomsubiri  

NA SAMMY WAWERU

KATIKA ziara ya Naibu Rais Rigathi Gachagua maeneo mbalimbali Kaskazini na Kusini mwa Bonde la Ufa mapema wiki hii, Seneta wa Uasin Gishu Jackson Mandago alitoa mwaliko wa dhati kwa Bw Gachagua kushiriki Kongamano la Ugatuzi 2023 linaloendelea.

Kongamano hilo la Makala ya Kumi lenye kauli mbiu “Miaka 10 ya Ugatuzi: Sasa na Siku zijazo,” linafanyika Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu.

Bw Mandago, ambaye awali alihudumu mihula miwili kama Gavana, kuanzia 2013 hadi 2022, alitoa mwaliko huo rasmi kwa Bw Gachagua akisema serikali ya Rais William Ruto ina mapochopocho kwa serikali za kaunti.

Seneta huyo hakujua hatashiriki ufunguzi rasmi.

Jumatano, Agosti 16, Rais William Ruto, pamoja na naibu wake na maafisa wengine wa ngazi ya juu serikalini, aliongoza uzinduzi wa mkutano huo wa kitaifa.

“Mheshimiwa Naibu Rais, tunakukaribisha kwenye mkutano wa ugatuzi. Serikali ya Kenya Kwanza chini ya uongozi wa Rais Ruto, imeahidi mengi kwa kaunti,” Mandago alisema.

Akaongeza, “Ni jukwaa ambalo litasaidia kutathmini kiwango cha ugatuzi…Litatoa ufahamu wa hali yetu ya sasa na mwelekeo”.

Bw Mandago, hata hivyo, amejipata kwenye kikaango moto kufuatia kashfa ya Mpango wa Masomo wa Finland na Canada ambapo anaandamwa kama mshukiwa mkuu wa ubadhirifu wa fedha zilizotolewa na wazazi.

Wakati wa utawala wake kama Gavana, mwaka 2021, alizindua mpango huo kwa vigezo vya ufadhili.

Hata hivyo, umegeuka kuwa sakata ya watu wenye ubinafsi kujinufaisha.

Yeye, pamoja na maafisa wengine wa kaunti, wanakabiliwa na tuhuma za kufuja kima cha Sh1.1 bilioni, fedha zilizotolewa na wazazi.

Wazazi na wanafunzi walioathirika katika hashfa hiyo, walisimulia kwa machungu hasara waliyokadiria wakitaka kurejeshewa pesa zao.

Gavana wa sasa Uasin Gishu, Jonathan Bii, amejitenga na sakata hiyo, akisema “Wale waliohusika katika mpango huo lazima wabebe mzigo wao wenyewe”.

Jumatano, Agosti 16, Mandago alitiwa nguvuni baada ya kujisalimisha mwenyewe katika Afisi za Idara ya Uhalifu na Jinai (DCI) Nakuru, kufuatia amri ya kukamatwa kwake iliyotolewa na mahakama.

Rais Ruto pia ameeleza msimamo wake kuhusu jambo hilo, akiwataka wanaodaiwa kuiba mamilioni kutoka kwa wazazi kupitia Mpango wa Finland kurejesha pesa walizoiba.

Akizungumza na wakazi wa Eldoret baada ya kuzindua rasmi Kongamano la Ugatuzi 2023 linaloendelea, Dkt Ruto alitaja kisa hicho kama cha aibu, akiahidi kutokubali matukio kama hayo kutokea chini ya utawala wake.

 

  • Tags

You can share this post!

Tuwei achaguliwa naibu rais wa Shirikisho la Riadha Duniani

Maafisa Lamu wakuna vichwa Al-Shabaab wakitumia mbinu mpya

T L