• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 6:36 PM
Tuwei achaguliwa naibu rais wa Shirikisho la Riadha Duniani

Tuwei achaguliwa naibu rais wa Shirikisho la Riadha Duniani

Na GEOFFREY ANENE

RAIS wa Shirikisho la Riadha Kenya (AK) Jackson Tuwei amechaguliwa kuwa mmoja wa manaibu rais wanne wa Shirikisho la Riadha Duniani kwenye kongamano la 54 katika jumba la mikutano la Hungexpo jijini Budapest, Hungary mnamo Alhamisi.

Tuwei, ambaye ni naibu rais wa Shirikisho la Riadha Afrika (CAA) na rais wa Shrikisho la Riadha la Afrika Mashariki, amechuguliwa pamoja na Ximena Restrepo kutoka Chile, Raul Chapado (Uhispania) na Adille Sumariwalla (India).

Restrepo alipata kura 154, Chapado (119), Sumariwalla (115) na Tuwei (104).

Wagombea Nawaf Bin Mohammed Al Saud (Saudi Arabia) na Geoff Gardner (Norfolk Island) ambao walikuwa wakitetea nyadhifa zao, walipoteza viti vyao.

Mnamo Agosti 16, 2023, Tuwei alikuwa ameelezea matumaini yake na msimamo kuwa Kenya ilistahili kupata kiti katika Shirikisho la Riadha Duniani kutokana na juhudi zake zilizoshuhudia ikisajili zaidi ya wanariadha 5,000 nchini Kenya, kupata uungwaji mkono kutoka kwa serikali na kuwa mstari wa mbele katika masuala ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya tabianchi pamoja na kuweka mipango kabambe ya maendeleo.

Mwingereza Sebastian Coe, ambaye alirithi urais kutoka kwa raia wa Senegal Lamine Diack mwaka 2015, amehifadhi kiti chake bila kupingwa.

  • Tags

You can share this post!

Mjakazi anayedaiwa kumuua afisa wa kaunti kuzuiliwa siku 14...

Mandago alivyomualika Gachagua kwa Kongamano la Ugatuzi...

T L