• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 5:50 AM
Mara mbili akila hasara lakini bado anang’ang’ana

Mara mbili akila hasara lakini bado anang’ang’ana

NA PETER CHANGTOEK

UONGEZEAJI thamani maziwa ni shughuli ambayo inaweza kumletea mkulima mapato zaidi. Hii ni kwa sababu bidhaa zilizoongezewa thamani huuzwa kwa bei za juu, ikilinganishwa na kuyauza maziwa ya kawaida.

Mmojawapo wa wale wanaochuma kutokana na uongezaji thamani kwa maziwa ni Margaret Njoki, ambaye alijitosa katika shughuli ya hiyo miaka saba iliyopita, wakati huo, akihudumu katika kampuni moja mjini Naivasha. Hata hivyo, alikuwa akiyauza maziwa tu mnamo mwaka 2015.

Baada ya kugundua kuwa wateja wengi walikuwa wakihitaji maziwa gururu (yoghurt), akaamua kuzitengeneza pamoja na bidhaa nyinginezo za maziwa; mathalani jibini, siagi n.k.

Kwa sasa, Njoki huongeza thamani maziwa na kupakia katika plastiki na kusambaza kwa wateja wake.

Aidha, huuza kwa dukakuu moja.

“Kandarasi yangu kazini ilipoisha 2016, nilikuwa na uhakika kuwa sitaki kuajiriwa tena. Nikahama ili kuendeleza uzalishaji katika eneo la Kabati. Mnamo 2017, nikapoteza gururu kutokana na uharibifu,” asema Njoki.

Kuharibika kwa bidhaa zake kulimshurutisha kufunga shughuli ya utengenezaji, baada ya kupoteza bidhaa zilizokuwa na thamani ya Sh400,000.

Kilichoonekana kama kutia chumvi kwenye kidonda, wafanyakazi wake wakamwibia bidhaa zilizokuwa zimebaki.

Kabla ya hasara hiyo, alikuwa akizitengeneza bidhaa kutoka kwa maziwa lita 700 kila siku na alikuwa akiziuza kwa muda wa siku mbili.

Hata hivyo, alifungua upya tena 2018.

Bi Margaret Njoki akionyesha baadhi ya bidhaa zake katika eneo la Ngara, Nairobi, wakati wa mahojiano. PICHA | PETER CHANGTOEK

Mambo yakaenda segemnege tena mwaka 2021, baada ya bidhaa zake kuharibika na kupata hasara ya takribani Sh600,000 na kulazimika kufunga biashara.

Licha ya changamoto, akaanza kuzitengeneza bidhaa kutoka kwa maziwa tena.

Njoki anafichua kuwa, amekuwa akinunua maziwa kutoka kwa mkulima mmoja tangu 2016. Huchakata maziwa lita 200 kila siku, anayoyanunua kwa Sh55 kwa lita.

“Nina wafanyakazi saba; watatu hapa na wanne kule Kabati,” asema Njoki, ambaye hutengeneza bidhaa nyingine katika eneo la Kabati, Kaunti ya Murang’a, na kadhaa katika eneo la Ngara, aliko na duka analouzia bidhaa zake.

Hutumia brandi ya Tarahji kwa bidhaa zake, na kampuni yake hujulikana kama Crystal Creamery Limited.

Hutengeneza bidhaa kuanzia 150ml hadi lita 5.

“Bidhaa yetu kuu ni gururu; tuna Tarahji Cultured Yoghurt. Tuna gururu iliyotiwa ladha ya matunda, aiskrimu, jibini (cheese), siagi na samli,” afichua, akiongeza kwamba, hutumia stroberi, vanila, karakara, mananasi pamoja na matunda mengine kutengeneza bidhaa zake.

Njoki hununua stroberi kilo moja kwa Sh300 kutoka kwa mkulima mmoja kutoka Nyahururu.

Pia, hununua kilo tano za matunda aina ya ‘blueberry’ kwa Sh1,500, karakara kwa Sh80 kwa kilo na mananasi kwa Sh50-Sh180 kila moja.

“Hupakia gururu kwa 150ml, 250ml, 500ml, lita 1, lita 2, lita 3 na lita 5. Pia, huwa tunauza kwa wingi, kuanzia lita 10 hadi lita 20, kwa wale wanaotaka za kuuza. Huuza gururu 12 za 150ml kwa Sh400, 12 za 250ml kwa Sh600, 6 za 500ml kwa Sh600,” afichua Njoki, anayejulikana kwa jina Mama Milky katika eneo la Ngara.

Yeye pia huwapa mafunzo watu wanaonuia kuanzisha biashara ya kutengeneza bidhaa kutoka kwa maziwa.

“Mimi hutoza Sh5,000 kwa kila bidhaa. Pia, huwa na mafunzo mtandaoni ambapo hutoza Sh3,500. Huchukua muda wa saa 2 hadi 3,” aongeza.

Anasema kwamba, mipango yake ya siku za usoni ni kulijenga jina lake katika shughuli ya kuongezea thamani maziwa.

Huuza bidhaa zake katika sehemu mbalimbali na huuza kwa dukakuu la Topmart na ameanza kuziuza kwa Jumia.

  • Tags

You can share this post!

Raila chaguo la wengi – tafiti za hivi punde

JIFUNZE BIASHARA: Ya kuzingatia wakati wa kutengeneza...

T L