• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Raila chaguo la wengi – tafiti za hivi punde

Raila chaguo la wengi – tafiti za hivi punde

NA CHARLES WASONGA

MGOMBEA urais wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga angali maarufu dhidi ya mwenzake wa Kenya Kwanza William Ruto, kulingana na matokeo ya kura ya maoni yaliyotolewa Jumanne.

Kulingana na utafiti uliendeshwa na kampuni ya Infotrak na kudhaminiwa na Shirika la Habari la Nation (NMG), Bw Odinga atapigiwa kura na 49 ya waliohojiwa ilhali asilimia 41 watampigia kura Dkt Ruto.

Kulingana na utafiti huo uliofanywa kati ya Julai 30 na Agosti 1, mgombea urais wa chama cha Roots George Wajackoyah ndiye wa tatu kwa asilimia mbili (2) huku David Waihiga wa chama cha Agano akiwa na asilimia 0.2 ya uungwaji mkono.

Asilimia saba (7) ya wapiga kura 2,400 waliohojiwa kote nchini walisema hawajaamua ni mgombea yupi wa urais watampigia kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumanne wiki ijayo.

Endapo Bw Odinga atapata uungwaji mkono kutoka kwa idadi kubwa ya watu hawa, anaweza kuibuka mshindi kwa awamu ya kwanza.

Kulingana na Katiba ya sasa, sharti mshindi katika uchaguzi wa urais apate asilimia 50 na kura moja ya idadi jumla ya kura zitakazopigwa na kuhesabiwa.

Matokeo haya yanaonyeshwa kuwa umaarufu wa Bw Odinga umeimarika kwa asilimia saba kutoka Mei mwaka huu huku ule wa Dkt Ruto ukishuka kwa asilimia moja.

Kulingana na matokeo ya utafiti wa wakati huo ambao pia uliendeshwa na Infotrak, kwa udhamini wa NMG, wagombeaji hawa wawili walitoshana kwa asilimia 42 kila mmoja.

Wakati huo huo, Bw Odinga bado alikuwa kifua mbele dhidi ya Dkt Ruto kulingana na matokeo ya utafiti ulioendeshwa na kampuni nyingine, Ipsos.

Uchaguzi mkuu ungefanyika leo, mgombea urais huyo wa Azimio angepata asilimia 47 ya kura huku Dkt Ruto akipata asilimia 41.

Profesa Wajackoyah naye ana uungwaji mkono wa asilimia 2.9 na Bw Waihiga atapigiwa kura ya asilimia 0.2 ya wapiga kura.

Asilimia 5.1 ya waliofikiwa wakati wa utafiti huo walikataa kusema ni mgombea urais yupi watampigia kura ilhali asimilia 3.8 kati yao walisema hawajafanya uamuzi kuhusu yule ambaye watampigia kura.

“Hata hivyo, watu hao walipoulizwa ni nani wanahisi kuwa atashinda urais, asilimia 54 walisema ni Bw Odinga huku asilimia 43 wakisema ni Dkt Ruto. Hii inaashiria kuwa huenda wengi wa watu hawa wakampigia kura Bw Odinga watakapofanya uamuzi huo Agosti 9,” akasema Bw Samuel Muthoka, ambaye ni mkurugenzi wa masuala ya utafiti katika Ipsos.

Bw Muthoka alisema jumla ya watu 6,105 walihojiwa katika utafiti huo kutoka kaunti zote 47 ndani ya kipindi cha wiki moja iliyopita.

“Mahojiano yaliendeshwa kwa njia ya ana kwa ana na waliohojiwa ni wale ambao wamesajiliwa kuwa wapiga kura pekee,” Bw Muthoka akawaambia wanahabari katika mkahawa wa Serena, Nairobi.

Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha kuwa Bw Odinga ana uungwaji mkono mkubwa katika kaunti 18 ambako asilimia 55 ya wapiga kura walisema watampigia kura Agosti 9.

Miongoni mwa kaunti ambako Bw Odinga anamshinda Dkt Ruto ni pamoja na Nairobi (asilimia 60), Pwani (asilimia 56), Ukambani (asilimia 67) na Nyanza (asilimia 78).Kwa upande mwingine Dkt Ruto ana ushawishi mkubwa katika kaunti 17 nchini.

Baadhi ya maeneo ambako Naibu Rais anampiku Bw Odinga kwa umaarufu ni pamoja na; Rift Valley ya Kati (asilimia 67), Mlima Kenya Mashariki (asilimia 78), Mlima Kenya Magharibi (asilimia 62).

Jumla ya kaunti 11 zinaonekana kama ambazo zitashuhudia ushindani mkubwa katika ya wagombea uraia hawa wakuu.

Kaunti hizo zinapatikana katika maeneo ya Kaskazini mwa Kenya, Kaskazini mwa Bonde la Ufa na kaunti za jamii ya Maa (Kajiado, Narok na Samburu).

Kulingana na utafiti huo wale ambao walisema watampigia Bw Odinga kura katika uchaguzi mkuu wiki ijayo wasema watafanya hivyo kwa misingi ya sifa zake kama mtetezi wa utawala wa kidemokrasia, shujaa wa ukombozi wa pili, tajriba ya uongozi miongoni mwa sababu zingine.

“Wale ambao watampigia kura Dkt Ruto walisema kuwa walifikia uamuzi huo kwa sababu atatoa matumaini kwa kutokana na sera zilizoko katika manifesto yake. Wengine wamtaja kama kiongozi aliye na uhusiano mwananchi wa kawaida,” Bw Muthoka akasema.

  • Tags

You can share this post!

Talanta ya soka ilimpa fursa ya kusoma kupitia ufadhili na...

Mara mbili akila hasara lakini bado anang’ang’ana

T L