• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Maswali yaibuka Kipchoge kukawia kupongeza chipukizi aliyevunja rekodi yake ya marathon

Maswali yaibuka Kipchoge kukawia kupongeza chipukizi aliyevunja rekodi yake ya marathon

NA LABAAN SHABAAN

SEHEMU ya Wakenya wametilia shaka kimya cha mwanamarathoni mashuhuri Eliud Kipchoge ambaye kufikia wakati tulipopeperusha taarifa hii hakuwa amempa heko mwanariadha Kelvin Kiptum aliyevunja rekodi yake.

Kiptum alivunja rekodi ya mbio za masafa marefu iliyoshikiliwa na Kipchoge alipotimka kwa saa mbili na sekunde 35.

Mwanariadha huyo ameingia kwenye orodha ya Wakenya 6 ambao wamewahi kuweka rekodi ya dunia ya mbio hizi.

Alinakili rekodi mpya ya dunia katika mashindano ya Chicago, Amerika Oktoba, 8, 2023 akivunja ya Kipchoge ya 2:01:09, Berlin, Ujerumani Septemba 25, 2022.

Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 23 hakuvunja rekodi hiyo tu, bali pia alivunja mitandao ya kijamii akimiminiwa sifa kedekede nchini na ulimwenguni.

Baada ya Kiptum kushangaza dunia, Wakenya wamemvamia Kipchoge kwa sababu hajasema chochote hadharani kuhusu kinda ‘aliyempokonya sifa.’

Rais William Ruto aliongoza taifa kumpongeza mmiliki mpya wa rekodi ya mbio za masafa marefu.

“Ameandikisha chapta mpya katika historia ya mbio za masafa marefu. Amekuwa binadamu wa kwanza kuvunja rekodi ya saa 2 na dakika 1. Kongole mfalme mpya wa marathon, Kelvin,” Rais alimpongeza kupitia taarifa aliyopachika kwenye akaunti yake rasmi ya mtandao wa kijamii wa X (awali Twitter).

Naibu Rais Rigathi Gachagua pia alimmiminia sifa staa huyo wa riadha.

“Kuvunja rekodi ya mwanariadha mashuhuri Eliud Kipchoge kunastaajabisha. Heko Kelvin kwa ushindi huu,” Bw Gachagua aliandika.

Kipchoge ambaye rekodi yake imefutwa, amenyamaza kimya chenye mshindo mkuu, na siku tatu baadaye Wakenya wanasubiri kumsikia.

“Sijaona ujumbe wa pongezi kwa Kiptum kutoka kwa Kipchoge mwenyewe. Ni nini kibaya na Kipchoge ambaye huturushia misemo ya motisha ya jinsi ya kukiuka mipaka? Kiptum alivunja mipaka, siyo?” alisema mtumiaji wa mtandao wa X, Abraham Mutai.

Mwengine, Thirsty Kipsowet, alisema, “Nimechoka kungoja. Saa 24 baada ya rekodi kuvunjwa, Eliud Kipchoge bado hajampa heko Kiptum! Lakini nikiongea mtasema nina mambo. Acha Mungu aamue kesi…”

“Nadhani ingekuwa busara kwa Eliud Kipchoge kumpongeza Kiptum,” alieleza Rogers Kipembe.

Mtumiaji mwengine wa mitandao ya kijamii alikubaliana na wengine akifoka, “Nilitaja hili mahali kuwa nchi imenyamaza na haipigi kelele kwa sababu si Kipchoge. Hongera Kiptum! Kumbuka hilo jina!”

Ila kuna sehemu ya Wakenya ambao hawana kinyongo na Kipchoge.

“Kwa nini watu wanamshambulia Kipchoge kwa kutotoa pongezi? Nani anajua kama wameongea kupitia simu? Lakini ukweli usemwe, mwaka huu Kipchoge alimtaja Kiptum kama mrithi wake,” alisema Julius Kones.

  • Tags

You can share this post!

Obama akashifu Hamas kwa ‘shambulizi la kigaidi lenye...

Akothee ajibu mashabiki wake kuhusu uraia wa Omosh

T L