• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Mbinu maalum anayotumia mfugaji kupata malisho eneo kame ng’ombe wake wazalishe maziwa    

Mbinu maalum anayotumia mfugaji kupata malisho eneo kame ng’ombe wake wazalishe maziwa   

NA SAMMY WAWERU

RICHARD Katiso ni mmoja wa wakulima Kaunti ya Makueni wanaomiliki trekta, mfumo wa kisasa kuboresha na kuendeleza zaraa. 

Akiwa na tajiriba ya muda mrefu katika kilimo cha nafaka, Katiso, ambaye ni mkulima eneo la Nziu, anataja matumizi ya mashine kama mbinu ambayo imemsaidia kuboresha ufugaji.

Aidha, hufuga ng’ombe wa maziwa na amekumbatia mfumo wa kujiundia malisho ili kupunguza gharama hasa kipindi hiki chakula cha bei yake ni mithili ya dhahabu.

Kupitia trekta, amekita mizizi kufanikisha deep tillage – mfumo au teknolojia ya kulima mitaro yenye kina kirefu.

Mkulima Richard Katiso wa Makueni akielezea kuhusu mfumo wa deep tillage ambao umemsaidia pakubwa kupunguza gharama ya ufugaji. PICHA|SAMMY WAWERU

Ni mbinu sehemu ya shamba ambayo haipandwi mimea, haiguswi. Inayolengwa pekee, ndiyo inalimwa.

Mitaro inahifadhi na kudumisha unyevuunyevu wa maji hivyo basi kusaidia kunawirisha mazao.

Katiso analima mahindi kwenye karibu ekari kumi, ambayo anasema hutumia majani na matawi yake kuunda chakula cha mifugo.

Hali kadhalika, husaga kiwango fulani cha mahindi na kuchanganya na virutubisho faafu kwa mifugo.

“Nilikumbatia mfumo wa deep tillage 2022, na kufikia sasa nimeona mabadiliko makubwa,” asema.

Richard Katiso akionyesha mbolea inayotokana na mifugo wake. PICHA|SAMMY WAWERU

Awali, Katiso alikuwa akitumia mafahali – Ox plough, mfumo wa kitambo unaotajwa kutatiza ustaarabu wa udongo, madini na pia virutubisho.

“Ox – Plough, shamba lote linalimwa – mitaro ikiwa na kina cha urefu wa sentimita 5 hadi 8 na haihifadhi maji,” Mark Nzivo, mtaalamu, aelezea.

Chini ya mfumo wa deep tillage, majembe ya kutandaza (chisel plough)  – yenye ncha kali yanatumika.

Huandaa mitaro yenye kina cha sentimita 15 hadi 25.

Mitaro ya Deep Tillage kwenye shamba la mkulima. PICHA|SAMMY WAWERU

Mfumo huu unahamasishwa maeneo kame nchini kupitia Kenya Crops and Dairy Market Systems (KCDMS) chini ya Shirika la United States Agency for International Development (USAID) ili kuongeza kiwango cha uzalishaji.

Aidha, Katiso anaambia Taifa Leo Dijitali kwamba tangu akumbatie deep tillage, uzalishaji wa mahindi katika kila ekari umepanda kutoka magunia matano hadi zaidi ya tisa, mfuko wa kilo tisini.

“Majani na matawi ya mahindi ninayasaga na kuunda hay na silage, na kiwango cha uzalishaji maziwa kimeongezeka mara dufu,” asema.

Majani na matawi ya mahindi ambayo Richard Katiso hutumia kuunda malisho ya ng’ombe wake wa maziwa. PICHA|SAMMY WAWERU

Anakiri kwamba amefanikiwa kupunguza gharama ya ufugaji kwa karibu asilimia hamsini.

“Ninanunua chakula kidogo tu cha madukani, kusawazisha virutubisho.”

Hata hivyo, kulingana na Mark Nzivo, ambaye ni miongoni mwa wataalamu wa mashinani (Village Based Advisors – VBA) wanaotumika na KCDMS kueneza mafunzo ya deep tillage, mkulima atapata mavuno ya kuridhisha endapo atazingatia kanuni faafu kitaalamu, zikiwemo matumizi ya mbolea na fatalaiza kunawirisha mazao.

  • Tags

You can share this post!

Askari wanavyohamasishwa Migori kupunguza visa vya...

Majonzi, hasara mvua ikiendelea kushuhudiwa nchini  

T L