• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 10:55 AM
Mbunge wa UDA apendekeza Raila aanze kupewa pesa za hazina za uzeeni

Mbunge wa UDA apendekeza Raila aanze kupewa pesa za hazina za uzeeni

NA SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Tinderet, Julius Melly amezua mdahalo mkali mitandaoni kufuatia pendekezo lake kiongozi wa upinzani, Raila Odinga asajiliwe kwa minajili ya kuanza kupokea pesa za hazina ya uzeeni.

Katika kile kinaonekana kama tani za kisiasa, Melly amesema Bw Odinga anapaswa kunufaika kupitia mpango huo kwa sababu amehitimu miaka 70.

Bw Odinga alizaliwa Januari 7, 1945. Kwa sasa, ana umri wa miaka 78 na wapinzani wake wamekuwa wakimtaka astaafu ulingo wa siasa.

Kupitia mpango wa Older-Persons-Cash-Transfer (OPTC), wanaopewa pesa za wazee za serikali ni waliofikisha umri wa miaka 65.

“Huyu mtu wa vitendawili (akimaanisha Raila Odinga) nafikiri amefika miaka 70, asajiliwe aanze kupokea pesa za wazee,” Bw Melly akasema, kupitia video inayosambaa mitandaoni.

Kwa mujibu wa jukwaa alilotoa matamshi hayo, ni katika ziara ya Naibu Rais, Rigathi Gachagua Kaunti ya Nandi.

Kwenye video hiyo, mbunge huyo anaskika akisifia utendakazi wa Bw Gachagua – akimtaja kama kiongozi mkakamavu anayesaidia Rais William Ruto kuhudumia Wakenya.

Mashambulizi ya Bw Melly kwa kinara wa Azimio la Umoja, Raila Odinga yalionekana kuchochewa na tetesi kuwa Waziri Mkuu huyo wa zamani anajaribu juu chini kujumuishwa katika serikali ya Kenya Kwanza.

“Tunamwambia hakuna Handisheki katika serikali hii hadi miaka kumi itakapoisha,” mbunge huyo wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) akasema.

Matamshi yake yanajiri wakati ambapo upinzani-Azimio na Kenya Kwanza, wawakilishi wake wanatarajiwa kufanya mazungumzo ya mapatano kati ya Bw Odinga na Dkt Ruto.

“Walio Bomas, waongee, wanywe chai na wapige porojo lakini mambo ya Handisheki yasitajwe,” Melly alisema.

Ukumbi wa Bomas, ndiko mazungumzo yanatarajiwa kufanyika kikao cha kwanza kiking’oa nanga Jumatatu, Agosti 14, 2023.

Rais Ruto na Bw Gachagua, wamefutilia mbali kuwepo kwa Handisheki.

  • Tags

You can share this post!

Wakubwa wa polisi wanavyohangaisha maafisa wa ngazi za...

Ndoa na familia za walimu sasa kuimarika

T L