• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 10:50 AM
Mgombea mwenza wa ugavana Mombasa alivyo na usemi mkuu

Mgombea mwenza wa ugavana Mombasa alivyo na usemi mkuu

NA PHILIP MUYANGA

UTEUZI wa mgombea mwenza wa ugavana Kaunti ya Mombasa ni suala zito ambalo yeyote anayewania ugavana lazima alitilie maanani, tofauti na kaunti nyingine za Pwani.

Kaunti ya Mombasa ni tofauti na kaunti nyingine za Pwani kwani wapigakura hutoka maeneo tofauti na wengi wao si wazaliwa wa kaunti hii.

Suala hili limefanya wanaogombea ugavana kuwachuja kwa makini wanaonuia kuwateua kuwa wagombeawenza kwani wakikosea kidogo tu, watapoteza kura.

Kulingana na wadadisi wa kisiasa, jamii, jinsia na dini ni mojawapo ya vigezo muhimu ambavyo mwaniaji ugavana katika kaunti ya Mombasa anafaa kuzingatia iwapo anataka kupata kura kutoka kwa kila kundi la wapigakura.

Hivi majuzi mwaniaji wa kiti cha ugavana Mombasa Bw Suleiman Shahbal alimteua Bi Selina Maitha Lewa kuwa mgombeamwenza katika kinyang’anyiro hicho.

Katika uteuzi huo, Bw Shahbal alionekana kuzingatia suala la jamii kwani Bi Lewa anatoka jamii ya Mijikenda ambayo ni kubwa katika kaunti ya Mombasa na kura zao zitakuwa muhimu kwake.

Pia Bw Shahbal alionekana kuangalia suala la jinsia kwani idadi ya wanawake ni kubwa na Bi Lewa atakuwa na nafasi kubwa ya kuwashawishi wanawake kumuunga mkono.

Katika mwaka wa 2013, gavana wa Mombasa Hassan Joho alimteua Bi Hazel Katana anayetoka katika jamii ya Mijikenda na ilionekana kuwa pia yeye alitaka kura za jamii hiyo na pia zile za wanawake.

Hata hivyo, mwaka wa 2017 ingawa hakumchagua mwanamke kama mgombea mwenza,Bw Joho alimchagua Dkt William Kingi ambaye anatoka jamii ya Wamijikenda.

Hii ilionyesha kuwa alikuwa anataka kura za Wamijikenda na pia kulingana na wachanganuzi wa kisiasa, itakuwa vigumu watu wa dini moja hususan katika kaunti ya Mombasa kuwa gavana na naibu.

Mwaka wa 2017, Bw Hassan Omar aliyegombea kiti hicho alimchagua Bi Linda Mariwa Shuma kuwa mgombeamwenza jambo lililoonekana kwa wakati huo kama kutafuta kura kutoka kwa wanawake na vijana.

Prof Halimu Shauri ambaye ni mchanganuzi wa siasa alisema kuwa uteuzi wa Bi Lewa kuwa mgombeamwenza wa Bw Shahbal ulitimiza baadhi ya vigezo vinavyotumiwa katika uteuzi kwani uliangazia kura za jamii ya Mijikenda, dini na pia kura za wanawake.

“Jamii ya Mijikenda ndiyo kubwa hapa Mombasa. Bw Shahbal amesawazisha dini, jamii na jinsia kwa pamoja kwa kumchagua Bi Lewa,”alisema Prof Shauri.

Prof Shauri aliongeza kusema kuwa uteuzi wa mgombea mwenza ni swala ngumu kwani kama mgombeaji wa ugavana ni lazima aangalie vigezo kadhaa ili kuweza kupata kura katika kila kundi la watu walioko katika kaunti.

“Kama makundi ua vigezo hivyo vitaleta kura,basi haina budi kwa mgombea ugavana kumteua mgombea mweza ambaye yuko katika makundi hayo yote kwa pamoja,”alisema Prof Shauri.

Kulingana na Prof Shauri,uteuzi wa mgombea mwenza pia unazingatia mvuto ambao mgombea huyo mwenza ako nao kwa wapiga kura.

Mchanganuzi mwingine wa siasa Bi Maimuna Mwidau alisema kuwa mchanganyiko wa watu katika kaunti ya Mombasa unaifanya kuwa ya kipekee katika uteuzi wa mgombea mwenza.

Bi Mwidau alisema kuwa mgombeaji ugavana lazima ahakikishe kuwa kila kundi linajumuishwa wakati wa uteuzi wa mgombea mwenza.

Alisema kuwa wengi wanaopigania kiti cha ugavana katika kaunti ya Mombasa ni wazaliwa wa mjini wengi wao wakiwa na uwezo wa kifedha ndiposa hutafuta kuungana na wakazi ambao huwa hawana kipato kikubwa ili kupata kura.

Bi Mwidau pia alisema kuwa kwa mwaniaji ugavana anayeteua mgombea mwenza mwanamke nafasi yake ya kupata kura za wanawake huwa kubwa mno.

“Masuala ya wanawake yanawaathiri wote licha ya tofauti zao za kidini au kijamii,” alisema Bi Mwidau akiongeza kuwa hatua hiyo huongeza thamani ya upigaji kura kwa mgombea yeyote.

Bi Mwidau alisema kuwa kila mgombeaji kiti cha ugavana katika kaunti ya Mombasa lazima aangalie ni wapi ambapo anatafuta mgombeamwenza.

“Kuna mienendo mingi na tofauti ambayo ina ushawishi na jamii inafaa kufahamu ni nani anayejihusisha na mgombea mwenza,” alisema Bi Mwidau.

Akigusia uteuzi wa Bi Lewa, mchanganuzi huyo alisema kuwa kuteuliwa kwake kunaweza kumsaidia Bw Shahbal kupata kura kutoka kwa wanawake na pia jamii ya Wamijikenda.

Mshauri wa masuala ya kisiasa Bw Bozo Jenje alisema kuwa uchaguzi wa mgombeamwenza unategemea sana upigaji kura wa jamii ambayo inaweza kubadilisha mkondo wa siasa.

“Katika kaunti ya Mombasa, kuna jamii mbili ambazo ni Mijikenda na Waswahili ambao chimbuko lao ni ukanda wa Pwani,” alisema Bw Jenje.

Kulingana na Bw Jenje, wadadisi wengi wa kisiasa wanasema kuwa jamii hizo mbili lazima zihusishwe katika uongozi wa kaunti ya Mombasa huku kura za jamii nyingine zikiwa za ‘kujazia’ tu.

“Kukosa kutambua jamii hizo mbili ni kama kujitafutia tikiti ya kushindwa katika uchaguzi,”alisema Bw Jenje.

Akizumgumza na Taifa Leo hapo awali,Bw Shahbal ambaye ni mgombea kiti wa ugavana wa kwanza kumteua mgombea mwenza alisema kuwa alimchagua Bi Lewa kwa kuwa anafaa katika nafasi hiyo.

Alisema kuwa kumteua Bi Lewa,alizingatia uwezo wake wa utenda kazi na wala sio jinsia au uhusiano wake na marehemu Karisa Maitha,aliyekuwa mwanasiasa shupavu Pwani.

Kumekuwa na tetesi za kisiasa ya kuwa wawaniaji ugavana wanaume ambao hawatawateua wanawake kama wagombea wenza hawatapata kura nyingi za wanawake.

Wengine wanaowania ugavana ni pamoja na Hassan Omar (UDA), Abdulswamad Nassir na naibu gavana wa Mombasa Dkt Kingi wote wa ODM.

Kando na Bw Shahbal,hakuna mwaniaji mwingine wa ugavana ameteua mgombea mwenza.

  • Tags

You can share this post!

Mtihani mgumu kwa Orengo akilenga ugavana Siaya

Ukraine yasema imetwaa jiji kuu

T L