• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
MIKIMBIO YA SIASA: Mipasuko ya Mulembe ilivyomponza Kizito

MIKIMBIO YA SIASA: Mipasuko ya Mulembe ilivyomponza Kizito

NA CHARLES WASONGA

MGAWANYIKO miongoni mwa wabunge kutoka jamii ya Waluhya (Mulembe) ulimkosesha aliyekuwa mbunge wa Shinyalu, Bw Justus Kizito Mugali nafasi katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA).

Wabunge na maseneta kutoka jamii hii wameiambia safu hii kuwa mipango ya wabunge na maseneta kutoka kaunti za Kakamega, Busia, Vihiga, Bungoma, Trans Nzoia kumpiga jeki Bw Kizito ilisambaratishwa na hatua ya wabunge fulani kukutana na Rais William Ruto katika Ikulu majuzi.

Wabunge hao ni Emmanuel Wangwe (Navakholo), Titus Khamala (Lurambi) na mbunge wa Ikolomani, Bw Benard Shinali.

Watatu hao waliandamana na aliyekuwa Mbunge wa Mumias Mashariki, Benjamin Njomo Washiali, ambaye alihudumu kama mshirikishi wa kampeni za urais za Rais Ruto katika kaunti ya Kakamega kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Ni kweli kwamba tulipanga sio tu kumpigia kura ndugu yetu Bw Kizito bali tulitaka kumfanyia kampeni miongoni mwa wenzetu kutoka maeneo mengine. Tulipanga kufanya mkutano katika hoteli ya Maanzoni, Machakos, kupanga mikakti hiyo,” anasema Mbunge wa Lugari, Nabii Nabwera.

“Lakini baadaye baadhi yetu tuling’amua kwamba ajenda nyingine ya mkutano huo ilikuwa ni kuturai kuiga mfano wa wale wenzetu walioenda Ikulu kwa kuhama Azimio na kuungana na Kenya Kwanza. Ndiposa sisi ambao ni waaminifu kwa Azimio tukaamua kujitenga na mkutano huo,” anaongeza mbunge huyo anayehudumu muhula wake wa kwanza.

Wengine ambao walikuwa wameahidi kuhudhuria mkutano huo wa Maanzoni mnamo Jumamosi wiki jana walikuwa seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna na wabunge wa jamii ya Waluhya kutoka mirengo yote miwili ya kisiasa.

Mkakati wao ulikuwa ni kukaidi miegemeo yao ya kisiasa na kumuunga mkono Bw Kizito, ambaye alikuwa mwaniaji wa kipekee kutoka jamii ya Waluhya miongoni mwa watu 27 walioidhinishwa kung’ang’ania nafasi tisa katika bunge la EALA.

Mbunge huyo wa zamani wa Shinyalu, ni miongoni mwa watu 12 kutoka mrengo wa Azimio walioidhinishwa kwa kinyang’anyiro hicho na miongoni mwa sita bora kutoka chama cha ODM.

Wadadisi wanasema ni mgawanyiko huo miongoni mwa wabunge kutoka jamii ya Waluhya uliochangia pakubwa ushindi wa bintiye kiongozi wa ODM Raila Odinga, Winnie na mfanyabiashara wa Mombasa Suleiman Shabhal.

“Bila shaka ilikuwa aibu kubwa kwa jamii ya Waluhya ambayo ni ya pili kwa ukubwa nchini Kenya kukosa uwakilishi katika bunge la EALA kutokana na migawanyiko na usaliti wa kisiasa miongoni mwa wabunge wao. Kinaya ni vigogo wawili wa kisiasa kutoka jamii hii wanashikilia nafasi kuu katika serikali hii. Wao ni Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi,” anasema mchanganuzi wa kisiasa Martin Andati.

Bw Andati anahoji sababu za wabunge kutoka jamii ya Waluhya kutoiga mfano wa wenzao kutoka Mlima Kenya ambao waliungana na kumkaidi Rais William Ruto kwa kumwezesha Bw Mwangi Maina, almaarufu Karobia, kushinda kiti cha EALA.

Bw Maina hakuwa kwenye orodha ya watu watano walioidhinishwa na Dkt Ruto kwenye mkutano wa kundi la wabunge wa Kenya Kwanza (PG) katika Ikulu ya Nairobi.

Wao ni Hassan Omar Hassan, Zipporah Kering, David Sankok, Falhada Dekow na Fred Muteti. Miongoni mwa hao, Bw Muteti alifelishwa kufuatia njama iliyoendelezwa na wabunge wa Mlima Kenya.

  • Tags

You can share this post!

JUNGU KUU: Mlima umeanza kumteleza Rais?

DARUBINI YA WIKI: Toleo Nambari 12 | Novemba 20, 2022

T L