• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 8:09 PM
MIKIMBIO YA SIASA: Mudavadi ahisi tetemeko kuu

MIKIMBIO YA SIASA: Mudavadi ahisi tetemeko kuu

HUKU chama Amani National Congress (ANC) kikijiandaa kwa kura za mchujo zinazoanza Jumanne, Aprili 12, imebainika kuwa chama hicho kimepoteza wawaniaji wengi katika ngome yake ya Kaunti ya Vihiga.

Hatua ya kiongozi wa chama hicho Musalia Mudavadi kujiunga na chama cha United Democratic Alliance (UDA) Januari mwaka huu, mawimbi ya muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya na hofu kwamba baadhi ya wawaniaji wanapendelewa ni miongoni mwa sababu zilizochangia wanasiasa hao kuhamia vyama vingine.

Vihiga ni nyumbani kwa Bw Mudavadi ambaye pia ni mmoja wa vinara ndani ya muungano wa Kenya Kwanza, unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto.

Mmoja wa wanachama nyota kutoka kaunti hiyo ambao wamegura ANC ni Seneta wa Vihiga George Khaniri ambaye amehudumu katika wadhifa huo kwa mihula mwili kwa tikiti ya chama hicho.

Bw Khaniri anasema alijiunga rasmi na chama cha United Democratic Party (UDP) mnamo Machi 23, 2022, atakachokitumia kuwania ugavana wa Vihiga katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Chama cha UDP kinaongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Lugari Cyrus Jirongo na ni mojawapo ya vyama tanzu katika muungano wa Azimio la Umoja –One Kenya.

Bw Khaniri ambaye pia amewahi kuhudumu kama Mbunge wa Hamisi tangu 1997 hadi 2013, alimsuta Bw Mudavadi kwa kufanya uamuzi “kivyake” kujiunga na Naibu Rais pasi kushauriana na wanachama wa ANC.

“Chama changu sasa ni UDP. Tuko ndani ya Azimio kwa sababu tunataka kiongozi ambaye atapambana na ufisadi wala sio wale watakaoturejesha katika hali ya sasa ambapo uovu huu umeharibu uchumi,” Bw Khaniri akasema akiongeza kuwa madiwani wengi wa ANC walihama pamoja naye kuelekea UDP.

Anaongeza: “Tunataka kujihusisha na Raila Odinga ambaye ni mwanamapinduzi na mtetezi wa demokrasia. Ndugu yangu Mudavadi alifanya uamuzi wake lakini mimi na wenzangu hatutafuata mkondo wake.”

Mbunge Maalum Godfrey Osotsi ni mwanachama mwingine aliyehama rasmi ANC kabla ya kukamilika kwa makataa ya hadi Machi 26, 2022, kulingana na sheria mpya ya Vyama vya Kisiasa.

Mbunge huyo ambaye aliasi sera na uongozi wa chama hicho tangu 2018, sasa atawania useneta wa Vihiga kwa tikiti ya chama cha ODM.

“Binafsi nilikosana na Mudavadi miaka mitatu iliyopita nilipong’amua kuwa ni kiongozi asiye na msimamo thabiti kuhusu masuala muhimu ya kitaifa na hasa jamii yetu ya Waluhya. Hii ndiyo maana nimeamua kujiunga na Raila Odinga ambaye ni kiongozi mwenye maono na ambaye sera zake zitaleta manufaa kwetu,” anaeleza.

Naye Katibu wa Kaunti ya Vihiga, Bw Francis Ominde, ambaye alikuwa mwanachama wa ANC, amejiunga na chama cha Federal Party of Kenya (FPK) na kutangaza kuwa atawania ugavana. Bw Ominde ameripotiwa akidai kuwa alichukua hatua hiyo baada ya kupata fununu kwamba ANC inapania kutoa tikiti ya moja kwa moja kwa Mbunge wa Sabatia Alfred Agoi. “Siwezi nikashiriki mchujo katika ANC ilhali tayari ANC imetoa tikiti ya moja kwa moja kwa Mheshimiwa Agoi,” mwanasiasa huyo akanukuliwa akisema. Hata hivyo, Bw Agoi amekana madai hayo.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Mark Oloo anaonya kuwa hatua ya wanachama wengi wa ANC kuhamia vyama vingine itaathiri pakubwa ushawishi wa Bw Mudavadi ndani ya muungano wa Kenya Kwanza.

“Ushawishi wa mwanasiasa yeyote yule kitaifa hutegemea pakubwa nguvu za chama chake haswa katika ngome yake ya Magharibi mwa Kenya. ANC haina nguvu katika eneo hilo sasa baada ya wabunge wengi kuhamia ODM na DAP-Kenya,” akaeleza.

Kufikia sasa Bw Mudavadi amesalia na wabunge Bw Agoi, Omboko Milemba (Emuhaya) na Arnest Kivai (Vihiga), kutoka kaunti yake ya Vihiga. Mbunge wa ANC aliyesalia mwaminifu ni Mbunge wa Nambale Bw Sakwa Bunyasi. Awali, wabunge; Tindi Mwale (Butere), Peter Nabulindo (Matungu), Askofu Titus Khamala (Lurambi), Oku Kaunya (Teso Kaskazini) na Christopher Aseka waligura ANC na kujiunga na ODM.

  • Tags

You can share this post!

JUNGU KUU: Ukosoaji wa Ruto wamletea presha

Simanzi watu sita wakiangamia Murang’a baada ya moto...

T L