• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
JUNGU KUU: Ukosoaji wa Ruto wamletea presha

JUNGU KUU: Ukosoaji wa Ruto wamletea presha

NA BENSON MATHEKA

HATUA ya Naibu Rais, Dkt William Ruto ya kukosoa serikali imemsawiri kama kiongozi aliyeshindwa kutekeleza au asiyefahamu majukumu yake ya kikatiba.

Ingawa alisema alichukua hatua hiyo kwa kuwa upinzani unaopaswa kukosoa serikali umejiunga na serikali kupitia handisheki ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, wachambuzi wa siasa na utawala wanasema ni kinaya kwa naibu rais wa nchi kurushia lawama serikali akiwa ofisini.

Mnamo Jumanne wiki hii, Dkt Ruto aliongoza wabunge washirika wake kukosoa vikali serikali kufuatia uhaba wa mafuta nchini akidai ilishindwa katika jukumu lake la kukinga Wakenya. Na baada ya bajeti kusomwa Alhamisi, washirika wake walidai haikuwa ya kikatiba.

Kulingana naye, uhaba wa mafuta ulitokea kwa kuwa viongozi wa serikali hawajali raia huku wakitoa kipaumbele kwa maslahi yao ya kibiashara.

Kinaya ni kuwa alihoji, japo ni madai tu, kwa nini pesa zilielekezwa kulipa madeni ambayo yalifadhili miradi anayojigamba alianzisha.

Alipokuwa akihutubia wanahabari katika makazi rasmi ya naibu rais mtaani Karen, ikulu ya Nairobi ilitoa taarifa kwamba Rais Kenyatta alikuwa ametia saini sheria ya kuwezesha serikali kulipa kampuni za kuuza mafuta pesa zilizodai.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa Brian Okwemba, hatua ya Dkt Ruto inatokana na ujeuri wake wa kutaka kupaka tope serikali ilhali yuko ndani ya serikali yenyewe.

“Amekuwa akifanya hivi mara kadhaa hasa alipodai kuwa miradi yote mikubwa ya serikali ya Jubilee ilipangiwa katika ofisi yake. Kinaya ni kuwa ni ofisi hiyo anayotumia kukosoa serikali,” asema Bw Okwemba.

Wachanganuzi wa siasa wanasema kwamba anafaa kujiuzulu ili aweze kukosoa serikali akiwa nje yake ikiwa haridhishwi na utendakazi wake.

“Viongozi wenye busara hujiuzulu wakitofautiana na sera na maamuzi ya serikali lakini Dkt Ruto amekataa kujiuzulu kwa hivyo hafai kukosoa serikali inayomlipa mshahara na kufurahia manufaa yote ya cheo chake,” asema Okwemba.

Dkt Ruto amekuwa akipuuza wanaotaka ajiuzulu akiwemo Rais Kenyatta akisema kuwa alichangia ufanisi wa serikali ya Jubilee.

Kinaya ni kuwa ingawa amekuwa akikosoa handisheki kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga, amekiri kuwa Rais Kenyatta alimfahamisha kabla ya muafaka wake na kiongozi huyo wa upinzani.

Michael Kimongo, mchanganuzi wa siasa ambaye pia ni mtaalamu wa utawala, anasema kwamba anachofanya Dkt Ruto ni kupaka tope Rais Kenyatta kwa kutomchagua kuwa mrithi wake.

“ Tunayoshuhudia kutoka kwa Dkt Ruto ni hasira kwa kukosa kuungwa mkono na Rais katika azma yake ya urais. Hii ndio sababu amekuwa akishambulia mkubwa wake na serikali,” asema Kimongo.

Mnamo Jumatano, Dkt Ruto aliongoza kikao kati ya serikali za kaunti na serikali ya kitaifa (IBEC) siku moja baada ya kudai alilazimika kujaza pengo la upinzani baada ya Bw Odinga kuzika tofauti zake na Rais Kenyatta.

Rais Kenyatta amekuwa akisisitiza kuwa Bw Odinga hayuko serikali wala hakutoa sharti ya kugawiwa serikali kwenye mazungumzo yaliyozaa handisheki yao ya Machi 9 2018.

Wadadisi wansema akiwa Naibu Rais, Dkt Ruto anafaa kupima kauli zake hata kama ni msimu wa uchaguzi hadi pale kampeni zitakapoanza rasmi

  • Tags

You can share this post!

Tiketi zinavyoweka Ruto mbele ya Raila

MIKIMBIO YA SIASA: Mudavadi ahisi tetemeko kuu

T L