• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 3:21 PM
MITAMBO: Kifaa cha kukausha mazao kuwafaidi wakulima wadogo

MITAMBO: Kifaa cha kukausha mazao kuwafaidi wakulima wadogo

NA RICHARD MAOSI 

WAKULIMA wengi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za kuhifadhi mazao yao mara tu baada ya kuyavuna, jambo ambalo huwafanya kupata hasara kwa kukosa njia bora za kuyahifadhi.

Hata hivyo, teknolojia na mbinu tofauti zinaendelea kuibuliwa na baadhi wamejifunza kutumia mitambo inayotumia miale ya jua au kifaa cha dehydrator, ambayo mara nyingi hutumika kwenye viwanda vya kutengeneza aina mbalimbali ya vyakula vilivyosindikwa.

Ndiposa kukavumbuliwa kifaa kidogo cha dehydrator ambacho kinaweza kukausha asilimia ndogo ya mazao kwa awamu, ili kukidhi mahitaji ya wakulima wenye kipato kidogo.

Mmoja wa wale waliofaidi kutokana na kifaa hiki ni Elizabeth Njoroge, mkulima wa viungo kutoka eneo la Kianjogu Kaunti ya Kiambu , ambaye ameamua kuwaelimisha wakulima namna ya kupunguza uwezekano wa kuyapoteza mazao hususan wakati ambapo hakuna soko.

Kifaa hiki kidogo cha dehydrator ni mwafaka zaidi kwa wakulima wadogo kwani hutumia kiwango kidogo cha nishati ya umeme. PICHA | RICHARD MAOSI

Elizabeth ambaye vilevile anafanya kazi katika shirika la Christian Aid eneo la Westlands, Kaunti ya Nairobi, hutumia shirika lao la kibinafsi kuwahimiza wakulima kutumia mifumo ya kisasa kuendesha kilimo kidijitali.

Kwanza anashauri kuwa ili kuepuka kero ya mabadiliko ya hali ya hewa na vile vile tabianchi ambayo mara nyingi haiwezi kutabirika, mkulima anaweza kutumia utaratibu wa kuyapanda mazao yake nyakati tofauti ili yakomae muda tofauti.

“Hii itasaidia kero ya mazao kukomaa kwa wakati mmoja.Vilevile humsaidia mkulima aendelee kutafuta soko mazao mengine yakiwa shambani,” anaeleza.

Anaungama kuwa mazao hususan mboga za majani huanza kupoteza ubora wake mara tu baada ya kuvunwa kutoka shambani, kwa sababu huanza kunyauka na hata kuoza endapo mkulima hana soko.

“Kuyahifadhi mazao katika mazingira baridi au kukausha katika jua kali, ni njia mojawapo ya kuyatunza mazao kwa muda mrefu yakisubiri kutafutiwa soko,” anasema.

Miale ya jua husaidia kupunguza uzito wa mazao kwa kuondoa unyevu na majimaji.

Vile vile husaidia kurahisisha usafirishaji kwa sababu mazao yaliyokaushwa yanaweza kupakiwa kama poda kwa ajili ya matumizi mbalilmbali kama vile kutengeneza viungo vya lishe.

Kwa mfano, kilo 10 za karoti zinapokaushwa hutoa kilo moja ya poda ya karoti.

“Awali wakulima wengi walikuwa wakikata mboga vipande vidogo vidogo kisha kuzitandaza juu ya karatasi ya nailoni ili ziweze kupoteza maji. Lakini mifumo ya teknolojia imekuja na njia mbadala ambazo ni bora zaidi, zinazofanya kazi kwa wepesi na kumpatia mkulima faida ya muda mrefu,” anasema.

Anaongeza, “Mbali na kutumia miale ya jua pia mkulima anaweza kutumia kifaa cha dehydrator ambacho hutumia stima na huchukua takriban muda wa saa tano kukausha mimea.”

Ijapokuwa kifaa hiki kinaweza kuwa ghali ikilinganishwa na kifaa kinachotumia jua cha solar drier, matumizi yake huwa ni mepesi na huchukua muda mfupi kukausha mazao.

Aidha mazao yanayokaushwa kupitia mfumo huu, huwa na ubora wa hali ya juu kwa sababu kupitia kifaa hiki, mkulima anaweza kuratibu kiwango cha joto ambacho kitahitajika kukausha mazao yake.

Elizabeth anahimiza kuwa kifaa hiki kidogo cha dehydrator ni mwafaka zaidi kwa wakulima wadogo kwani hutumia kiwango kidogo cha nishati ya umeme.

Pili, kinaweza kutumika mijini na mashambani mradi mhusika apate mazao ya shambani.

Paul Nyongesa kutoka kijiji cha Sikali kilichoko Kaunti ya Kakamega akionyesha matumizi ya solar drier ndogo ambayo hutumika kukausha mazao kwa muda wa saa 12-24 kulingana na hali ya hewa. PICHA | RICHARD MAOSI
  • Tags

You can share this post!

Pep akiri Arsenal ni moto zaidi

Mshukiwa wa ulaghai akana kuwapunja wauzaji magari Sh3...

T L