• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
MITAMBO: Kifaa kinachopima ubora wa maziwa na kuepusha hasara

MITAMBO: Kifaa kinachopima ubora wa maziwa na kuepusha hasara

NA RICHARD MAOSI

KILA mkulima, mfugaji au mfanyabiashara huwa na matarajio ya kujiundia faida katika shughuli anazoendesha.

Kwa wafugaji ng’ombe wa maziwa au wenye viwanda vya maziwa, kupata maziwa salama ni jambo wanalolizingatia kwa kina.

Maziwa yanaweza kuathiriwa ikiwa ngo’mbe inatatizwa na maradhi kwa chuchu zake, masalio ya dawa iliyopuliziwa, kukama kwa kutumia mikono michafu, miongoni mwa sababu nyingine.

Kwa hivyo, ili mfugaji kujiepusha na hasara ya kurudishiwa maziwa na viwanda vya kununua maziwa, anaweza kuchukua sampuli ya maziwa yake ili kuyapima kwa kutumia kifaa cha Alcohol Milk Testing Gun.

Gabriel Kwendo ambaye ni muuzaji maziwa na pia anatengeneza bidhaa za yoghurt, anasema kuwa uchuuzi wa maziwa unafaa kudhibitiwa ili kuwakabili wauzaji wanaotumia njia za mkato kuwapunja wanunuzi.

“Kifaa hiki kina uwezo wa kutambua hadhi ya maziwa endapo yanaafikia kanuni za uuzaji wa maziwa kwenye kiwango cha kitaifa na kimataifa,” anasema Kwendo.

Kwendo ambaye amebobea kwenye maswala ya mifugo na mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu Cha Egerton, anasema sifa za maziwa zinaweza kubainika mara moja baada ya muuzaji kuyachemsha.

Alifichulia Akilimali kuwa maziwa huanza kubadilika pindi tu yanapotiwa mekoni, ndio sababu kifaa hiki kilizinduliwa ili kuwasaidia wanunuzi wa maziwa hasa vyama vya ushirika kukwepa hasara.

Pili, wavumbuzi walilenga kuwakinga wanunuzi dhidi ya maziwa mabovu ambayo yamejaa sokoni, ikizingatiwa kuwa si wakulima wengi wanafahamu maradhi yanayoweza kutokana na vimelea wanaokaa ndani ya maziwa.

Utaratibu wa matumizi ya kifaa cha Alcohol Milk Testing Gun

Anasema kabla ya kuyapima maziwa kifaa cha Alcohol gun hunyonya asilimia 20 ya mvinyo wa ethanol ambao huchanganywa na asilimia 80 ya maji safi.

“Milimita tano ya maziwa hatimaye huchukuliwa na kuchanganywa na mseto wa mvinyo wa ethanol ili kutambua endapo maziwa yatakuwa yameongezewa kitu kingine kama vile maji,” asema.

Kwendo anasema kuwa matumizi ya kifaa hiki huwa ni mepesi na wanunuzi wa maziwa wanaweza kukitumia ili kuyachunguza maziwa kabla ya kutengeneza bidhaa kama vile mala.

Gabriel Kwendo kutoka Comrades Dairy Nakuru akionyesha matumizi ya kifaa cha Alcohol gun, ambacho hutumika kupima ubora wa maziwa. PICHA | RICHARD MAOSI

Kutoka hapo matone ya mvinyo kutoka kwa Alcohol gun, hunyunyizwa juu ya milimita tano ya maziwa.

Anasema ikiwa sampuli ya maziwa yataganda humaanisha kuwa huenda yameongezewa maji, au mifugo wana maradhi ya chuchu, na hivyo basi si salama kwa matumizi.

Aidha anasema kuwa amekuwa akitumia kifaa hiki ili kujua endapo amekuwa akiyanunua maziwa kwa ajili ya usindikaji, usalama na ubora wake.

Kifaa cha Alcohol gun, ambacho hutumika kupima ubora wa maziwa. PICHA | RICHARD MAOSI

Anasema pia maziwa ambayo huwa yamekolea kiwango cha juu cha asidi au madini ya calcium , magnesium na patassium kupita kiasi hayafai kutumika kama lishe.

Hata hivyo, Kwendo anashauri kuwa ikiwa maziwa yatakuwa ni salama kwa matumizi ya binadamu huhifadhiwa ndani ya vyombo safi kisha yakachemshwa.

“Kutoka hapo yanaweza kutumika kutengeneza maziwa ya unga na bidhaa nyinginezo zenye ubora na thamani ya juu zinazompatia mkulima hela nzuri,” anasema.

Kwa siku za baadaye, Kwendo anasema kuwa kifaa hiki kitawasaidia wakulima kuwepo na huduma bora za afya ya mifugo na hatua za kuzuia maradhi ikiwemo chanjo za mara kwa mara.

  • Tags

You can share this post!

UhuRuto waliharibu ladha ya manifesto

UDA bado ndio kusema Mlima Kenya – Gachagua

T L