• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 7:55 AM
MITAMBO: Mfumo wa maji ya kufugia samaki na kukuza mazao

MITAMBO: Mfumo wa maji ya kufugia samaki na kukuza mazao

NA RICHARD MAOSI

MTINDO wa aquaponics ni mfumo wa uzalishaji chakula na kwa wakati huo mkulima anaweza kawafuga samaki hii ikiwa ni katika mazingira ya kutegemeana.

Mfumo huu unamuwezesha mkulima kupata kitoweo cha samaki kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na vilevile kuvuna mboga, kunogesha kilimo-biashara.

George Onyango ambaye ni mtaalam wa aquaponics anasema kuwa mfumo huu umekuja na faida nyingi kwani hupunguza matumizi ya maji bila mpangilio maalum.

Hatua kwa hatua maji hutoka kwenye matanki ya kufuga samaki kisha yanaelekezwa kwa ndoo zilizojazwa mawe aina ya pumice.

Kwa kawaida mawe ya pumice humiliki chembechembe ambazo hutumika kusafisha maji ya bahari, na vilevile huwa katika orodha ya lishe za kusafisha mwili wa binadamu.

Katika sehemu ya pili, maji yanaweza kufuata mkondo tofauti, yakaelekezwa kwenye bustani kukuza mboga au matunda na hatimaye mzunguko utakuwa umekamilika yanaporejea tena kwenye mazingira ya samaki.

Pili, anasema kuwa kupitia kwa mfumo huu hakuna haja ya mkulima kutumia mbolea za viwandani kwa sababu maji kwenye tanki la kufugia samaki huwa yamebeba virutubisho vyote muhimu.

Anaeleza kuwa hakuna haja ya kutupa taka zinazotokana na samaki ikizingatiwa kuwa mchakato mzima una uwezo wa kusafisha maji kabla ya kurejea tena kwenye mazingira ya kuhifadhi samaki.

“Hivyo basi ubora wa maji hubakia kuwa katika hali ya juu kwa uzalishaji wa samaki na kukuza mboga za majani au matunda,” asema.

Mtindo wenyewe hupunguza uharibifu unaotokana na wadudu au vimelea vinavyobeba maradhi kwa sababu maji huwa hayana udongo, ambao aghalabu ndio huchafua maji.

Anasema kuwa ukuaji wa mimea kupitia mbinu hii, ni wa kasi ya ajabu ikilinganishwa na njia za jadi ambazo zinategemea udongo tu kustawisha mimea.

“Uchafu unaopatikana ndani ya maji mara nyingi hutokana na madini ya phosphate, sulphur na nitrojeni ndani ya mbolea. Madini haya ndio hutengeneza asidi inayoangamiza samaki.

Onyango anasema wizara ya kilimo nchini iliona haja ya kubuni mfumo huu ili kuwasaidia wakulima kukabiliana na changamoto za uchafuzi wa vyanzo vya maji.

Aidha wataalam walilenga kutengeneza mazingira safi na salama kwa samaki kudumu kwani siku hizi mabomba ya majitaka hufunguliwa na kuchanganyika na maziwa au mito.

 

George Onyango akionyesha mfumo wa kusafisha maji kibayolojia kufuga samaki. PICHA | RICHARD MAOSI

Kupitia mtambo huu wa RAS, maji huvutwa kutoka kwenye aina spesheli ya tanki ya kulea samaki hadi kwenye ndoo ambazo huwa zimeunganishwa na paipu na kuangikwa katika sehemu ya juu.

Ndoo hizi huwa zimejazwa mawe spesheli ya pumice ambayo husafisha maji kibayolojia.

Onyango anaongezea kuwa maji haya yanaweza kuelekezwa shambani yakatumika kukuza mboga za sukumawiki, mnavu, kunde na hata spinach.

Kulingana na Onyango mtambo wa RAS unaweza kuwa wa manufaa kwa wakulima wanaoishi mijini, sehemu ambazo kuna uhaba wa mashamba kutokana na ongezeko la idadi ya watu.

“Mradi wenyewe unaweza kuendeshwa katika kipande kidogo cha ardhi ambapo mkulima anaweza kupata samaki wa kuuza na kwa wakati huo akavuna mboga za kutosha kwa ajili ya matumizi ya nyumbani,” anaeleza.

Tilapia na catfish, ndio spishi zinazopendekezwa kwa mfumo huu ambapo mara nyingi inashauriwa kufuga samaki wa jinsia moja.

You can share this post!

UJASIRIAMALI: Bidhaa zake zavutia wateja tele ughaibuni

Sakaja aruka kiunzi cha mwisho

T L