• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 1:20 PM
MITAMBO: Mtambo unaotawanya nafaka na maganda bila kuvunja mbegu

MITAMBO: Mtambo unaotawanya nafaka na maganda bila kuvunja mbegu

NA SAMMY WAWERU

WANASAYANSI na wataalamu wa masuala ya kilimo wanaendelea kutafiti mbegu bora za nafaka zinazostahimili athari za tabianchi.

Kiangazi na ukame, ni athari ambazo zimegeuka kuwa ratiba ya kila mwaka zikichangiwa na mabadiliko ya hali hewa.

Hali kadhalika, msambao wa magonjwa ya mimea na wadudu kama vile nzige wa jangwani, ni athari zilizotajwa kuchochewa na tabianchi.

Watafiti wanazidi kujituma kukabiliana na changamoto hizo, ili kuangazia baa la njaa na usalama wa chakula.

Hilo linaenda sambamba na mifumo ya uongezaji mazao thamani.

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Mimea na Uimarishaji Mifugo (Kalro), tawi la Katumani, Machakos linahusika na masuala ya mashine na mitambo – Amri, limeibuka na mashine ya kisasa kutawanya nafaka na maganda yake, bila kuvunja punje.

Maarufu kama ‘multi crop thresher’, inadondoa nafaka kama vile mawele, wimbi, mtama, kunde na mbaazi.

Kulingana na Mhandisi Nasirembe Wanjala kutoka Amri, mtambo huo pia unatawanya mbegu za mboga kama vile mchicha (almaarufu terere) na za nafaka zingine kutoka kwenye maganda.

Mtambo huo unatumia mafuta ya dizeli, petroli au nguvu za umeme.

“Anachofanya mkulima, ni kubadilisha vichujio na kuweka kinachoandamana au kuwiana na kipenyo (diameter) cha nafaka,” Mhandisi Wanjala aelezea.

Mhandisi Wanjala Nasirembe kutoka Kalro tawi la Machakos – Amri, akieleza jinsi multi crop thresher inavyofanya kazi. PICHA | SAMMY WAWERU

Kulingana na afisa huyo, nafaka zinapaswa kuwa zimekauka vyema, ili kudondolewa.

Kasi ya mashine hiyo ya kisasa, inaweza kuongezwa au kupunguzwa ambapo maganda huondolewa na kupeperushwa na kusalia na nafaka safi.

“Mashine aina nyingine huvunja punje, ila multi crop thresher imeboreshwa kwa zaidi ya asilimia 95,” Wanjala akaambia Akilimali, akisifia namna mashine hiyo inavyofanya kazi.

Chini ya saa chache, alisema mashine hiyo inafanya kazi ambayo badala yake ingetekelezwa kwa siku kadhaa.

“Inadondoa kwa dakika,” akasisitiza.

Aidha, nafaka zilizodondolewa ni tayari kupakiwa, kuliwa na hata kusagwa kinyume na za mashine nyingine ambazo lazima zikaguliwe kuondoa maganda yaliyosalia.

Mhandisi Wanjala Nasirembe, kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Mimea na Uimarishaji Mifugo (Kalro), tawi la Katumani, Machakos linalohusika na masuala ya mashine na mitambo – Amri. PICHA | SAMMY WAWERU

Katika makala ya pili ya kongamano na maonyesho ya Muungano wa Wadauhusika Sekta ya Kibinafsi katika Kilimo (ASNET) 2022, Amri ilikuwa miongoni mwa taasisi za serikali zilizohudhuria.

Hafla hiyo iliandaliwa katika makao makuu ya Kalro, jijini Nairobi.

  • Tags

You can share this post!

Mwalimu kizimbani kwa kumnajisi mwanafunzi

IMF yahujumu ahadi watoazo Ruto, Raila

T L