• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 8:55 AM
MITAMBO: Mtambo wa kuondoa chumvi kwenye maji yatumike kuendeleza kilimo

MITAMBO: Mtambo wa kuondoa chumvi kwenye maji yatumike kuendeleza kilimo

NA SAMMY WAWERU

WASHIRIKA katika mtandao wa uzalishaji wa chakula wamekuwa wakihimiza wakulima kukumbatia mifumo ya kisasa kuendeleza zaraa.

Kuanzia wadauhusika, Wanayasansi na watafiti, wanasisitiza kwamba suala la uhaba wa chakula nchini litaangaziwa endapo wakulima watatumia teknolojia za kileo kukuza mimea.

Athari za tabianchi ni bayana, janga la ukame likiwa ratiba ya kila mwaka Kenya.

Kero ya wadudu kama vile nzige wa jangwani na magonjwa, inazidi kuhangaisha sekta ya kilimo.

Huku baadhi ya maeneo nchini wakazi wakikosa kuingilia kilimo kwa sababu ya changamoto za maji ya chumvi, teknolojia kuziangazia imeibuka.

Agrigreen, kampuni yenye makao yake makuu Israili, imevumbua mtambo unaoondoa chumvi kwenye maji na kuyafanya yatumike kukuza mimea.

Maarufu kama Alvatech, ina kifaa ‘kinachoyatakasa’ kwa kutoa chembechembe za Sodium na Chloride, kulingana na Yariv Kedar, Mkurugenzi Mkuu Agrigreen Consulting Corp Ltd – Kedar GAP Group, Afrika.

“Ulivumbuliwa miaka miwili na nusu iliyopita Israili, na kufanyiwa majaribio Uingereza,” Kedar aelezea.

Alvatech inatumia kawi ya sola, iliyounganishwa na mfereji unaopampu maji ukiyaelekeza kwenye mimea au shambani, baada ya kutakaswa.

“Ina mfereji mwingine wa kuyaingiza mtamboni kuondolelewa chumvi,” asema afisa huyo.

“Maji ya visima, vidimbwi na mabwawa yenye chumvi yanaweza kutumika katika shughuli za kilimo kupitia mtambo wa Alvatech,” afafanua.

Agrigreen imekuwa ikiendeleza miradi kuhamasisha wakulima kuhusu teknolojia hiyo kwa ushirikiano na Shirika la Msalaba Mwekundu, Kedar akiambia Akilimali tayari baadhi ya wakulima Lamu wameikumbatia.

Maeneo mengine ni Kaskazini Mashariki mwa Kenya, afisa huyo akisema si ajabu sehemu hizo zikijiunga na mtandao wa uzalishaji mazao ya kilimo nchini.

“Mfano maji ya Ziwa Turkana ambayo yana chumvi, kwa kutumia Alvatex yanaweza ‘kusafishwa’ wakazi wayatumie kulima na kuangazia uhaba wa chakula,” asema mtaalamu huyo mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 40 katika kilimo.

Utendakazi wa mashine hiyo, kulingana na Kedar, unaokoa matumizi ya maji kwa asilimia 20 – 30.

Bei, mtambo wa gharama ya juu ni Dola 11,000 (sawa na Sh1,296, 570 pesa za Kenya).

“Zipo mashine za Dola 1, 900 (Sh223,953),” adokeza, akiongeza kuwa Agrigreen imeanza kushirikiana na benki na mashirika ya kifedha yanayotoa mikopo kupiga jeki wakulima wakumbatie mfumo huo, kupitia mpango wa malipo ya polepole.

Akisifia mtambo huo kama ‘bongo la maji’, hata hivyo anasema hayapaswi kunywewa na watu.

Yariv Kedar, Mkurugenzi Mkuu Agrigreen akifafanua kuhusu mashine ya Alvatech ambayo huondoa chumvi kwenye maji ili yatumike katika kilimo. PICHA | SAMMY WAWERU

Agrigreen ilikuwa miongoni mwa kampuni zilizoshiriki kongamano la Avokado Afrika 2022, mwezi uliopita, Juni, lililoandaliwa na Chama cha Ushirika cha Kitaifa cha Wazalishaji Maparachichi (ASOK).

“Athari za tabianchi zinaendelea kutatiza mazingira na shughuli za kilimo, tunahimiza wakulima wa avokado wakumbatie mifumo ya kisasa kuendeleza jitihada zao,” akashauri Ernest Muthomi, Afisa Mkuu Mtendaji ASOK.

Alitaja unyunyiziaji mimea na mashamba maji kwa mifereji na teknolojia za uongezaji mazao thamani, kama baadhi ya mifumo wanayopaswa kukumbatia kuboresha kilimo cha avokado.

“Ukizuru Italia, masoko na maduka ya nchi hiyo hayana maparachichi kutoka Kenya. Tukaze kamba kuongeza kiwango tunachokuza,” akahimiza.

Kenya imeorodheshwa taifa la saba bora ulimwenguni kuuza mazao ya avokado nje ya nchi.

  • Tags

You can share this post!

Dereva afungwa jela miaka mitatu kwa kuua mtoto wa Naibu...

Ushirikiano wa kibiashara waimarika baada ya DRC kujiunga...

T L