• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 10:27 AM
MITAMBO: Smoker itakusaidia kukaribia mzinga na kuvuna asali murwa

MITAMBO: Smoker itakusaidia kukaribia mzinga na kuvuna asali murwa

NA RICHARD MAOSI

WAKULIMA wengi huingilia ufugaji wa nyuki kwa lengo la kurina asali.

Ufugaji huo unatambuliwa kama mojawapo ya shughuli ambazo zinaweza kutunza misitu, kwa njia endelevu ya kuongeza kipato kwa mjasiriamali.

Soko la asali ni kubwa, kwa sababu si wakulima wengi wanaojihusisha na aina hii ya kilimo, baadhi wakiwa na dhana kuwa ni shughuli hatari, ambayo huendeshwa na watu wenye kipato cha chini.

Hata hivyo, mambo ni tofauti kwa mkulima Moses Kiptoo Arap Suge kutoka eneo la Mlango, Kaunti ya Nandi.

Amekuwa akihamasisha wakulima wazingatie faida pana za ufugaji nyuki na si kupata asali pekee.

Mbali na kuuza asali, Kiptoo ambaye ni mfugaji mzoefu wa nyuki, anatoa ushauri nasaha kwa wakulima wadogo ikiwa ni pamoja na kuwafunza namna ya kutunza nyuki.

Vilevile, anafanya shughuli ya kuchonga mizinga aina ya Langstroth Hives, na kutengeneza vifaa vinavyofahamika kama smoker, kifaa kinachotumika wakati wa kuvuna asali.

“Kifaa cha smoker kinachoagizwa kutoka Marekani huuzwa Sh4,500, ilhali kile kinachoundwa humu nchini ni Sh2,000 ingawa matumizi yake huwa ni sawa,” anaeleza.

Kiptoo ambaye alijifunza namna ya kufuga nyuki katika taasisi ya Bee Keeping Station Lenana, anasema kuwa wakulima wengi kutoka kaunti ya Nandi wamekuwa wakifuga nyuki kwa ajili ya kupata asali inayotumika nyumbani, wakati mwingine ikichanganywa na dawa.

“Mbali na kutengeneza tiba za kiasili kuna aina nyingine tisa ya bidhaa zenye thamani ya juu kuliko asali, ambazo hutokana na nyuki,” anaeleza.

Anasema kuwa asali ni chakula hivyo basi mrinaji anastahili kudumisha usafi wa hali ya juu kuanzia wakati wa kuvuna mpaka hatua ya kupakia, ambapo anaungama kuwa asali ya hadhi ya juu ni lazima iwe na ubora zaidi.

Anaongezea kuwa zamani wafugaji wa nyuki walikuwa wakitumia moto kuwachoma nyuki, jambo ambalo mara nyingi lilifanya asali kuwa na rangi nyingi tofauti.

Kitaalam asali inafaa kuwa na rangi moja tu ya nta hii ndio maana wakulima wanashauriwa kuendesha kilimo cha nyuki katika maeneo ambayo ni mbali na makazi ya watu, mazingira mazuri yenye spishi mbalimbali za mimea inayozalisha chakula cha nyuki.

Pia anashauri kuwa uvunaji wa asali unafaa kufanyika mchana, wakati ambapo kuna mwangaza wa kutosha ili kumzuia mrinaji asije akachafua asali.

Aidha anaonya kuwa kemikali isichanganywe na mabomba ya kutoa moshi.

Yeye hutumia kifaa kinachofahamika kama smoker ambacho ni chombo maalum kinachoshindiliwa pumba za mbao.

Kisha huwashwa moto na kupuliza moshi mzingani, jambo ambalo huwafanya nyuki kupata ulegevu.

Anasema kutokana na mitambo ya kisasa, mjasiriamali anaweza kuunda aina mbalimbali ya bidhaa kama vile sumu ya nyuki, mafuta ya nyuki, poleni, na gundi.

Kiptoo anasema kuwa bidhaa kama vile mafuta ya nyuki (royal jelly) hufanya ngozi kuwa laini kwa kuondoa chunusi na kumfanya mtumiaji asizeeke, ambapo kilo moja huuzwa Sh3,900.

Pili kuna poleni (pollen), ambayo husaidia kutibu maradhi ya kansa hususan saratani ya kizazi kwa wanaume kilo moja ikiuzwa Sh3,500.

Anaongezea kuwa sumu ya nyuki (bee venom) wakati huwa wamekasirika inaweza ikakusanyawa , kwani inaweza kutibu maradhi ya athritis.

Pia anaeleza kuwa mjasiriamali anaweza kutengeneza gundi ambayo mara nyingi hutumika katika sekta ya kutengeneza viatu, na kilo moja huuzwa Sh1,000.

You can share this post!

Vijana wa UDA Kilifi waendelea kumpigia debe Ruto aingie...

Urusi yashutumiwa kwa ‘kulinda’ waasi

T L