• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 8:50 AM
Mpango wa kandanda Githunguri kuokoa vijana kutoka kwa kero ya pombe na mihadarati  

Mpango wa kandanda Githunguri kuokoa vijana kutoka kwa kero ya pombe na mihadarati  

NA SAMMY WAWERU 

MBUNGE wa Githunguri Bi Gathoni Wamuchomba amezindua mpango maalum kusaidia kukabiliana na kero ya pombe na dawa za kulevya eneobunge lake, unaohusisha kukuza vipaji katika soka.

Mpango huo, maarufu kama Maathe Githunguri Grassroots Football (MGGF) unalenga wanafunzi wavulana walio na umri kati ya miaka 7 – 14.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali mapema wiki hii wakati wa uzinduzi wa mradi huo katika Uwanja wa Githunguri, Kaunti ya Kiambu, Bi Wamuchomba alisema oparesheni dhidi ya unywaji wa pombe haramu na matumizi ya dawa za kulevya na mihadarati itafanikishwa kwa kuanza na watoto.

Mbunge wa Githunguri, Gathoni Wamuchomba akiwa na baadhi ya wanafunzi wa Shule za Msingi eneobunge lake wakati wa uzinduzi wa mpango kuokoa watoto wavulana kutoka kwenye minyororo ya pombe na dawa za kulevya. Picha|SAMMY WAWERU

Huku takwimu za Mamlaka ya Kupambana na Pombe na Matumizi ya Dawa za Kulevya (NACADA) zikionyesha wengi wanaolemewa na kero hiyo hutekwa wakiwa chini ya miaka 10, mbunge huyo alisema mbinu ya kipekee kuokoa vijana na kizazi kijacho ni kwa kuwashirikisha kwenye michezo.

“Licha ya kuwa tunapambana kuokoa vijana walio kati ya miaka 18 – 35, changamoto ya pombe na dawa za kulevya inawanyemelea wakiwa hata na miaka 7,” Bi Wamuchomba alisema.

Gathoni Wamuchomba, mbunge wa Githunguri akihutubu wakati wa uzinduzi wa mpango kuokoa watoto wavulana eneobunge lake dhidi ya pombe na dawa za kulevya. Picha|SAMMY WAWERU

Sawa na maeneo mengine eneo la Kati, alitaja eneobunge la Githunguri analowakilisha bungeni kama mojawapo ya yaliyoathirika pakubwa.

Wamuchomba alisema kwa kushirikisha wavulana kwenye kandanda na michezo mingineyo, kama njia bora kuwachomoa kutoka ‘vituo’ na ‘mashimo’ yanayowateka kutumia pombe na mihadarati.

Isitoshe, mawazo ya watoto na vijana yanapokosa kutekwa kupitia mambo faafu na maendeleo, ninasikitika wengi wanapoteza muda wakitazama video chafu hatua inayochangia kuchafua maadili yao, akasisitiza.

Bi Gathoni Wamuchomba akitangamana na wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi za umma Githunguri wakati wa uzinduzi wa mpango kuokoa watoto wavulana kutoka kwa hatari ya pombe na matumizi yadawa za kulevya. Picha|SAMMY WAWERU

Ni kupitia mpango wa Mamacare Mentorship Program na Gathoni Wamuchomba Africa Foundation (Gamafrica), mbunge huyo amezindua Maathe Githunguri Grassroots Football unaolenga kunufaisha shule zote za msingi za umma Githunguri.

“Timu 51 zimepata mipira miwili kila moja, na wavulana wote sare maalum za soka,” Bi Wamuchomba akasema, akidokeza kwamba hatua hiyo ni mojawapo ya sera na ahadi alizotoa akiomba kura 2022 “kupiga jeki wavulana ili kuwaokoa kutoka kwa minyororo ya pombe na dawa za kulevya”.

Mpango wa Gathoni Wamuchomba unalenga kunusuru vijana eneobunge la Githunguri, wajiepushe na unywaji wa pombe na matumizi ya mihadarati kupitia kandanda. Picha|SAMMY WAWERU

Watakuwa wakishiriki tonamenti za mashinani kwa minajili ya kukuza talanta, anaoamini baadhi watafanikiwa kuchezea timu za kitaifa na hata vilabu vya kimataifa katika soka.

“Kila wadi Githunguri itakuwa ikiandaa michuano ya kandanda, na pia daraja la eneobunge tupate timu itakayomenyamana na timu za kitaifa. Tunaomba wasamaria na wahisani wajitokeze kutupiga jeki angalau tuwe tunatuza washindi.”

Uzinduzi wa MGFF uligharimu kima cha Sh2.2, Bi Wamuchomba akisema ufadhili ulifanikishwa na marafiki na wanafunzi wa zamani shule za msingi Githunguri waliojitokeza kumsaidia.

Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba akionyesha mipira aliyosambaza kwa zaidi ya timu 50 za shule za msingi za umma eneobunge lake kusaidia kuondoa vijana kutoka kwenye unywaji wa pombe na utumizi wa dawa za kulevya. Picha|SAMMY WAWERU

“Ninaamini vita dhidi ya pombe na mihadarati itafanikishwa kwa ushirikiano. Kupeleka walioathirika seli au jela, sio suluhu. Suluhu ni kulenga kinachowachochea,” alielezea, akiahidi kuwa mpango alioanzisha ni wa kudumu.

Uzinduzi huo pia ulifanikishwa kupitia ushirikiano na uongozi wa shule na pia kutoka idara ya elimu.

Gathoni Wamuchomba ametaja kushirikisha wanafunzi wavulana kwenye michezo kama mojawapo ya mbinu kuwaepusha kushiriki maovu. Picha|SAMMY WAWERU

“Tumeshuhudia baadhi ya wavulana wanafunzi wakishiriki unywaji pombe na kutumia dawa za kulevya. Mpango kuwahusisha kwenye soka, tunaamini utatusaidia kuokoa vizazi vijavyo na kuboresha elimu,” akasema Bi Nancy Kihara, Mkurugenzi Mkuu Idara ya Elimu Kaunti Ndogo ya Githunguri.

Bi Wamuchomba alisema sehemu ya mgao wa Fedha za Hazina ya Kitaifa ya Ustawishaji Maeneobunge (NG-CDF), 2024 atatenga kutumika kununulia wanafunzi na walimu magwanda maalum ya spoti.

Mradi mwingine anaoendeleza chini ya wakfu wake, ni kuangazia mimba za mapema miongoni mwa wanafunzi na kuwanunulia taulo za hedhi.

Mbunge wa Githunguri, Gathoni Wamuchomba akikagua gwaride la heshima la wanaskauti lililoandaliwa na mseto wa wanafunzi kutoka shule za umma eneobunge lake. Kando na kusaidia wavulana, pia ana mipango ya watoto wa kike. Picha|SAMMY WAWERU
  • Tags

You can share this post!

Maswali mazito yaibuka kufuatia kuongezeka kwa mashambulio...

Makahaba wa mijini wakubali mavuno ya shambani,...

T L