• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 2:24 PM
MUME KIGONGO: Mwanamume atunze afya kupata mbegu bora ya uzazi – Watafiti

MUME KIGONGO: Mwanamume atunze afya kupata mbegu bora ya uzazi – Watafiti

NA CECIL ODONGO

JAPO mwanamke ndiye hubeba mimba, mwanaume hutekeleza wajibu muhimu kwa kuwa lazima awe na mbegu bora za kiume ndipo mwanamke apate ujauzito.

Watafiti kutoka Chuo cha Kimatibabu cha Northwestern Marekani, wamebaini kuwa iwapo mwanaume hana mbegu bora za kiume basi hawezi kumpachika mwanamke mimba.

Kutokuwa na mbegu bora za kiume hutokana na mtindo wa maisha ya mwanaume, mazingira anakoishi na jeni zake.

Utafiti huo unasema kuwa mara nyingi iwapo mwanamke hawezi kupata ujauzito basi asilimia 40 ya tatizo hilo huchangiwa na mwanaume.

Ili kuepukana na hili, kati ya mambo mwanaume anahitaji kujizuia nayo ni unene kupita kiasi.

Wanasayansi wanasema unene huathiri ubora wa mbegu za kiume kwa kuharibu chembechembe za DNA ndani yake.

Pia aliye na unene kupita kiasi huwa na mbegu za kiume kwa uchache tena hafifu kwa hivyo si rahisi mpenzi wake kupata mimba.

Utafiti mwingine ulioendeshwa na wanasayansi Marekani mnamo 2012, ulibaini kuwa na mafuta mengi mwilini huathiri sio tu homoni za uume, bali hata nyingine ndani ya mwili wa mwanaume.

Pia, kudhibiti magonjwa kama sukari, shinikizo la damu na maradhi mengine sugu kunaweza kusaidia mwanaume kuwa na mbegu bora za kiume.

Hata hivyo, ni vyema iwapo mwanaume atashauriana na daktari kwa kuwa baadhi ya dawa zinazotumika kutibu magonjwa hayo nazo pia zinaweza kuathiri ubora wa mbegu za kiume.

Mwanaume anastahili kufanya mazoezi ya mara kwa mara ila kwa kipimo kisha pia kula vyakula vyenye vitamini kuepukana na tatizo hili.

Pia, hawafai kuvaa chupi ambazo zinabana sehemu zao za siri na waepuke kutumia mihadarati hasa uvutaji sigara.

  • Tags

You can share this post!

Qatar yaweka rekodi kwa kuandaa Kombe la Dunia katika...

JIJUE DADA: Lishe bora, usingizi mwanana ni njia bora ya...

T L