• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 10:55 PM
Muthama atafuna ngome ya Kalonzo

Muthama atafuna ngome ya Kalonzo

NA BENSON MATHEKA

MWENYEKITI wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) Johnson Muthama angali mwiba kwa kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka huku akisuka na kutekeleza mikakati ya kupunguza umaarufu wa makamu rais huyo wa zamani.

Bw Muthama ambaye alikuwa mshirika wa karibu wa Bw Musyoka kabla ya kuhama Wiper na kujiunga na Naibu Rais Dkt William Ruto miaka minne iliyopita, amekumbatia jina mpya la Kiamba, huku akijiandaa kugombea ugavana kaunti ya Machakos.

Mwanasiasa huyo anasema kwamba lengo lake ni kuona jamii ya Wakamba ikiungana kutetea maslahi yake na kuwa katika serikali ijayo.

“Palipo na mgawanyiko, jamii haipati maendeleo. Ninataka kuhakikisha jamii imeungana na eneo letu kuwa katika serikali ya William Ruto katika muungano wa Kenya Kwanza hata ninapogombea ugavana kaunti ya Machakos,” asema Bw Muthama.

Kulingana na wadadisi wa siasa, tatizo kubwa la Bw Musyoka katika ngome yake ya Ukambani ni Bw Muthama.

Wanasema kwamba seneta huyo wa zamani wa Machakos amekuwa akileta pamoja viongozi ambao wanagawanyika kwa sababu ya msimamo wa Bw Musyoka.

“Muthama anabomoa umaarufu wa Bw Musyoka kupitia mikakati yake ya kisiasa ya kuunganisha wakazi na viongozi. Ana ushawishi katika kaunti zote tatu za Ukambani jambo ambalo haliwezi kupuuzwa,” asema mdadisi wa siasa za Ukambani Karen Kioko.

Duru zinasema kwamba Bw Muthama anapanga mkutano mkubwa ambao utabadilisha kabisa siasa za Ukambani.

“Akiwa mwenyekiti wa UDA anafahamu jamii itanufaika chini ya serikali ya chama hicho. Mkutano huo utaleta pamoja viongozi wa kisiasa, kidini, kijamii, vijana, wanawake, wafanyabiashara, wataalamu na mashirika ya kijamii kutoka sehemu zote za Ukambani. Ninachojua ni kwamba wimbi la siasa za eneo hilo litabadilika baada ya mkutano huo,” asema diwami mmoja kutoka kaunti ya Makueni ambaye aliomba tusitaje jina kwa kuwa si msemaji rasmi wa Bw Muthama.

Bi Kioko anasema kwamba Bw Muthama ana nguvu za kifedha na anapendwa sio tu na wakazi wa Machakos bali katika kaunti za Kitui na Machakos.

“Mikakati yake lazima itayumbisha umaarufu wa Bw Musyoka ambaye huwa anachukua muda kufanya maamuzi ya kisiasa akisubiri kuidhinishwa na vigogo wengine wa kisiasa. Hata kama kiongozi huyo wa Wiper amekuwa akipigwa vita na magavana wa kaunti tatu za Ukambani, mwiba unaomsumbua ni Bw Muthama anayefahamu udhaifu na nguvu zake kisiasa,” asema mchanganuzi wa siasa John Kisilu.

Kulingana na Bw Kisilu, ubabe halisi wa msemaji wa jamii ya Wakamba ni kati ya Bw Musyoka na Bw Muthama.

“Hawa wawili wamekuwa washirika wa kisiasa kwa miaka mingi kabla ya kutofautiana. Musyoka amekuwa msemaji wa jamii akiungwa na Bw Muthama ambaye amekuwa akisuka mikakati ya kumvua mshirika wake wa zamani joho la msemaji wa jamii,” asema Kisilu.

  • Tags

You can share this post!

Hofu Ruto alijikwaa kisiasa nje

MALEZI KIDIJITALI: Kuwakinga wasichana matineja mtandaoni

T L