• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 5:15 PM
Hofu Ruto alijikwaa kisiasa nje

Hofu Ruto alijikwaa kisiasa nje

NA WANDERI KAMAU

NAIBU Rais William Ruto anaonekana kujikwaa zaidi kisiasa, kufuatia ziara yake katika nchi za Amerika na Uingereza iliyodumu kwa siku 12.

Dkt Ruto aliondoka nchini Februari 27, ambapo aliwahutubia Wakenya wanaoishi ng’ambo katika mataifa hayo mawili.

Nchini Amerika, Dkt Ruto alisema kuwa kuna njama za serikali kuiba kura kwenye uchaguzi wa Agosti, akiirai jamii ya kimataifa kuelekeza macho yake yote kwenye maandalizi ya uchaguzi huo.

Dkt Ruto alitaja vitisho kutoka kwa serikali na usaliti wa kisiasa kama changamoto kuu zinazotishia uchaguzi huo kuwa huru na wenye haki.

Nchini Uingereza, Dkt Ruto alimlaumu vikali Rais Uhuru Kenyatta kwa kuwa “skwota” kwenye serikali yake mwenyewe, kutokana na hatua yake kubuni ushirikiano wa kisiasa na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Vile vile, alisema kuwa hakutengewa majukumu yoyote rasmi na Rais Kenyatta licha ya kuwa naibu wake kwa miaka tisa.

Kufuatia kauli hizo, wadadisi wanasema Dkt Ruto alijipiga mjeledi wa kisiasa, ikizingatiwa matamshi yake yalikinzana na yale ambayo amekuwa akisema kwenye mikutano ya kampeni.

Wanasema Dkt Ruto aliihadaa jamii ya kimataifa, kwani licha ya kudai kutengwa na kuhangaishwa na idara mbalimbali za serikali, bado hajajiuzulu wadhifa wake.

“Ziara hizo zilikuwa nafasi bora kwa Dkt Ruto kujipigia debe kama kiongozi anayefaa zaidi kumrithi Rais Kenyatta. Alifaa kujiuza kama kiongozi bora kuliko washindani wake wakuu, kama vile Bw Odinga. Hata hivyo, ni kinaya kuwa alimshambulia Rais Kenyatta, akiwa bado hajajiuzulu nafasi yake. Wengi walifasiri hilo kama hadaa ya kisiasa,” asema Dkt Godfrey Sang’, ambaye ni mtaalamu wa mahusiano ya kimataifa.

Wadadisi wanasema kuwa kwa kumshambulia Rais Kenyatta ili kujisawiri kuwa “msafi”, Dkt Ruto alijiweka lawamani, kwani alionekana kushindwa kujibu baadhi ya maswali aliyoulizwa, kama hali ya kiangazi nchini na ahadi za serikali ya Jubilee ambazo walitoa pamoja na Rais Kenyatta mwaka 2013 na 2017.

Wanasema alionekana kuwa mnafiki, kwani licha ya kujisawiri kama mwathiriwa wa usaliti wa kisiasa, kesi yake bado inaendelea katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ambapo anahusishwa na tuhuma za kuwahonga na kuwatishia mashahidi.

“Dkt Ruto alisahau kuwa hadhira ambayo angekutana nayo ng’ambo ni tofauti na ile ambayo amezoea Kenya. Kinyume na Kenya, watu wanaoishi ng’ambo hufuatilia matukio yanayoendelea nchini kwa kina, hivyo ilitarajiwa angeulizwa maswali mazito,” asema Prof Macharia Munene, ambaye ni mhadhiri wa Historia na Mahusiano ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha USIU, Nairobi.

Wadadisi wanasema waandalizi wa ziara ya Dkt Ruto walikosa kumwandaa vilivyo kuhusu maswali ambayo angekumbana nayo, hasa kutoka kwa wanahabari wa mashirika ya habari ya kimataifa.

“Ugumu ambao Dkt Ruto alikumbana nao kujibu baadhi ya maswali ulidhihirisha wazi hakuwa amejitayarisha vilivyo kuyakabili. Ni hali ambayo imemsawiri kama kiongozi anayeficha ukweli fulani,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Ikizingatiwa Bw Odinga pia amepangiwa kufanya ziara nchini Uingereza hivi karibuni, ambapo pia atatoa hotuba katika majukwaa mbalimbali, wadadisi wanasema kuna uwezekano akamponda Dkt Ruto kwa kurejelea “mapungufu” yaliyojitokeza kwenye hotuba zake (Ruto).

Wanasema ushindani uliopo kati ya Dkt Ruto na Bw Odinga ni kupata uungwaji mkono wa kimataifa, ambapo Bw Odinga anaonekana kuwa mbele ikilinganishwa na (Ruto).

“Bw Odinga ndiye Balozi Maalum wa Afrika kuhusu Miundomsingi. Kwa upande mwingine, Rais Kenyatta amejizolea umaarufu mkubwa katika ngazi ya kimataifa kutokana na juhudi ambazo amechukua kuinua hadhi usemi na ushawishi wa Kenya. Hayo ni masuala mawili yanayomweka kifua mbele Bw Odinga ikilinganishwa na Dkt Ruto,” akasema Bw Muga.

Hata hivyo, washirika wa Dkt Ruto wanataja ziara hiyo kuwa yenye manufaa sana kwake kisiasa.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Boda: Msako kusitishwa ni nafasi ya kutafuta...

Muthama atafuna ngome ya Kalonzo

T L