• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Muturi yuko ngangari kuwania urais

Muturi yuko ngangari kuwania urais

Na WACHIRA MWANGI

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi anasisitiza kuwa hatajiondoa kutoka kinyang’anyiro cha urais huku akikabiliwa na shinikizo la kuwa mgombea mwenza wa Naibu Rais William Ruto.

Bw Muturi ambaye ametangaza kuwa atawania urais kwa tiketi ya chama cha Democratic Party (DP) aliwataka wapinzani wake kuwa tayari kwa ushindani mkali katika uchaguzi wa urais 2022.

“Siku moja katika siasa ni kipindi kirefu zaidi, kwa hivyo subiri tu. Nina washirika kote nchini. Nitaenda hadi mwisho. Kila mgombeaji aruhusiwe kuuza manifesto yake. Mimi ninasimamia uadilifu, uwazi na uwajibikaji,” akasema.

Bw Muturi alisema hayo jana baada mkutano wa kila mwaka kati ya tume za utumishi wa umma katika serikali kuu na serikali za kaunti. Mkutano huo wa mashauri ambao ulidumu kwa siku tatu uliofanyika katika mkahawa wa Travellers mjini Mombasa.

Bw Muturi vile vile alilaani mwenendo wa watumishi wa umma kuendeleza ubadhirifu wa pesa za umma nchi, akisema uovu huo unarudisha nyuma maendeleo nchini. Spika huyo alisema kuwa ipo haja kwa Bodi za Utumishi wa Umma kote nchini kuwa huru sio tu kwa maneno bali kwa vitendo.

“Ili bodi hizo ziweze kufanya maamuzi yao bila kuingiliwa, zinahitaji uwezo kifedha. Hii itawawezesha kuendesha shughuli zake bila kuingiliwa na magavana au maafisa wa serikali za kaunti. Sharti sheria ifanyiwe mabadiliko.

Bodi hizo ni asasi za kitaalamu ambazo zinawez kuwa na masuala ya kutekelezwa. Lakini sheria isipobadilishwa ili kuzipa ushuru, zitajipata kufanya yale ambayo magavana na maafisa wakuu katika serikali zao wanataka. Bodi hizo pia zinahitaji uwezo wa kifedha,” Spika Muturi akaeleza.

You can share this post!

Juventus washuka hadi nafasi ya tisa kwenye Serie A baada...

Watoto walemavu zaidi ya 200 Mukuru wapigwa jeki kielimu...

T L