• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
MWALIMU WA WIKI: Mwalimu kiongozi alengaye uhadhiri

MWALIMU WA WIKI: Mwalimu kiongozi alengaye uhadhiri

MWALIMU aliye na wito wa kufundisha na mapenzi ya dhati kwa taaluma yake, ana jukumu la kuchochea wanafunzi wake kupiga hatua kubwa katika safari ya elimu inayohitaji subira na moyo wa kujitolea.

Zaidi ya kuwafahamu wanafunzi wake kwa jina, mwalimu bora sharti awe na bidii na msukumo wa kutaka kujifunza mambo mapya. Awe mwepesi wa kuchangamkia masuala yanayofungamana na mtaala na asome kutoka kwa vyanzo mbalimbali ili awe chemchemi ya maarifa kwa wanafunzi wanaomtegemea.

Haya ni kwa mujibu wa Bi Margaret Njogu ambaye sasa ni Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika shule ya Magomano Girls, Kaunti ya Nyandarua.

Kwa mtazamo wake, mwalimu bora lazima ajitahidi kuhudhuria vipindi vyote, awe mnyumbufu katika maandalizi ya vipindi hivyo vya masomo na mbunifu katika uwasilishaji wa anachokifundisha.

“Atoe mazoezi ya kutosha kwa wanafunzi, arejeshe masahihisho ya kazi zao mapema na awape matokeo ya majaribio ya mitihani kwa wakati unaofaa. Anastahili pia kutumia nyenzo anuwai za ufundishaji zitakazowaamshia wanafunzi ari ya kuthamini masomo na kukuza vipaji vyao,” anasema.

Margaret ana shahada ya ualimu (Kiswahili/Muziki) kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta (1999-2003). Alilelewa katika eneo la Kagumo, Kaunti ya Kirinyaga na alianza masomo katika shule ya msingi ya Kiamaina, Kagumo, kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Kiburia Girls iliyoko Gichugu, Kirinyaga (1994-1997).

Kabla ya kufuzu chuoni, alishiriki mafunzo ya nyanjani katika shule ya Kiburia mnamo 2003 na akaamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi. Aliwahi pia kufundisha katika shule ya St Philip’s, Embu (2003-2004) kabla ya kuhamia shule ya Ngorika, Nyandarua (2005-2007) kisha St Anuarite Girls iliyoko Njabini, Nyandarua (2007-2008).

Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimwajiri 2008 na kumtuma kufundisha katika shule ya Karoti Girls, Kirinyaga. Alihudumu huko kwa miaka sita kabla ya kuhamia Magomano Girls mnamo 2014.

Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Ushauri Nasaha mnamo 2017 kabla ya kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili. Aliwahi kuwa Kaimu Naibu wa Mwalimu Mkuu wa Magomano Girls kati ya 2021 na 2022.

Mbali na ualimu, Margaret pia ni mshairi shupavu na mwanafasihi chipukizi. Alichapishiwa ‘Mwongozo wa Tamthilia ya Kifo Kisimani’ (Kithaka wa Mberia) mnamo 2009 na sasa ana mswada wa diwani ya mashairi uliopo katika hatua za mwisho mwisho za uhariri.

Tangu mwaka wa 2014, Margaret amekuwa mstari wa mbele kushirikisha wanafunzi wake katika mashindano ya ngazi na viwango tofauti kwenye tamasha za kitaifa za muziki (KMF). Shairi lake ‘Anasa’ lililokaririwa na wanafunzi wa Magomano Girls katika KMF 2018 liliambulia nafasi ya tatu kitaifa.

Kubwa zaidi katika maazimio ya Margaret ni kujiendeleza kitaaluma na kuwa mhadhiri wa Kiswahili katika vyuo vikuu. Kwa pamoja na mumewe Bw Isaac Njogu, wamejaliwa watoto watatu. Bw Njogu kwa sasa anafundisha Hisabati na Biashara katika shule moja ya upili iliyoko Nyandarua.

  • Tags

You can share this post!

Barcelona wapiga Villarreal na kufungua mwanya wa pointi 11...

Real Madrid watandika Al-Hilal ya Saudi Arabia na kutwaa...

T L