• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Real Madrid watandika Al-Hilal ya Saudi Arabia na kutwaa ufalme wa Klabu Bingwa Duniani

Real Madrid watandika Al-Hilal ya Saudi Arabia na kutwaa ufalme wa Klabu Bingwa Duniani

Na MASHIRIKA

REAL Madrid walitawazwa wafalme wa Kombe la Klabu Bingwa Duniani (Fifa Club World Cup) baada ya kukomoa Al-Hilal 5-3 mnamo Jumamosi jijini Rabat, Morocco.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), sasa wanashikilia rekodi ya kutwaa Kombe la Dunia mara nyingi zaidi (mara tano).

Real walionyakua ubingwa wa dunia mara nne kati ya 2014 na 2018, sasa wamehakikisha kwamba makala 10 yaliyopita ya kipute hicho yanatamalakiwa na klabu kutoka bara Ulaya.

Vinicius Jr na Federico Valverde walifunga mabao mawili kila mmoja huku bao jingine la Real likijazwa kimiani na Karim Benzema. Al-Hilal walifungiwa na Moussa Marega pamoja na Luciano Vietto aliyetikisa nyavu mara mbili.

Real walifuzu kwa fainali baada ya kutandika Al Alhy ya Misri 4-1 katika nusu-fainali – raundi ambapo mabingwa wa soka ya bara Ulaya huingia kwenye mashindano ya Kombe la Dunia kwa Vilabu.

Al-Hilal, ambao ni wafalme wa soka ya bara Asia, kwa sasa wananolewa na kocha wa zamani wa Oxford United, Ramon Diaz. Walicharaza Flamengo ya Brazil 3-2 katika nusu-fainali na kuwa kikosi cha kwanza kutoka Saudi Arabia kuwahi kuingia fainali ya Kombe la Dunia kwa Vilabu.

Licha ya kufungiwa magoli mawili na Vietto ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa Fulham, Al-Hila walipoteza fursa ya kuwa klabu ya kwanza ya bara Asia kuwahi kunyanyua Kombe la Dunia.

Chelsea walitawazwa mabingwa wa dunia mnamo 2022 baada ya kupepeta Palmeiras ya Brazil 2-1 katika fainali iliyofanyika katika Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE). Hata hivyo, hawakuweza kutetea taji hilo mwaka huu kwa kuwa ni wafalme wa mabara na mabingwa wa soka katika nchi inayoandaa fainali (mwenyeji) pekee ndio hualikwa kushiriki kipute hicho.

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) lina mpango wa kubadilisha utaratibu na muundo wa kivumbi hicho kuanzia Juni 2025 na kuanza kushirikisha timu 32 zitakazokuwa zikiwania ubingwa kila baada ya miaka minne.

Flamengo waliridhika na shaba mwaka huu baada ya kukung’uta Al Ahly 4-2 katika pambano la kutafuta mshindi nambari tatu.

Al Ahly ndicho kikosi cha Afrika kinachojivunia kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa Vilabu mara nyingi zaidi. Mabingwa hao mara 10 wa bara la Afrika waliambulia nafasi ya tatu mnamo 2006, 2020 na 2021.

TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Raja Casablanca kutoka Morocco ndizo klabu zilizowahi kutia fora zaidi katika Kombe la Dunia. Ziliambulia nafasi za pili mnamo 2010 na 2013 mtawalia.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

MWALIMU WA WIKI: Mwalimu kiongozi alengaye uhadhiri

Barobaro amsaka Karen Nyamu awe mpenziwe Valentine’s...

T L