• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
MWALIMU WA WIKI: Mwalimu mbobevu na mtunzi chipukizi

MWALIMU WA WIKI: Mwalimu mbobevu na mtunzi chipukizi

NA CHRIS ADUNGO

MWALIMU ana nafasi kubwa katika kuchochea hamu ya wanafunzi wake kupenda masomo na kufaulu katika safari nzima ya elimu.

Kule kujua kusoma na kuandika tu ni mchango mkubwa wa mwalimu katika maisha ya mtoto; achilia mbali wale wanafunzi wanaofanikiwa kusoma hadi ngazi za juu.

“Walimu wetu, hasa wa shule za msingi na sekondari, ndio waliotujengea msingi imara ambao umetuwezesha baadhi yetu kufikia umbali huu kielimu na maishani,” anatanguliza mwalimu Bonface Ambunya anayefundisha katika shule ya St Martha’s Mwitoti, Mumias, Kakamega.

Kwa mujibu wa Ambunya, yeyote ambaye amesomea kazi ya ualimu anatakiwa kuwa kielelezo chema na anastahili kujiepusha na mambo yatakayomjengea taswira mbaya kwa wanafunzi wake na jamii kwa jumla.

“Mwalimu bora na makini anapaswa kujiheshimu na kuwa mwadilifu. Zaidi ya kuwa mbunifu darasani, anatakiwa kuwa mnyumbufu na tajiri wa mbinu za ufundishaji. Asiwe wa kukariri mambo tu. Ajiandae ipasavyo kwa ajili ya somo lake na ajitahidi kusoma kutoka kwa vyanzo mbalimbali ili aboreshe maarifa yake,” anasisitiza.

Kuwajali na kuwathamini wanafunzi ni sifa nyingine muhimu ambayo Ambunya anashikilia kuwa ni lazima mwalimu awe nayo.

“Wapende na kuwajali wanafunzi wako na ujitume kuhakikisha kuwa wanafaulu katika masomo yao. Washauri mara kwa mara na uwe tayari kuwasaidia kwa hali na mali ili wasiathiriwe kimasomo,” anaelezea.

Bonface almaarufu Bonita Mswahili, alilelewa katika kijiji cha Lubinu, eneo la Mumias, Kaunti ya Kakamega. Ndiye wa nne kuzaliwa katika familia ya watoto sita wa Bi Margaret Were na marehemu Bw Francis Ambunya.

Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Bumwende, Mumias, kabla ya kujiunga na shule ya upili ya St Martha’s Mwitoti, Mumias (2013-2016).

Ingawa alitamani sana kuwa mwanahabari, alihiari kusomea taaluma ya ualimu (Kiswahili/Historia) katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU).

Zaidi ya ualimu, Ambunya amekuwa akichangia makuzi ya Kiswahili kupitia mijadala ya kitaaluma katika vipindi vya lugha redioni, mitandaoni na runinga za KU TV na EDU TV Channel tangu mwaka wa 2021.

Uandishi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani yake katika umri mdogo.

Insha nyingi alizoziandika shuleni zilimvunia tuzo za haiba kutoka kwa walimu wake wa Kiswahili na akawa maarufu mno miongoni mwa wanafunzi wenzake.

Alitunga pia idadi kubwa ya mashairi yaliyofana katika mashindano ya viwango na ngazi mbalimbali na akapata fursa tele za kupanda majukwaa anuwai ya makuzi ya Kiswahili akiwa mwanafunzi wa shule ya upili.

Baadhi ya hadithi ambazo amechangia vitabuni ni ‘Msalaba wa Jinsia’ katika diwani ‘Maisha Karakana na Hadithi Nyingine’, ‘Maiti Mkataa Kaburi’ katika antholojia ‘Ufunguo wa Uhuru na Hadithi Nyingine’ na ‘Chozi la Samaki’ katika mkusanyiko ‘Kitumbua cha Mauti na Hadithi Nyingine’.

Riwaya ‘Dunia Jangwa’ pamoja na hadithi fupi ‘Mwalimu Unaniua’, ‘Taifa Linadondokwa Chozi’ na ‘Nyongo ya Mauti’ ni baadhi ya kazi zake ambazo sasa ziko katika hatua za mwishomwisho za uhariri katika kampuni na mashirika mbalimbali ya uchapishaji wa vitabu humu nchini.

Miongoni mwa mikota wa lugha wanaozidi kumchochea kitaaluma na kumwelekeza vilivyo katika bahari pana ya uandishi wa Kiswahili ni mwalimu Timothy Omusikoyo Sumba na mwanahabari Ali Hassan Kauleni.

Kubwa zaidi katika matamanio ya Ambunya ni kujiendeleza kitaaluma na kuwa profesa wa Kiswahili, mhadhiri wa chuo kikuu na mwandishi maarufu wa kazi bunilizi.

  • Tags

You can share this post!

Wakenya milioni moja wakodolewa macho na njaa

Man-City na Newcastle nguvu sawa katika EPL ugani St...

T L