• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:55 AM
MWALIMU WA WIKI: Mwalimu Simiyu ni dawa mujarabu

MWALIMU WA WIKI: Mwalimu Simiyu ni dawa mujarabu

NA CHRIS ADUNGO

MWALIMU bora anastahili kuwa mwajibikaji na mwepesi wa kuelekeza wanafunzi kimaadili huku akichangamkia vilivyo masuala yote yanayofungamana na mtaala.

Haya ni kwa mujibu wa Bw Abraham Simiyu Wafula ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Idara ya Kiswahili na msimamizi wa masuala ya mitihani katika shule ya msingi ya Namundi FYM iliyoko Lwandanyi, Kaunti ya Bungoma.

“Jukumu kubwa la mwalimu ni kuamsha ari ya wanafunzi katika kusoma na kuandika pamoja na kuwakuza katika stadi za kusikiliza na kuzungumza,” anatanguliza.

“Raha ya mwalimu yeyote aliye na wito wa kufundisha na mapenzi ya dhati kwa taaluma yake ni kuona mtoto aliyeingia shuleni bila kufahamu chochote akipiga hatua kubwa katika safari ya elimu,” anasema.

“Ualimu ni zaidi ya kuwasilisha vipindi vya masomo darasani. Mwalimu anapaswa pia kutambua na kupalilia vipaji vya wanafunzi wake katika fani mbalimbali huku akiwatia moyo wale wasiokuwa wepesi wa kuelewa mambo anayowafundisha,” anaeleza Abraham.

Abraham alilelewa katika kijiji cha Machakha, Sirisia, Kaunti ya Bungoma. Ndiye wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto saba wa Bw Benson Wafula Walucho na Bi Margaret Wekesa.

Alisomea katika shule za msingi za Namubila S.A, Mufungu S.A, Machakha R.C, Ndakaru S.A na Katomei C.P.K zilizoko Sirisia kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Bungoma Boys (2001-2004).

Ingawa matamanio yake yalikuwa kuwa mwanahabari au mhudumu wa sekta ya utalii, alihiari kusomea ualimu katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Kaimosi, Kaunti ya Vihiga (2007-2009).

Baada ya kuhitimu, alianza kufundisha katika shule ya msingi ya Marell Academy iliyoko Bungoma mnamo 2009. Alihudumu huko kwa kipindi kifupi kabla ya kuhamia mjini Nakuru alikofundisha shule za St Cecilia Academy (2010), Kagaki (2011-2014) na Hill Valley (2014-2015).

Alipata pia fursa adhimu ya kuwa mtunzi wa misururu ya ‘Mitihani ya JESMA’ iliyotegemewa pakubwa na shule nyingi za msingi katika eneo la Bonde la Ufa.

Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimwajiri Abraham mnamo Septemba 2015 na kumtuma katika shule ya Namundi FYM. Mbali na Kiswahili, anafundisha pia Hisabati, Zaraa, Sanaa, Kwata na somo la Jamii.

Uzoefu wake katika ufundishaji na utahini wa Kiswahili, umemwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kushauri, kuelekeza na kuhamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa.

Kwa mtazamo wake, siri ya kufanya wanafunzi kuchapukia masomo ni kuwasikiliza, kuelewa changamoto zinazowakabili kisha kuwaelekeza hatua kwa hatua.

“Kufaulu kwa shughuli nyingi za darasani hutegemea ujuzi wa mwalimu, kiasi cha kutangamana kwake na wanafunzi, uelewa wake wa stadi za mawasiliano na wepesi wake wa kubuni mbinu anuwai za ujifunzaji na ufundishaji,” anasisitiza.

Kubwa zaidi katika maazimio ya Abraham kitaaluma ni kujiendeleza kielimu na kuwa mhadhiri wa chuo kikuu. Amekuwa akisomea shahada ya ualimu (Bayolojia/Zaraa) katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) tangu 2019. Anatarajia kufuzu mwakani.

Kwa pamoja na mkewe Bi Benah Nafula Marumbu, wamejaliwa watoto wawili – Bastin Obed na Haggai Barry.

  • Tags

You can share this post!

TALANTA YANGU: Ngoi na msakata densi

Arsenal kuteremkia Oxford kombe la FA

T L