• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:55 AM
TALANTA YANGU: Ngoi na msakata densi

TALANTA YANGU: Ngoi na msakata densi

NA PATRICK KILAVUKA

KUWA ngoi wa nyimbo na kusakata densi ni mambo ambayo alikuwa anayachochea tangu akiwa mdogo.

Hususan wakati alikuwa anahudhuria sherehe au hafla na kuwaona watu wengine wakiongoza nyimbo kwa weledi.

Alifahamu fika kwamba siku yaja ambapo hata yeye atakuwa ngoi na kuwezesha kwaya yake kunogesha muziki katika majukwaa mbalimbali.

Christabel Chogo,13, mwanafunzi wa shule ya msingi ya Thogoto, kaunti ndogo ya Kikuyu, Kaunti ya Kiambu na mwanambee katika familia ya watoto wanne wa Bw David Chogo na Catherine Chogo anasema kiu ya kuwa ngoi ilimsakama mwaka wa 2018 wakati ambapo alikuwa anashiriki katika nyimbo, mashairi na densi.

Wakati huo, alikuwa na takriban miaka tisa hivi na mwalimu wake wa Ibada za Watoto katika kanisa la Thogoto PAG Leah Kutima akawa na mori ya kumuelekeza zaidi.

Mwalimu Lea anakiri kwamba, ungoi wa Christabel si ule wa kuiga bali ni talanta adimu ambayo asili tangu utotoni kwa sababu ni mtu anayependa kufurahi na kutabasamu, hali ambayo humweka sawa katika kuongoza nyimbo hususan za sherehe kuongoa wageni na katika mashindano.

Amekuwa kiongozi wa nyimbo kanisani tangu 2018 hadi leo. Aliwahi kuongoza kwaya ya Ibada za Watoto kushiriki mashindano ya kikao cha Kabete na wakaibuka wa tatu bora katika kitengo chao nyuma Baraka na Kabete.

Aidha, mwanadensi huyu aungama kwamba mamaye amechangia pakubwa katika kunoa makali ya talanta zake kwani kwa zaidi ya miaka mitano, amekuwa akimfuatilia kwa makini sana katika kuongoza nyimbo kwani hata nyumbani, amekuwa akimwekea nyimbo kwenye redio na kumsikiliza akiziongoza na kuzisakata wakati wake wa ziada.

Hii ni hatua ambayo imekuwa ikimpa motisha zaidi.

Aidha, amekuwa akifanya mazoezi ya ziada na mwenzake Assumpta Kanina kabla ya wao kujiunga na kikundi chao kanisani kukiongoza na hata wakiwa shuleni.

Hamasa nyingine ilitokana na mwalimu wake wa kusakata densi Geofrey Witende ambaye anadokeza kwamba, ushauri wake ulimuondolea wasiwasi na akawa sasa anaimarika katika mazoezi kila uchao mpaka wakati alipoanza kupiga shughuli ya kunengua mwaka 2018.

Yeye na kikundi chake walishiriki mashindano katika Kaunti ya Kisumu na wakaibuka wa pili bora.

Christabel anafichua kwamba, bidii, hulka ya kuwa mchangamfu na kupenda muziki ni vigezo ambavyo vimekuwa daraja la ufanisi kwake na sasa yu tayari kuongoza kwaya yoyote ile katika mashindano ya ngazi mbalimbali kwani anachotambua ni kwamba, kujitolea katika kufanya jambo lolote ndiyo ngazi ya kukufikisha katika upeo.

Anasema changamoto kuu ambayo yeye hukumbana nayo ni pamoja na hali kwamba kuna nyimbo nyingine ambazo huhitaji kufuata tamrini zake kwa makini la sivyo mambo huenda mrama!

Isitoshe, mazoezi yafaa yawe kama ibada ili mtu afaulu kuwa ngoi mzuri mbali na kufuatilia wangoi ambao wamekutangulia na wenye uzoefu kwani kujifunza jambo ni safari ambayo haina mwisho.

Siku za usoni Christabel angependa kusomea uhandisi wa kemia hatua ambayo inamsukuma kujitahidi sana kupita katika kila somo kama njia ya kutimiza ndoto yake.

Uraibu wake ni kusakata kabumbu mbali na kutazama runinga kujipatia maarifa na ujuzi wa kunengua na kuongoza nyimbo.

Ushauri wake ni kwamba, unafaa kuwa na malengo ya kuafikia ndoto yako pasi na kukata tamaa. Pia jinoe kila mara, saka ushauri kwa wazoefu unapotatizika na ujifunze kudhamini kila mtu kwani usanii ni mwanya tu wa kuelimisha, kuburudisha na kuhamasisha jamii.

  • Tags

You can share this post!

Wanafunzi 600 kutoka Landi Mawe wanufaika na basari kutoka...

MWALIMU WA WIKI: Mwalimu Simiyu ni dawa mujarabu

T L