• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
MWALIMU WA WIKI: Ni mwalimu na mwandishi ibuka

MWALIMU WA WIKI: Ni mwalimu na mwandishi ibuka

Na CHRIS ADUNGO

ZAIDI ya kufahamu uwezo wa kila mwanafunzi katika masomo mbalimbali, mwalimu anapaswa kuwa rafiki wa karibu wa wanafunzi wake.

Kutokana na usuhuba huo, wanafunzi watakuwa huru kumweleza matatizo yao bila uoga wowote. Mwalimu aliye karibu na wanafunzi wake hutambua kwa wepesi udhaifu wa kila mmoja wao na kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwasaidia na kuwaelekeza ipasavyo katika kila hatua.

Haya ni kwa mujibu wa Bw Stephen Gitau Njau anayefundisha Kiswahili na somo la Dini katika shule ya Munyaka iliyoko Kaunti ya Nyandarua.

“Shughuli za ujifunzaji na ufundishaji zitakuwa nyerezi iwapo mwalimu atasikiliza wanafunzi, kubaini mahitaji ya kila mmoja wao na kushughulikia baadhi ya changamoto zinazowakabili,” anatanguliza Bw Gitau.

“Mwalimu bora anajituma kazini bila kushurutishwa na ni mnyumbufu katika maandalizi ya vipindi vya somo lake. Anaelewa masuala yote yanayofungamana na mtaala na ana msukumo wa kutaka kujifunza mambo mapya.”

“Anastahili kuteka saikolojia ya wanafunzi wake kwa wepesi, kupalilia vipaji vyao na kuwatia moyo wanapotatizika kulimudu somo lake darasani.”

“Wanafunzi wanahitaji mazoezi mengi ili wajiamini katika ujifunzaji wa dhana mpya. Wapewe fursa nyingi za kuhusisha wanachokisoma na matukio ya kawaida katika jamii,” anashauri.

Gitau alilelewa katika eneo la Matunda, Kaunti ya Trans-Nzoia. Ndiye wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto watatu wa Bw Joseph Karuku na Bi Jane Muthoni.

Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Moi Township iliyoko Moi’s Bridge (1992-1999) kabla ya kujiunga na shule ya msingi ya Mathanja, Kaunti ya Kiambu (2000-2002) kisha shule ya upili ya Kiambu (2003-2006).

Ingawa matamanio yake yalikuwa kuwa mwanajeshi, alihiari kusomea ualimu katika Chuo Kikuu cha Makerere jijini Kampala, Uganda (2008-2012).

Alirejea Kenya baada ya kuhitimu na akafundisha katika shule ya Mukuyu, Kiambu (2012-2013) kabla ya kuhamia shule ya Tulaga, Nyandarua (2014-2015). Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimwajiri mwaka wa 2016 na kumtuma kuhudumu katika shule ya Munyaka.

Aliteuliwa kuwa kocha wa handiboli na kandanda shuleni Munyaka mnamo 2016, mwaka mmoja baada ya kusajiliwa kuwa mshambuliaji wa klabu ya Fosa FC inayoshiriki ligi ya North Rift kutoka Nyandarua.

Zaidi ya ualimu, Gitau pia ni mwandishi stadi wa vitabu vya Kiswahili. Alifyatua riwaya ‘Malipo ya Usaliti’ akiwa mwanafunzi wa chuo kikuu mnamo 2010. Vitabu vingine ambavyo amechapishiwa kufikia sasa ni ‘Jitathmini Katika Karatasi ya Pili’ (2016), ‘Tukienzi Kiswahili’ (2016) na ‘Tujifunze Fasihi Simulizi’ (2020).

Mbali na kuchangia hadithi ‘Mchelea Mwana Kulia Hulia Mwenyewe’ katika antholojia ya ‘Nchi ya Miiba na Hadithi Nyingine’, ana mswada wa diwani ya mashairi uliopo katika hatua za mwishomwisho za uhariri.

Kubwa zaidi katika maazimio yake ni kujitosa kikamilifu katika sanaa ya uandishi na kutoa vitabu vitakavyobadilisha sura ya ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili ndani na nje ya Afrika Mashariki.

You can share this post!

Gretsa kuhamisha makao kutoka Thika hadi Makuyu

WANTO WARUI: Wazazi wasaidie watoto wao kukubali na...

T L