• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 5:46 PM
NASAHA: Ipe mipango yako ya kiakademia kipaumbele ili upate ufanisi

NASAHA: Ipe mipango yako ya kiakademia kipaumbele ili upate ufanisi

Na HENRY MOKUA

WIKENDI iliyopita nilimzuru jamaa yangu fulani kushauriana naye kuhusu mradi fulani aliokuwa anauwazia.

Niliwahi mapema ili nimfae kwani amekuwa wa msaada kwangu mara si moja.

Dakika kadhaa baada ya kuwasili kwake, aliingia mhandisi ambaye alimtarajia kuushughulikia mradi alioupangia.

Alishauriana na mhandisi wake nami nikatoa mchango wangu wa maoni baadaye.

Muda ulisonga taratibu nikizidi kujihakikishia ningekiwahi kikao nilichonuiwa kukihutubia baadaye siku hiyo.

Hatimaye niligundua nimeelekea kuchelewa, naye mwenyeji wangu ananishawishi nimsubiri tuondoke pamoja. Hatimaye alinifikisha pa kujiandalia kuenda kikaoni.

Licha ya kujaribu kukiwahi kikao, nilichelewa.

Mara si haba, tunajikuta katika hali sawa na hii ambapo tunajaribu ‘kurudisha mkono’ kwa wenzetu kutokana na mema waliyotutendea.

Hata hivyo, kuna wakati tunajiumiza pasi na kutarajia.Je, wewe mwanafunzi umehusika mara ngapi katika hali kama hii? Ni mara ngapi umeingia katika kundi la marika wako gumzo likashika kasi mpaka ukasahau mipango yako mingine? Nakisia yamewahi kutokea. Si vibaya kushukuru, si vibaya ‘kurudisha mkono’… lakini mipaka ni muhimu.

Changamoto kubwa hutokea nyumbani hasa wakati wa likizo.

Nimewasikia wazazi wengi wakilalamika kwamba wanao wanatumia muda wao mwingi kucheza na kujishughulisha na marika wao huku wakipuuza wajibu wao kiakademia.

Kinachotokea aghalabu ni mwanafunzi kushawishiwa na rafiki zake akanywea katika mipango yao na kusahau kwamba kuna ya mno yanayomhitaji.

Unahitaji kuukumbatia ubinafsi kwa kiasi fulani ili kujikuza na kujiendeleza. Wazia kuifuata mikakati yako ya kiakademia vyema zaidi kuanzia sasa.

Hakikisha kwamba gumzo halikuteki kiasi kwamba unaiacha mikakati yako ididimie.

Njia mojawapo ya kulihakikisha hili ni kuungana na mwenzako, wenzako wenye nia sawa na yako ili mkumbushane mara kwa mara kwamba mnapaswa kuutumia muda wenu kwa makini zaidi ili mjifae.

Athari

Muda mfupi mfupi huu unaoupoteza na kudhani hautakuathiri una uwezekano mkubwa wa kukuvurugia mambo.

Nina mazoea ya kuwaambia wanafunzi wangu na wale nipatao fursa ya kuwahutubia kwamba nusu alama katika somo moja inatosha kumvusha mwanafunzi hadi chuo kikuu au kumsaza.

Si kwamba kujiunga na chuo kikuu ndiyo njia hakika au ya pekee ya kufanikiwa maishani; hata ikawa chuo cha kadri, matakwa ya msingi yapo – kuyapata au kuyakosa wakati mwingine ni tofauti ya nusu alama tu.

Nusu alama hii ndiyo hupotea wakati ukikawia mahali fulani kwa kusudi la kumfurahisha mwenzako.

Msimamo mkali ni muhimu katika kuitunza mikakati yako ichipuke na katika kuipalilia ikue!

Unapoona kwamba mwenzako anakushawishi udumu naye zaidi wakati ukihisi kwamba ni wakati wako wa kuondoka kuyashughulikia mengine, kuwa imara, jiondokee! Huenda wenzako wakakuona kama unayejifanya lakini hatua hii ni muhimu kwako.

Kuanza kuna mambo yake lakini itabidi uanze katika mkondo huu mpya. Anza taratibu kujitoa kwenye vikao au shughuli zinazokukawisha au kukuzuia kuyatekeleza mambo ya ya msingi uliyoyapanga.

Hatua kwa hatua utagundua kwamba umejizoeza kujiondoa popote pale wakati wa shughuli muhimu unapohitajika.

Ushikwapo shikamana! Mwombe mwenzako akusaidie kuyakuza mazoea haya ya kuzingatia muda.

Wapo wanafunzi ambao ni wazuri tu katika kutunza muda, mkabili mmoja wao umshawishi kukufaa katika kuhakikisha unajifunza kutoka kwake. Andamana naye kwa muda ili ujifunze jinsi ya kuutunza muda.

Taratibu, mambo yataanza kukutengenea na baada ya kipindi kifupi utaanza kupiga hatua za haja kiakademia na maishani kwa jumla.

You can share this post!

Shaqiri atia saini mkataba wa miaka mitatu kambini mwa Lyon

KINA CHA FIKIRA: Kiswahili kitukuzwe kwa vitendo badala ya...