• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:02 PM
NDIVYO SIVYO: Tofauti iliyopo baina ya maneno ‘moyo’ na ‘roho’

NDIVYO SIVYO: Tofauti iliyopo baina ya maneno ‘moyo’ na ‘roho’

LUGHA za kwanza hukumbwa na utata katika kupambanua msamiati ‘roho’ na ‘moyo’.

Waama, katika lugha hizo, halipo neno moja linaloweza kutumiwa kuitajia dhana ‘roho’ japokuwa hii ndiyo sehemu inayohimili uhai wa viumbe.

Kutokana na utata huu, baadhi ya watu huzikanganya dhana hizi katika mawasiliano yao.

Aghalabu, neno ‘roho’ hutumiwa katika mazungumzo ambayo yanapasa kulitumia neno ‘moyo’.

Mathalani, katika mojawapo ya mahojiano ya runinga kuhusu afya, nilimsikia kijana mmoja akimweleza mwanahabari aliyekuwa akimhoji kwamba anaendelea kupata nafuu baada ya kufanyiwa upasuaji wa roho! Hiyo haikuwa mara ya kwanza kulisikia neno ‘roho’ likitumiwa visivyo katika mazungumzo.

Lenyewe hujitokeza katika kauli kama hizi: ‘Nimekufa roho’ au ‘Jipe roho’.

‘Roho’ ni sehemu ya kiumbe isiyoonekana kwa macho inayompa uhai. Neno lenyewe aidha huhusishwa na tabia ya huruma na wema. Mtu mwenye hulka hizi husemekana kuwa na ‘roho safi’. Sehemu au kitu kilicho muhimu katika kuendeshea jambo husemekana kuwa ‘roho’ ya jambo hilo. Mathalan, injini ni ‘roho’ ya gari. Waumini wa dini ya Kikristo huamini kuwapo kwa Roho Mtakatifu ndani ya Mkristo ambaye huielekeza dhamiri yake licha ya kutekeleza majukumu mengine muhimu ya kiungu.

Waafrika, Wakristo, Wahindi, Waislamu miongoni mwa waumini wengine wanasadiki kuwapo kwa ‘roho safi’ na ‘roho wachafu’ ulimwenguni.

Kazi ya ‘roho wachafu’ ni kusababisha usumbufu au mateso kwa binadamu ilhali ‘roho safi’ huleta bahati njema.

Zipo nahau mbalimbali zinazozunguka dhana hii na ambazo aghalabu hujitokeza katika mazungumzo.

YATAENDELEA

  • Tags

You can share this post!

Kaunti yapigwa breki kuchota mabilioni ya Bandari ya Mombasa

Kiswahili na Viswahili: Je, kuna haja au hatari yoyote ya...

T L