• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
HUKU USWAHILINI: Hata sisi tumepigwa na hii corona, haijakuwa mchezo

HUKU USWAHILINI: Hata sisi tumepigwa na hii corona, haijakuwa mchezo

Na SIZARINA HAMISI

HUKU Uswahilini janga la corona halijatupita kando.

Ingawa wengi ni wabishi wanaposhauriwa kujikinga na janga hili, matukio ya hivi karibuni yamefanya baadhi ya majirani wavuruge mahusiano.

Mmojawapo akiwepo mama pashkuna ambaye aliwapiga marufuku wanae wasiende nyumba ya jirani yake sababu waliugua corona.

Habari za kuugua kwa majirani zilisambaa mtaa mzima na wengi walihepa kuwasogelea kwa muda wa karibu wiki tatu.

Baada ya muda huo, majirani walirudi kwenye shughuli zao na kuendelea na maisha.

Lakini huku Uswahilini waliwekewa alama kwamba ni waugua corona. Mtaani wakawatenga katika kila shughuli na hata watoto wakazuiwa kukaribia nyumba yao.

Wanasema usilolijua ni kama usiku wa giza. Na sababu nina uelewa kiasi kuhusu janga hili, nikajipa jukumu la kumuelimisha mama pashkuna jinsi virusi vya corona vinavyoambukizwa na iwapo mtu akiugua ugonjwa huu na akapona, anaweza kuwa ni tisho kwao.

Nikamwuliza kisa cha kuwapiga marufuku wanae wasiende kwa jirani yake, akaniambia bila kupepesa macho, kule kuna corona, wanangu wataambukizwa wakienda nyumba ile.

Nikamwuliza zaidi anieleze anavyoelewa kuhusu kuambukizwa kwa ugonjwa huo.

Akaniambia, “Si ukimkaribia mtu anayeumwa na wewe unaupata ugonjwa.”

Nikataka kuelewa zaidi uelewa wake, nikamwuliza na mgonjwa akipona bado anaweza kumwambukiza mtu mwingine?

Bila kusita, akaniambia “Ndio, ugonjwa wenyewe si wa kuambukiza ambukiza tu. Watoto wangu wala mimi siende karibu yao wale, wote wanaambukiza”

Sababu naelewa mambo yetu huku kwetu, nikachukua muda kidogo ili nimuelimishe kwamba mtu akiugua na akipona, hawezi kumuambukiza sababu hana tena maambukizo ya virusi.

Itachukua muda kuelimishana, kwani hii dhana imeenea miongoni mwetu.

Nikakumbuka hata huko kwa wadosi nakofanya kazi, pia kuna unyanyapaa kwa wanaougua na kupona corona.

Nikakumbuka jinsi nilivyotengwa na kupatiwa maelekezo nisiwakaribie mabosi kwa mwezi mzima hata baada ya kupimwa na kuhakikishiwa ni salama.

Wale majirani waliougua nao nikataka nijue upande wao maisha yamekuwaje.

Na kama nilivyotabiri, mzee wa mwenye boma akaniambia nia ya kuhama mtaa, sababu hakuna anayetaka kuhusiana naye sababu aliugua pamoja na familia yake.

“Huu mtaa nitahama, maana wananitenga na kunibagua sababu nimeugua.” Akaniambia mzee wa boma.

Jamani, wenzangu wa Uswahilini, msitenge mtu aliyeugua na kupona corona.

Mjikinge kwa kuvaa barakoa na kuosha mikono mara kwa mara. Halafu hizi ngoma za mfululizo, pumzikeni nazo wakati huu.

[email protected]

You can share this post!

Mwanamme afariki baada ya kudungwa kisu na majambazi South B

MALEZI KIDIJITALI: Muda kwa mitandao usipite saa 1 kwa siku

T L