• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
PENZI LA KIJANJA: Ukiweka azimio la ndoa kuwa kwenye mali, utajuta

PENZI LA KIJANJA: Ukiweka azimio la ndoa kuwa kwenye mali, utajuta

NA BENSON MATHEKA

NI mwaka mpya na watu wako na maazimio mapya ya maisha yao ya mapenzi.

Kwa Sheila, mwaka jana alikosa kutimiza azimio lake la kuolewa baada ya mchumba aliyemwekea matumaini kumtema.

“Sitaki kurudia kosa la mwaka jana na mwaka huu nimeamua kuacha kila kitu kuchukua mkondo wake,” asema Sheila ambaye atagonga umri wa miaka 30 Juni 3 mwaka huu.

Sheila hayuko peke yake, Dennis, barobaro mwenye umri wa miaka 28 alichezewa shere na demu aliyevuruga maazimio yake ya mwaka jana na mwaka huu ameamua kutoweka maazimio yoyote.

“ Yaliyonipata mwaka jana, yamenifunza kumtumainia Mungu pekee katika mipango yangu. Imagine kuachwa na demu baada ya kukamilisha mipango yote ya ndoa. Inavunja moyo sana,” asema Dennis.

Kulingana na wataalamu wa masuala ya mahusiano, Sheila na Dennis wanawakilisha idadi kubwa ya watu wanaoamua kutoweka maazimio ya mapenzi mwaka mpya kwa sababu ya kuchezewa shere na wachumba waliovuruga mipango yao.

“Ukweli wa mambo ni kuwa ulimwengu wa mapenzi umejawa na udanganyifu wa hali ya juu na kutoaminiana. Watu wanawavunja moyo na kuvuruga mipango ya maisha ya wengine wakijifanya wapenzi wa dhati na kuwatema dakika za mwisho,” asema Isabela Samuel, mtaalamu wa masuala ya mahusiano wa kituo cha Maisha Mema jijini Nairobi. Isabela anasema mtu anapomchezea shere mwingine na kumuacha dakika za mwisho huwa anamtumbukiza katika hali tata sana.

“Kuna wale wanaozama katika mfadhaiko na kuchukia maisha ya mapenzi. Kuna wanaoamua kulipiza kisasi kwa mbinu hatari na kuna wanaosahau na kusonga mbele na maisha. Hivyo basi, kabla ya kuazimia kuoa mwaka huu, hakikisha kuwa unayetaka awe mwenzio wa maisha ni mtu atakayesafiri nawe hadi mwisho,” asema Isabela.

Kulingana na mshauri huyu, baadhi ya wanaowatema wachumba wao dakika za mwisho, huwa hawajakata kauli kufunga pingu za maisha au huwa wanagundua kitu ambacho hawakuwa wameona katika wanaowaacha.

David Opasu, mwanasaikolojia katika kituo cha Life Center, Nairobi anasema kuwa maazimio ya mapenzi ya mwaka hasa kuhusu ndoa, yanafaa kutegemea hisia za dhati za mapenzi na sio mwonekano, mali, kazi au sura.

“Mambo haya huwa yanatoweka na ikiwa unaweka mipango yako kwa mtu kwa sababu ya kazi, pesa, umbo au gari lake, kuna hatari ya kuvunjwa moyo. Mali na kazi huwa zinaisha na ikiwa hisia za mapenzi zinakitwa kwa hali hizi, basi kuna hatari ya kuachwa,” asema.

Njia ya pekee ya kuhakikisha azimio la ndoa limeafikiwa ni likifanywa pamoja na wahusika wote, kupangwa na kudumishwa kwa heshima ya hali ya juu, asema Isabela.

You can share this post!

FATAKI: Wanawake walio mamlakani wasiogope kupambana na...

BAHARI YA MAPENZI: Huwezi kuepuka, pesa ni muhimu katika...

T L