• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Ukitumia fomula za wanaojifanya wajuaji utaua penzi lako kwa umpendaye

Ukitumia fomula za wanaojifanya wajuaji utaua penzi lako kwa umpendaye

NA BENSON MATHEKA

JE, unadhani mpenzi wako hakupendi kwa dhati kwa sababu amekubania asali hadi usiku ambao mtaoana rasmi?

Unadhani ni mshamba kwa kuwa hakupigi mabusu moto moto na kukudekeza wafanyiwavyo watu wengine na wapenzi wao hadi uwe mkewe au mumewe rasmi?

Umesikia watu wakidai kwamba kuoa au kuolewa na mtu kabla ya kuonjeshana asali ni sawa na kununua gari bila kulifanyia majaribio ili kubaini iwapo injini yake inanguruma vyema?

Usiamini hekaya hizi. Zinapotosha.

Kuonjeshana asali hakumaanishi mtu anakupenda na madai kwamba anayekubania asali huenda ana dosari au wapenzi wengine wanaomburudisha ni injili ya shetani.

“Nimeona watu wengi ambao hupigana busu la kwanza siku ya harusi na kuonjeshana asali usiku wa kwanza wa fungate na kuwa na ndoa imara yenye furaha. Wanachopaswa kujua wanaoingia katika uhusiano wa mapenzi ni kuwa, kulishana uroda hakumaanishi watu wanapendana,” asema Chris Igwala, mshauri katika shirika la Palace of Peace Christian Outreach Worldwide.

“Kudekezana nje ya ndoa sio mapenzi. Kama uroda ungekuwa muhuri wa mapenzi, basi makahaba wangekuwa watu wanaopendwa zaidi ulimwenguni. Hawangekuwa kwenye biashara.”

Anasema uongo wa aina hii ni sawa na porojo kwamba kuoa mapema au kuchelewa, kunanyima au kuhakikishia mtu furaha katika ndoa.

“Kuoa mapema au kuchelewa maishani sio hakikisho la kuwa na ndoa imara. Unaweza kuoa mapema au kuchelewa maishani na ujute. Hivyo basi, kilicho muhimu ni umakinifu, bidii na kujitolea kuhakikisha ndoa inafaulu,” asema Igwala.

Anasema kuna watu wanaooa au kuolewa wakiwa na umri wa miaka 25 na kujenga ndoa imara huku wengine wakianza maisha ya ndoa wakiwa na miaka 39 na kukosa kuidumisha.

“Ukweli ni kwamba umri sio ukomavu. Ukiwa na zaidi ya miaka 18 na uhisi kwamba uko tayari kuoa au kuolewa pasi kulazimishwa, usijifungie lakini usioe kwa sababu ya raha ya tendo la ndoa pekee, kuwa na malengo, chagua vyema na ufanye uamuzi wa busara,” asema.

Igwala anaonya vipusa na mabarobaro.

“Usiolewe au kuoa mtu unayetilia shaka mienendo yake ukidhani utamfanya abadilike. Wewe sio roho mtakatifu uweze kubadilisha moyo na tabia za mtu. Hauwezi kubadilisha mtu. Akiwa na tabia ambazo unahisi hauwezi kuzivumilia katika ndoa, usimvumilie kama mpenzi wako,” anashauri Igwala.

Katika ulimwengu ambao michepuko imekuwa kama mtindo, mshauri huyu anasema kuna watu wanaokwepa hulka hiyo.

“Usiogope ndoa kwa sababu ulimwengu umejaa michepuko ukihofia mtu wako atakusaliti. Kuna wanandoa wa miaka mingi ambao wamekuwa waaminifu kwa waume na wake zao,” asema.

  • Tags

You can share this post!

Naibu Rais asifia juhudi za Ruto kujitolea kuwekeza katika...

Sheria mpya ya KPLC: Kila ploti kuwa na mita moja pekee  

T L