• Nairobi
  • Last Updated April 12th, 2024 4:55 PM
Vidonge vya kuongeza nguvu za kiume ni njia ya kujipeleka mapema kaburini

Vidonge vya kuongeza nguvu za kiume ni njia ya kujipeleka mapema kaburini

NA BENSON MATHEKA

VISA vya wanaume kufariki kwa kumeza vidonge vya kuongeza nguvu zao kiume ili kutamba chumbani vimeongezeka.

Azma ya kuonyesha vipusa ubabe wa tendo la ndoa imekuwa ikiwaelekeza wanaume kaburini na kuwaacha vipusa wanaowania kuonyesha ustadi wao chumbani wakiendelea kufurahia maisha.

Kilicho wazi ni kuwa wanaotumia vidonge hivi hawafahamu madhara yake na iwapo wanafahamu wanayapuuza.

Wengi wanaovitumia ni mabarobaro wasio na matatizo yoyote ya kiafya na hawafai kuvitumia.

Wanachotaka ni kuonyesha vipusa ubabe wao wa kutekeleza tendo la ndoa.

Vinapaswa kutumiwa kwa ushauri wa daktari na watu ambao wamefanyiwa uchunguzi wa kimatibabu.

Kulingana na jarida la mtandaoni la Journal for sexual health, baadhi ya vidonge ambavyo watu wananunua madukani wakinuia kuongeza nguvu za kiume ni hatari kwa maisha yao.

Utafiti wa wanasayansi wa jarida hilo, unasema matumizi mabaya ya vidonge hivyo yanatokana na ukosefu wa uthibiti na tamaa ya mabarobaro kupotoshwa na wanayoiga katika mitandao ikiwemo mitandao ya ponografia.

Wataalamu wanasema vidonge vinavyouzwa mitaani kuamsha hanjamu ni hatari.

Vikitumiwa kiholela, wanaeleza, vinasababisha maradhi ya moyo, figo na ini.

“Inasikitisha vijana wa umri wa miaka 20 wanatumia vidonge vya kuongeza nguvu za kiume. Hii inaonyesha kuwa watu wana matatizo ya kisaikolojia kwa sababu tendo la ndoa ni la kisaikolojia. Mabarobaro wanaotumia vidonge vya kuongeza uwezo wao wa kufanya mapenzi wanajiweka katika hatari ya kufupisha maisha yao,” asema Dkt Robert Kiinga wa hospitali ya Aga Khan.

Na wanasaikolojia wanalaumu vipusa kwa kufanya wanaume kumeza vidonge hivi.

Doreen Mwangi, mwanasaikolojia katika shirika la Big Hearts, Nairobi, anasema wanaume wengi wanatumia vidonge vya kuongeza nguvu za kiume kutokana na shinikizo za wachumba wao.

“Wanawake wanatarajia mengi kutoka kwa wanaume ambao ili wasidharauliwe au kutemwa na wachumba wao, wanaamua kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume ambazo huwaelekeza kaburini mapema,” asema.

Doreen anahusisha hali hii na habari za kupotosha ambazo kizazi cha sasa kinapata kwenye mitandao.

“Kuna habari nyingi za kupotosha siku hizi kuhusu tendo la ndoa kwenye mitandao. Zinapotosha wanaume na wanawake. Kuna matangazo kila mahali kuhusu vidonge vya kuongeza nguvu za kiume na za kufanya mtu achangamkie tendo la ndoa, ambayo yamefanya watu kutamani yasiyowezekana chumbani,” aongeza Doreen.

Kulingana na wataalamu, vidonge vya kuongeza nguvu za kiume vinaweza kupokonya mtu uwezo wake asilia wa kutekeleza tendo la ndoa.

“Vinafanya mtu kuwa mtumwa wa kuvitumia ili kutamba chumbani huku akiharakisha safari yake kuelekea kaburini. Asipopata mshtuko wa moyo, vinaharibu figo zake,” asema Dkt Kiinga.

  • Tags

You can share this post!

Afueni Kilifi ikipata mahakama mpya

Mwakwere atawazwa kuwa msemaji rasmi wa jamii ya Wadigo

T L