• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
PAUKWA: Madhila aondoka kwa Kizito mzito wa moyo

PAUKWA: Madhila aondoka kwa Kizito mzito wa moyo

NA ENOCK NYARIKI

MADHILA aliondoka nyumbani kwa bwana wake bila kusema ‘buriani’.

Hasira zilizomjaa na kumpwa zilimfanya asizisikie salamu za Bi Kizito ambaye alikuwa amejitokeza ili kumuaga.

Hakuzisikia sauti za Wila na Mila, pacha wa mwajiri wake, ambao walimpungia mikono kupitia dirishani. Mabinti hawa wawili walikuwa vipenzi wa Madhila.

Majirani wangesema nini iwapo wangemwona amerudi mikono mitupu baada ya miaka na mikaka ya ‘kumezwa’ na jiji?

Mkewe na watoto wangempa makaribisho ya aina gani baada ya kipindi kirefu cha kutowatumia chochote cha kuwaauni kwa njaa?

Mawazo yalizagaa kichwani mwake mithili ya jeshi la siafu. Aliona miaka yote aliyotumika kwa Bwana Kizito kama iliyoyeyuka katika hewa yabisi.

Mawazo yake yalikatizwa na matone mawili mazito ya mvua yaliyoanguka kwenye mianzi yake ya pua. Kutahamaki, ilifuata mvua iliyokunya kidindia. Kwa kuwa alipokuwa amefika palikuwa mbali na makazi ya watu, mvua iliishia mwilini. Kifurushi alichokibeba kilikuwa kizito baada ya kuloa maji rovu rovu. Kicha kilichokuwamo kilikifanya kuwa kizito zaidi.

Mto Mtatago unaokigawa kijiji chao cha Pangupakavu na Madongoinama ulikuwa umefurika furi na kulifunika daraja dogo la miti. Kwa hasira, Madhila alikitoa kicha cha funguo mkobani na kukivurumisha kwa nguvu kuelekea majini.

Kisha, aliikunja suruali yake na kujitosa mtoni ili kuvuka kuelekea ng’ambo ya pili. Kijiji cha Pangupakavu kilikuwa kimepitia mabadiliko mengi ya hali ya hewa yaliyomfanya kukata tamaa.

HADITHI ITAENDELEA

  • Tags

You can share this post!

Kang’ata kujua hatma yake ya ugavana leo Jumatatu

WANDERI KAMAU: Ruto, Raila wachezea Wakenya karata hatari...

T L